WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Profesa Palamagamba Kabudi ameweka hadharani barua ya Waziri wa Mambo ya Nje nchini Zambia inayoeleza kwamba mipaka baina ya nchi hizo mbili haijafungwa.
Akizungumza leo Mei 13,mwaka 2020 Bungeni Mjini Dodoma , Profesa Kabudi ametumia nafasi hiyo kueleza kwa kina kuwa Zambia haijafunga mpaka na Tanzania.
" Nataka niwaambie Zambia haijafunga mpaka na Tanzania, narudia tena Zambia haijafunga mpaka na Tanzania ,haya si maneno yangu,ninayo barua kutoka kwa Waziri wa Mambo ya Nje nchini Zambia Joseph Malanji ambaye Mungu amemjaalia kujua lugha nyingi.
"Kwa hapa Tanzania anazungumza kinyakyusa , Kinyiha, Kinyamwanga, na jana na leo tumezungumza kwa Kiswahili. Naomba nisome barua yake japo ni jambo ambalo si la kawaida , ameniandikia barua ambayo imefika leo baada ya kufanyika kwa mazungumzo,"amesema Profesa Kabudi na kisha kuisoma barua hiyo iliyoandikwa kwa lugha ya Kingereza.
Wakati anaisoma barua hiyo Wabunge kadhaa walionekana kufurahishwa na uamuzi wa Zambia wa kutofunga mpaka wake na Tanzania licha ya kuwepo kwa jitihada mbalimbali zinazoendelea kwa kila nchi kukabiliana na Corona.
Profesa Kabudi amefafanua kwa mujibu wa barua hiyo ambayo imefafanua kwa kina kuwa Zambia haijafunga mpaka, imeeleza kuwa Kamati ya timu ya watalaamu kutoka Tanzania na Zambia watakutana kwa pamoja kuweka mambo sawa na kisha huduma kurejea kama kawaida.
"Kwa hiyo hii ndio barua kutoka Zambia imeeleza wazi kabisa haijafunga mpaka ila ilichukua hatua kwa siku tano kusimamisha ile hali ili kukabiliana na hali, na amerudia kueleza kamati ya pamoja ya Tanzania na Zambia zitakutana ili kuweka mambo sawa,"amesema .
Amesisitiza ameona ni vema hilo akaliweka wazi licha ya kwamba sio kawaida kusoma barua bila idhini, hivyo alimuomba Waziri wa Zambia asome barua hiyo ili wale wasioitakia mema nchi yetu waelewee.
Post a Comment