Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amekabidhi magari 10 ya kubebea wagonjwa kwa wabunge ikiwa ni mwendelezo wa jitihada za dhati za Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli za kuhakikisha Watanzania wanapata huduma bora za afya karibu na makazi yao.
Magari hayo 10 ni kati ya magari 50 ya kubebea wagonjwa yenye thamani ya sh. bilioni sita yaliyonunuliwa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kupitia Global Fund. Kati ya magari hayo, 18 yatapelekwa kwenye Hospitali za Rufaa za Mikoa na 32 ni kwa ajili ya hospitali za Halmashauri pamoja na vituo vya afya.
Waziri Mkuu amekabidhi magari hayo leo (Jumatano, Aprili 29, 2020) kwenye viwanja vya Ofisi ya Waziri Mkuu, Mlimwa jijini Dodoma. Ambapo amesema mbali na magari hayo kutolewa kwa ajili ya kuboresha huduma za mama na mtoto pia yatatumika kuwahudumia wagonjwa wa corona ili kuokoa maisha ya wananchi.
“Eneo hili tumeliwekea nguvu za kutosha na Watanzania wote ni mashahidi kwa namna ambavyo Serikali imejitahidi sana katika kupunguza vifo vya mama na mtoto kwenye jamii zetu. Magari haya yatakwenda kutumika kwa ajili ya mama na mtoto lakini kwa kuwa gari litakuwepo kituoni litawahudumia na wagonjwa wengine.”
Waziri Mkuu amewashukuru wabunge wote kwa namna wanavyoishauri Serikali katika kufanya maboresho ya sekta mbalimbali za maendeleo ikiwa ni pamoja na sekta ya afya ambapo leo wameshuhudia matunda ya ushauri wanaoutoa.
“Magari haya yatakwenda kufanya kazi ya kuokoa maisha ya Watanzania wengi kwa kuwasafirisha wagonjwa wa rufaa kutoka kituo cha afya kwenda hospitali ya wilaya na hospitali ya wilaya kwenda hospitali ya rufaa.”
Kwa upande wake, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu amesema ununuzi wa magari hayo ni utekelezaji wa ahadi za Rais Dkt. John Pombe Magufuli za kuboresha zaidi huduma afya kwa wananchi.
Waziri Ummy amesema Wizara imenunua magari hayo ili kuimarisha huduma za rufaa kwa wagonjwa hususani kwa akina mama wajawazito hata hivyo kutokana na changamoto ya ugonjwa wa corona pia magari hayo yatatumika kwa ajili ya kubebea wagonjwa wa corona.
“Watanzania wameshuhuduia kazi kubwa na nzuri inayofanywa na Rais wa Awamu ya Tano, Dkt. John Pombe Magufuli, wameshuhudia upatikanaji wa dawa, wameshuhudia maboresho makubwa katika upatikanaji wa vifaa tiba, ujenzi wa vituo vya afya, ujenzi wa hosptali za halmashauri pamoja na hospitali za rufaa za mikoa na uboreshwaji wa miundombinu ya kutolea huduma za afya.”
Akizungumza kwa niaba ya wabunge waliopokea magari hayo, Mbunge wa Ileje, Janneth Mbenne amemshukuru Rais Dkt. Magufuli kwa kitendo hicho cha kihistoria. “Tunamshukuru Mheshimiwa Rais kwa mawazo na maono makubwa ya maendeleo ya Taifa. Magari haya yatakwenda kuboresha huduma za afya katika majimbo yetu.”
Naye Mbunge wa Kilolo, Venance Mwamoto ameishukuru Serikali ya Awamu ya Tano kwa utekelezaji wa Ilani ya CCM ya 2015-2020 kwa vitendo. “…moyo usio na shukurani hukausha mema yote na heri wale wanaowajali wagonjwa kwa maana ufalme wa Mungu ni wao.”
Pia, Mbunge wa Nyasa na Naibu Waziri wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Stella Manyanya amesema kwa niaba ya wananchi wa wilaya ya Nyasa wanamshukuru Rais Dkt. Magufuli kwa msaada huo kwani walikuwa na changamoto kubwa na gari la kubebea wagonjwa.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU.
Post a Comment