Evariste Ndayishimiye
BURUNDITume ya uchaguzi nchini Burundi imemtangaza mgombea wa chama tawala nchini humo CNDD-FDD Jenerali mstaafu Evariste Ndayishimiye kuwa mshindi wa uchaguzi wa urais uliofanyika juma lililopita.
Jenerali mstaafu huyo ameshinda kwa 68.72% ya kura zilizopigwa, wakati Agathon Rwasa, kutoka chama kikuu cha upinzani akipata 24.19% ,matokeo yaliyotangazwa na tume hiyo hii leo.
Kwa kuwa Ndayishimiye amepata zaidi ya 50% ya kura, ameepuka kufanyika kwa duru ya pili ya uchaguzi.
Haya ni matokeo ya awali ya uchaguzi , ambapo matokeo ya mwisho yatatangazwa na mahakama ya kikatiba tarehe 4 mwezi Juni.
Jenerali Ndayishimiye liteuliwa kupeperusha bendera ya chama cha CNDD-FDD katika kikao kisicho cha kawaida kilichofanyika Gitega, mji mkuu wa kisiasa baada ya mazungumzo yaliyodumu kwa saa tatu ya chama tawala cha CNDD-FDD.
Ndayishimiye ni miongoni mwa wanasiasa mashuhuri katika siasa za Burundi walio karibu na Pierre Nkurunziza, ambaye uamuzi wake wa kuwania madaraka kwa muhula wa tatu kwenye uchaguzi wa mwaka 2015 ulisababisha mzozo na mgomo wa upinzani.
Wagombea wengine waliochuana kwenye kinyang'anyiro hicho ni pamoja na, Gaston Sindimwo (Uprona) - 1.64%,
Domitien Ndayizeye (Kira Burundi) - 0.57%, Léonce Ngendakumana (FRODEBU) - 0.47%, Nahimana Dieudonné - 0.42%, Francis Rohero - 0.20%
Post a Comment