Featured

    Featured Posts

WAFUASI WA CHADEMA MARUFUKU KUFIKA MAHAKAMANI


MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam imetoa amri kuwa  hakuna shabiki yetote atakayeruhusiwa kuingia mahakamani hapo kusikiliza rufaa iliyokatwa na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake saba kupinga hukumu iliyotolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Jaji Mfawidhi wa Kanda hiyo, Lameck Mlacha ametoa amri hiyo leo Aprili 28,2020 wakati kesi hiyo ilipokuja kwa ajili ya kutajwa.

Amri hiyo imetolewa ikiwa ni njia moja wapo ya kuepukana na mikusanyiko katika kipindi hiki ambacho nchi inapopambana na ugonjwa hatari la Corona .

"Siku ya usikilizwaji wa kesi wanaotakiwa kuwepo ni warufani wenyewe nane, mawakili wao na mawakili wa upande wa wajibu rufani" amesema Jaji Mlacha.

Hata hivyo, Jaji Mlacha amepanga kesi hiyo kuanza kusikilizwa mbele ya Jaji Elvin Mgeta Mei 13, mwaka huu.

Katika rufaa hiyo namba 76 ya mwaka 2020 wakata rufani ni Mbowe, wengine ni Katibu Mkuu wa chama hicho, John Mnyika, Naibu Katibu Mkuu-Zanzibar, Salum Mwalimu,  Mbunge wa Iringa Mjini,  Peter Msigwa, Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko, Halima Mdee (Kawe), John Heche (Tarime Vijijini) na Ester Bulaya (Bunda).

Machi 10, 2020 Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu iliwahukumu warufani hapo pamoja na  Dk Vicent Mashinji aliyehamia CCM mwaka huu akitokea Chadema alikokuwa katibu mkuu.

Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba  aliwahukumu kulipa faini ya Sh milioni 350 au kifungo cha miezi mitano jela baada ya kuwatia hatiani kwa makosa 12 kati ya 13 yaliokuwa yakiwakabili.

Warufani hao kwa nyakati tofauti walilipa faini hiyo na kukwepa kifungo.

Mbowe na wenzake wanapinga
 hukumu iliyotolewa na Mahakama ya Kisutu kwamba imefanya  makosa ya kisheria kufikia maamuzi ya kesi ya msingi bila ya upande wa mashitaka kuthibitisha pasipo shaka.

Wanadai Mahakama ya Kisutu ilikosea kisheria  kushindwa kufanya mchanganuo mzuri kwa kufuata ushahidi uliotolewa.

Pia wanadai mahakama imeshindwa  kuainisha viini vya makosa dhidi ya mashitaka na kuwahukumu bila   kuzingatia utetezi wa washitakiwa.

Wanadai mahakama imeshindwa kuzingatia ushahidi kwa kushindwa kuangalia uwepo au ushiriki wa baadhi ya washitakiwa kwenye mkutano na kuwahukumu kwenye mashitaka ya  2,3 na 4.

 Warufani hao wanadai mahakama hiyo ilikosea kupokea vielelezo vya kielektroniki ambavyo ni video, imekosea kisheria kuzingatia mashitaka ya 11,12 na 13 yamewafanya washitakiwa washindwe kujitetea. 

Mahakama ilikosea kisheria kuangalia maneno yaliyotolewa katika mashitaka ya 5,6,7,8,9,10 kwamba hayawezi kuhesabika kuwa makosa ya jinai kwa mujibu wa maamuzi yaliyotolewa katika kesi ya Hussein Katanga dhidi ya Jamhuri (1974) ukurasa wa 97 wa hukumu hiyo.

Pia wanadai hakukuwa na maelekezo ya awali yaliyofanyika sambamba na  kupuuzwa kwa haki ya uwakilishi.

Wanadai mahakama imekosea katika kutoa adhabu dhidi ya warufani ya  kulipa faini ambayo  ilikuwa inajitegemea wakati adhabu ya kifungo ilikuwa inaenda kwa pamoja hali hiyo imesababisha kuleta mkanganyiko wa kisheria.

Hata hivyo, warufani hao wanaiomba mahakama iamuru hukumu na adhabu iliyotolewa dhidi ya warufani ifutwe.
author

Author Name

Author Description!

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

www.CodeNirvana.in

Magazeti Ya Leo

Copyright © Magazeti ya Leo, Habari Leo Tanzania, Mwananchi, Michuzi, mwanaspoti, nipashe, Udaku | Designed By Code Nirvana