Charles James, Michuzi TV
KATIKA mwaka wa fedha 2018/19 mamlaka 126 za Serikali za Mitaa zilipanga kukusanya mapato jumla ya Sh Bilioni 463.95 kutokana na vyanzo vya ndani, mamlaka hizo zilifanikiwa kukusanya Sh bilioni 342 hivyo kuwa na upungufu wa Sh bilioni 121 sawa na asilimia 26 ya bajeti yote.
Kwenye mwaka huo wa fedha ulioisha Junior 2019, mamlaka 182 za serikali za mitaa zilipokea jumla ya ruzuku ya maendeleo sh bilioni 913.6 hata hivyo fedha zilizotumika ni sh bilioni 655 na kubaki na jumla a sh bilioni 258 sawa na asilimia 28 ya fedha zilizopokelewa.
Kushindwa kutumia fedha za miradi ya maendeleo kwa wakati kunakwamisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi kama ilivyokusudiwa.
Hayo yamesemwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere alipokua akitoa ripoti yake ya mwaka wa fedha ulioisha Juni 2019 kwa wandishi wa habari jijini Dodoma leo.
Kichere amesema alifanya ukaguzi katika mamlaka 185 za serikali za mitaa na katika ukaguzi huo alibaini mambo ambayo serikali inapaswa kuyafanyia kazi ili kuboresha usimamizi wa rasimali za umma.
Kuhusu Sh bilioni 17.41 za mapato ya vyanzo vya ndani ambazo hazikupelekwa kwenye miradi ya maendeleo, amesema ukaguzi ulibaini kuwa kiasi cha sh bilioni 109 kilikusanywa na mamlaka 60 za serikali za mitaa ambapo kati ya kiasi hicho, sh bilioni 43.78 kilipaswa kutengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo ikiwa ni asilimia 40 mpaka 60 ili kutekeleza matakwa ya sehemu ya 5.0 ya mwongozo wa maandalizi ya mpango wa bajeti kwa mwaka 2018/19.
Amesema hata hivyo kiasi cha sh bilioni 26 ndicho kilihamishwa kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo na kuacha kiasi cha sh bilioni 17 ambacho hakikupelekwa.
" Wakati wa ukaguzi nilibaini matukio ya udanganyifu yenye jumla ya sh bilioni 1.25 ambayo yanahitaji uchunguzi zaidi. Matukio haya yanaashiria mapungufu katika mifumo ya udhibiti wa ndani inayolenga kubaini na kudhibiti vitendo vya udanganyifu.
Ukaguzi pia ulibaini malipo yaliyolipwa kwa watumishi waliokoma utumishi wao ya kiasi cha sh milioni 167.44 kutokana na sababu mbalimbali kama vile kustaafu, kufariki, utoro kazini au waliofukuzwa kazi. Kati ya kiasi kilicholipwa sh milioni 132.6 ilikua ni malipo ya mishahara na sh milioni 34 ni makato ya watumishi hao," Amesema Kichere.
Sababu ya kutokea mapungufu hayo inatajwa kuwa ni kutokuepo kwa mawasiliano kati ya Mamlaka ya Ofisi ya Rais-Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Hazina kwa ajili ya kufuta watumishi ambao hawapo tena katika utumishi wa umma.
Ukaguzi pia unaonesha mamlaka 19 za serikali za mitaa zilishindwa kutekeleza miradi ya maendeleo iliyopangwa yenye thamani ya sh bilioni 24 kutokana na kutokuletwa kwa fedha kutoka serikali kuu na makusanyo hafifu ya mapato ya ndani. Vilevile miradi yenye thamani ya sh bilioni 1 katika halmashauri 12 haikutekelezwa licha ya fedha kuwepo.
Post a Comment