Featured

    Featured Posts

CHADEMA NA ACT NI MAVI YA KALE: MWANANCHI MZALENDO

NA PETER JOHN-Mwananchi Mzalendo
Mimi ni mpenzi wa siasa na niliyefurahishwa sana na siasa za Tanzania, kuanzia chama kimoja yaani kabla ya mwaka 1992 na baada ya kuanza kwa vyama vingi ambavyo uchaguzi wake wa kwanza ulifanyika mwaka 1995.

Naomba nikiri kuwa nilipendezwa sana na siasa za upinzani zilipoanza mwaka 1992, nilifurahishwa na namna wanasiasa kama akina Augustine Lyatonga Mrema walivyokuwa wanajenga hoja na kutoa changamoto kwa Serikali ya Awamu ya Pili ya Mzee Ali Hassan Mwinyi na baadaye serikali zilizofuata za Awamu ya Tatu ya Mzee Mkapa na Awamu ya Nne ya Mzee Kikwete.

Siasa tamu zilichagizwa na wanasiasa mahiri akina Mabere Marando na zikanoga zaidi mwaka 1995 ambapo Mrema alihama CCM na kuingia NCCR Mageuzi. Ndani ya CCM kwenyewe walikuwepo wanasiasa machachari wengi tu ambao wengi wetu tunawakumbuka.

Nasema nilifurahia siasa ambazo zilijikita kwa hoja zenye mashiko. Wanasiasa wa upinzani walishika bango dhidi ya kukithiri kwa rushwa na ufisadi, matumizi mabaya ya mali za umma, kasi ndogo ya maendeleo ya Watanzania. Tulisikia hoja nzito za kuzorota kwa shirika la ndege (ATCL), kusombwa kwa madini na wageni huku wazawa wakiachwa solemba, wakulima kukosa watetezi, hali duni ya miundombinu ya kutolea huduma za kijamii kama vile elimu, afya, barabara, maji, umeme n.k

Kwa hakika Serikali ilikuwa inabanwa hasa hadi unaona upinzani una maana kubwa kwa Watanzania.

Ubora wa upinzania ukaimarika zaidi kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, kazi nzuri iliyofanywa na Dk. Wilbrod Slaa akiwa Mbunge na baadaye Katibu Mkuu wa CHADEMA. Kwa uwezo wake wa kujenga hoja nzito na zenye maslahi mapana kwa Watanzania mwaka 2010 akagombea kiti cha Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, akamhenyesha Mzee Kikwete na kufanikiwa kupata kura nyingi katika uchaguzi Mkuu, japo hakushinda lakini alifanikiwa kuimarisha CHADEMA kwa kupata wafuasi na wanachama wengi na pia kuongeza idadi ya Wabunge.

Dk. Slaa baada ya uchaguzi mkuu wa 2010 akawa Katibu Mkuu wa CHADEMA na akakiimarisha chama vizuri mpaka mwaka 2015 alipokihama chama hicho baada ya Mwenyekiti wake Freeman Mbowe kuibuka na Mgombea wa Urais kutoka CCM Ndg. Edward Lowassa.

Anguko la CHADEMA likaanzia hapo, kwani wapenda mageuzi wengi walimpenda Dk. Slaa kutokana na uwezo wake wa kujenga hoja na dhamira ya dhati ya kuijenga Tanzania. Alikuwa mtu wa utafiti, hoja nzito na aliyeheshimika sana.

Kuondoka kwake CHADEMA kukakiondoa chama hicho kutoka chama chenye hoja za msingi na kuwa chama kinachoendeshwa na matukio. Ajenda haikuwa tena kupambana na wizi, rushwa na ufisadi na badala yake wale ambao walituhumiwa kwa uhalifu huo wakachukuliwa na CHADEMA na kwenda kugombea nafasi za Urais na Ubunge. Wengine wakapewa heshima ya kuwa wajumbe wa Kamati Kuu na wengine Wazee wa chama.

Lazaro Nyalandu waliyedai kafanya ufisadi mkubwa akiwa Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kutumia fedha za umma kula bata na warembo Marekani na Ulaya na kuuza wanyamapori kwa familia za wafalme Saudia na Oman akapewa heshima ya uongozi, Edward Lowassa waliyemtuhumu kwa wizi na kuhusika katika kashfa za Richmond na nyingine kiasi cha kufikia hatua ya kujiuzulu Uwaziri Mkuu akapewa nafasi ya kugombea urais na baadaye mjumbe wa Kamati Kuu, Fredrick Sumaye aliyekuwa akituhumiwa kufisadi ardhi akapewa ujumbe wa Kamati Kuu na wengine wengi waliotoka CCM kwa kashfa.

CHADEMA ikageuka kuwa chama cha kutetea wakwepa kodi, wezi wa rasilimali za umma na kuwa wanaharakati wanaoungana na mataifa ya nje ya nchi ambayo yana nia ya kuikandamiza Tanzania katika maeneo mbalimbali.

CHADEMA sasa wameacha masuala ya maendeleo na sasa wana ajenda za kubumba na za kupika za haki za binadamu, demokrasia na maandamano. 

Tundu Lissu wa CHADEMA na Zitto Kabwe wa ACT Maendeleo wao wamejivika jukumu la kufoka hadi mate yakiwatoka wakitukana Serikali na viongozi wake hasa Rais, wakaanza kupata umaarufu ambao ukamtisha sana Mbowe na huenda alifurahishwa sana na tukio la Tundu Lissu kupigwa risasi.

CHADEMA na ACT Maendeleo vimekuwa vyama vinavyotumiwa na mabeberu na wasioitakia mema Tanzania.

Kwa mwendo wa kudandia hoja CHADEMA na ACT Maendeleo vimedandia hoja ya ugonjwa wa Corona, inawezekana wengi hawajui jinsi vinavyotumiwa katika hoja hii. Vinatumika kuogofya watu. Mbowe na Zitto wanalazimisha Tanzania ifuate maelekezo ya mabeberu, wanataka Watanzania wafungiwe ndani, biashara zifungwe, Watumishi wa Serikali wasiende kazini, huduma zisitishwe, Mipaka ifungwe, makanisa na misikiti ifungwe na wanalazimisha Serikali itoe fedha za kununulia vifaa vya uchunguzi wa Corona bila ya kujali usalama wake. 

Mbowe akawatoa wabunge wa CHADEMA katika vikao vya Bunge kule Dodoma na kukejeli hatua mahsusi zinazochukuliwa na Serikali. Jamaa wanaleta siasa kwenye ugonjwa ambao unahitaji umakini mkubwa kukabiliana nao.

Matokeo yake leo tunashuhudia hata hayo mataifa yaliyokuwa yanawatuma kufanya uchochezi yameanza kubadilika na yanakubaliana na msimamo wa Tanzania na Rais wake Dk. John Pombe Magufuli. Mataifa hayo yameanza kufungua mipaka, kuwaruhusu watu kutembea badala ya kuwafungia ndani.

Nimeshangazwa hata na Ubalozi wa Marekani kutoa tahadhari kwa raia wake waliopo Tanzania, kwamba kuna hatari kubwa ya kupatwa na Corona wakati dunia nzima inajua kuwa Marekani ndio nchi iliyoathirika zaidi kwa idadi ya wagonjwa na vifo.

Nimemshangaa pia Baba Askofu Niwemugizi wa Jimbo Katoliki la Rulenge-Ngara ambaye ameongozwa na mihemko ya kisiasa na kufuata mkumbo kwa kuamua kufunga makanisa, sunday school na Jumuiya. Baba Askofu Niwemugizi ameshindwa kufanya tafakari ya kiimani na kufuata miongozi ya biblia. Sasa sijui siku akifungua Makanisa yake atawaambia nini Waumini ambao tumewasikia wakihuzunishwa na kukosa kufanya ibada katika makanisa waliyoyajenga wao wenyewe.

Haya sasa Shirika la Afya Duniani WHO linasema Corona itabidi tuishi nayo kama UKIMWI, najiuliza Makanisa ya Rulenge-Ngara yatabaki yamefungwa?

Nadhani Baba Askofu atayafungua Makanisa kwa aibu na kuomba watu warudi kusali kisha atatuhubiria Mungu ni mtatuzi wa shida zote. Alisahau hata Makanisa na nyumba anazotumia zimejengwa na Waumini. Lakini kikubwa alisahau kuwa yeye ni Mwakilishi wa Kristu na sio wakala wa Kisiasa au Kiserikali. 

Taarifa za Kitaalamu zilizopo ni kuwa hivi sasa ugonjwa umekabiliwa vilivyo kwa kiasi kikubwa hapa nchini. Taharuki imeisha na kesi za wagonjwa zinapungua. Inawezekana Watu wamejenga kinga (immunity ya mwili) na kupiga nyungu kunasaidia. Lakini pia dawa za Kienyeji na hatua zingine zilizoelekezwa na Wataalamu zimesaidia. 

Kikubwa Mungu aliye juu amesaidia Nchi yetu kama tulivyomuomba tukiongozwa na Rais wetu Mhe. Dr. John Pombe Magufuli. Ni Ushauri wangu kama tulivyoomba sasa Rais ATUONGOZE kumshukuru Mungu. 

Nahitimisha kwa kusema, siasa za upinzani hapa Tanzania kwa sasa ambapo CHADEMA na ACT Maendeleo wanajimwambafai kuwa ndio vinara hazina mvuto tena, imebaki vijembe na matusi, kejeli na vitisho. Hakuna tena nguvu za hoja. Hakuna tena utamu wa siasa.

Tuchape kazi jamani, nchi hii inahitaji maendeeo sio maneno na kuvujana moyo.

Mimi Mwananchi Mzalendo
Peter John
14 Machi, 2020.
author

Author Name

Author Description!

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

www.CodeNirvana.in

Magazeti Ya Leo

Copyright © Magazeti ya Leo, Habari Leo Tanzania, Mwananchi, Michuzi, mwanaspoti, nipashe, Udaku | Designed By Code Nirvana