Na Leandra Gabriel, Michuzi TV
MADAGASCAR imekua nchi ya kwanza barani Afrika kutangaza dawa ya asili inayotibu virusi vya Corona ambapo Rais wa nchi hiyo Andry Rajoelina aliwataarifu wananchi juu ya uimara wa dawa hiyo na Mei 03, 2020 Rais wa Tanzania Dkt. John Joseph Magufuli aliuhakikishia umma juu ya Serikali ambayo hailali kwa Kuhakikisha wananchi wote wanakua salama na kueleza kuwa yupo tayari kutuma ndege nchini Madagascar ili kuleta dawa ambayo itawasaidia watanzania waliopatwa na homa hiyo ya mapafu (Covid -19) inayosababishwa na virusi vya Corona.
Mambo yanayovutia kuhusu Madagascar ni haya;
Inajulikana rasmi kama Jamhuri ya Madagascar, ikiwa nchi ya kisiwa (katika bahari ya Hindi kwa Pwani ya Afrika Mashariki) na ni kisiwa cha nne kwa ukubwa duniani.
Kuanzia mwaka 1895 ilitawaliwa na Ufaransa na ikawa nchi huru 1960 na kuitwa Jamhuri ya Malagasy na baadaye 1975 ikawa Jamhuri ya Demokrasia ya Madagascar na mwaka1993 ikawa Jamhuri ya Madagascar huku Mji mkuu wa Madagascar ni Antananarivo ukiwa na watu wapatao milioni 2.
Lugha rasmi nchini humo Malagasy na Kifaransa, na inakadiriwa kuwa na wakazi zaidi ya milioni 25.
Wananchi wengi wa Madagascar wanaamini katika mizimu na miiko hata katika wakati huu wa sayansi na teknolojia na imeelezwa kuwa wakazi wengi nchini humo ni wakristo (dini ililetwa na wamisionari) lakini bado wanaamini katika nguvu za mababu, uchawi, mizimu na miiko; wengi wao huwazika wapendwa wao katika mapango wakiwa katika majeneza na baadaye kufanya sherehe na masalia ya mifupa hiyo na hata kupiga nayo picha.
Pia imeelezwa kuwa nchi hiyo ina zaidi ya aina 10,000 ya mimea ya dawa asili huku asilimia 90 ikiwa zimefanyiwa utafiti na zinapatikana katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo.
Mlima mkubwa zaidi nchini humo ni Maromokotro wenye mita 2876 na kubwa zaidi ni kwamba viumbe 250,000 vinavyopatikana nchini humo havipatikani sehemu nyingine duniani na hii ni pamoja na mimea ya asili 14,000 inayopatikana Madagascar ambayo haipatikani sehemu nyingine duniani.
Tafiti zinaonesha kuwa asilimia 50 za idadi ya vinyonga duniani wanapatikana Madagascar ikiwa ni pamoja na vinyonga wakubwa zaidi, huku aina 156 za vinyonga wanaopatikana ulimwenguni nusu yake wanapatikana Madagascar.
Pia Madagascar imepambwa na miti ya mibuyu, miti yenye umbo la chupa, miti iliyoelekeza mizizi angani na vivutio vingi vya kiasili.
Post a Comment