UWEKAJI wazi wa Daftari la Awali na Uboreshaji wa Daftari Wapiga Kura Awamu ya Pili, unaanza rasmi kesho Ijumaa 17 Aprili, 2020. na kukamilika Mei 4, 2020 kwa Nchi nzima.
Hayo yametangazwa hivi karibuni na Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji mstaafu, Semistocles Kaijage wakati wa mkutano na viongozi wa vyama vya siiasa na wadau wengine kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere, Dar es Salaam.
Jaji Kaijage, amesema kuwa,mazoezi hayo yatafanyika kwa siku tatu (3) tu kwenye kila Mkoa na katika route mbili badala ya route tatu zilizopangwa hapo awali na yatazingatia, wakati wote, tahadhari zinazoshauriwa na Serikali na Wataalam wa afya kuhusu mapambano dhidi ya Corona.
Alitaja mikoa mikoa 12 yenye vituo 2005 itakayoanza katika Route ya kwanza inayoanza kesho Aprili 17 hadi 19Aprili, 2020, kuwa ni:- Arusha, Kilimanjaro, Manyara, Tanga, Mara, Simiyuna Mwanza. Mikoa mingine ni; Shinyanga, Geita, Kagera, Kigoma na Tabora.
Route ya pili itakayoanza Mei 02, hadi 04 Mei 2020, itahusisha Tanzania Zanzibar na mikoa 14 ya Tanzania Bara ambapo vituo vya kuandikisha wapiga kura vipatavyo 2001 vitahusika. Mikoa ya Tanzania Bara itakayofikiwa ni Katavi, Rukwa, Singida, Dodoma, Iringa, Songwe, Njombe, Ruvuma, Lindi, Mtwara, Morogoro, Mbeya, Pwani na Dar es Salaam.
Alitaja vituo vya kuandikisha Wapiga Kura vitakavyotumika katika Awamu hiyo kuwa ni 4,006, badala ya 8,031 tvilivyotajwa hapo awali. Kati ya hivyo, vituo 3,956vitakuwa Tanzania Bara na vituo 50vitakuwa Tanzania Zanzibar.
Aidha Jaji Kaijage amesema kuwa, uboreshaji huo utafanyika katika kila Kata ambapo kutakuwa na Mwandishi Msaidizi na BVR Kit Operator watakaowa na orodha ya vituo vyote katika Kata husika. Watendaji hao watakuwa na uwezo wa kuboresha taarifa za Mpiga Kura yeyote atakayefika kituoni.
Pia, Mpiga Kura atakayefika kituoni ataandikishwa kulingana na kituo atakachopigia kura siku ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu ndani ya Kata husika.
Mpiga Kura ambaye atakuwa amehakiki taarifa zake na kuhitaji kufanyiwa marekebisho ama Mpiga Kura anayehitaji kumwekea pingamizi Mpiga Kura mwingine, atatakiwa kwenda kwenye kituo cha Kata husika kilichopangwa.
Zoezi hili la uwekaji wazi daftari litawahusu Wapiga Kura wote, wakiwemo wale walioandikishwa mwaka 2015 na wale walioandikishwa katika awamu ya kwanza ya Uboreshaji.
Aidha, utaratibu wa kuweka pingamizi kwa aliyeandikishwa utafanyika kwa mujibu wa Kifungu cha 24 (1) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi na kifungu cha 30(1) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa.
Mtu yeyote ambaye jina lake lipo kwenye Daftari la Awali la Mpiga Kura anaweza kuweka pingamizi dhidi ya kuendelea kuwepo kwa jina lake mwenyewe au jina la mtu mwingine yeyote iwapo mtu huyo atakuwa amepoteza sifa za kuwemo kwenye Daftari au amefariki.
Vilevile, pingamizi la Uandikishwaji linaweza pia kuwekwa na Mkurugenzi wa Uchaguzi, Afisa Mwandikishaji au Afisa Mwandikishaji Msaidizi.
Mpiga Kura anayetaka kuweka pingamizi atatakiwa kufika kituoni na kujaza fomu maalum ambayo inafahamika kama Fomu Na. 3B ambayo, pamoja na mambo mengine, itamtaka atoe sababu za kuweka pingamizi hilo.
Mweka Pingamizi anatakiwa kuwasilisha pingamizi ndani ya siku saba (7) kuanzia siku ya mwisho ya Uwekaji Wazi wa Daftari la Awali katika eneo husika. Pingamizi hilo litafanyiwa kazi na Afisa Mwandikishaji au Afisa Mwandikishaji Msaidizi ndani ya siku saba (7) na kisha kutolewa uamuzi.
Uamuzi huo unaweza kukatiwa Rufaa katika Mahakama ya Wilaya na Mahakama hiyo inatakiwa kutoa uamuzi ndani ya siku 14 tangu tarehe ya Rufaa kupokelewa Mahakamani. Uamuzi wa mahakama hiyo ni wa mwisho.
Kimsingi, uwekaji wazi wa Daftari kama ilivyo kwa Uboreshaji wa Daftari utazingatia Sheria za Uchaguzi na Kanuni zilizotungwa chini ya Sheria hizo.
Post a Comment