Uamuzi huo wa WHO umefikiwa baada ya ripoti ya wanasayansi iliyochapishwa katika jarida maarufu la kitabibu la The Lancet wiki iliyopita, ikisema matumizi wa hydroxychloroquine yalikuwa yakizidisha hatari ya kufa miongoni mwa wagonjwa wa COVID-19, amesema mkuu wa shirika hilo Tedros Adhanom Ghebreyesus katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika kwa njia ya video jana jioni.
Tedros alisema kile kinachofahamika kama 'mshikamano wa majaribio' kinachohusisha mamia ya hospitali ulimwenguni ambazo zimekuwa zikiijaribu dawa hiyo kwa wagonjwa wa virusi vya corona kimeacha majaribio hayo kama hatua ya tahadhari tu. Mkuu wa huduma za dharura katika shirika la WHO Mike Ryan amesisitiza kuwa hakuna matatizo mengine yaliyojitokeza.
''Uamuzi huu hausiani na matatizo yoyote, hakuna matatizo yaliyojitokeza katika mshikamano wa majaribio, wala hakukuwa na dalili za matatizo,'' amesema Ryan na kuongeza kuwa wameamua hayo kwa sababu ya matokeo ya utafiti wa hivi karibuni, kuhakikisha kwamba majaribio ya kikundi hicho yanafanyika katika usalama wa kutosha.
Kupigiwa debe na Rais Donald Trump hakujasaidia kitu
Tedros amesema wakati majaribio hayo ya hydroxychloroquine yakiwa yamesitishwa, bodi ya kufuatilia usalama wa data ya mshikamano wao wa majaribio, itakuwa ikitathmini kwa kina usalama wa dawa hiyo.
Ingawa dawa hiyo awali ilitumiwa kutibu malaumivu ya misuli, baadhi ya watu, rais Donald Trump wa Marekani miongoni mwao, wamekuwa wakiipigia debe kama tiba kwa virusi vya corona, na nchi kadhaa zimekuwa zikiiagiza kwa wingi. Wiki iliyopita, waziri wa afya wa Brazil alishauri matumizi ya dawa hiyo, pamoja na nyingine ya Chloroquine inayotibu malaria, kwa ajili ya wagonjwa wa COVID-19.
Virusi vya corona vilivyoanzia China mwishoni mwa mwaka uliopita, vimewaambukiza watu zaidi ya milioni 5.5 kote duniani, zaidi ya 350,000 miongoni mwao wakipoteza maisha. Hadi sasa hakuna dawa wala chanjo dhidi ya virusi hivyo.
Tahadhari kwa nchi zinazolegeza vikwazo
Katika mkutano huo na waandishi wa habari, WHO ilitoa tahadhari kwa nchi nyingi ambazo zinaanza kulegeza masharti na vikwazo vya kudhibiti kusambaa kwa virusi vya corona, ikizitolea mwito wa kuendelea kuhimiza watu kutosogeleana, na kuongeza uchukuaji wa vipimo kubainisha walioambukizwa virusi hivyo.
Nchi nyingi za Ulaya, ikiwemo Ujerumani zimetangaza kupunguza hatua kwa hatua vikwazo vilivyokuwa vimewekwa kuzuia kasi ya kusambaa kwa virusi vya corona, kadri maambukizi ya virusi hivyo yanavyoendelea kushuka.
Mtaalamu wa shirika la WHO Maria Van Kerkhove amezishauri nchi hizo kufanya hivyo kwa tahadhari kubwa, ili maambukizi ya virusi hivyo yasipewe fursa nyingine ya kushamiri.
Post a Comment