Featured

    Featured Posts

MAANDAMANO MAKUBWA KUFUATIA JINAI ZA POLISI WA MAREKANI DHIDI YA WAMAREKANI WEUSI

Pamoja na hayo suala ambalo katika miaka ya hivi karibuni limekuwa likiakisiwa zaidi, ni ukatili usio na ukomo wala mpaka wa polisi wa Marekani dhidi ya Wamarekani wenye asili ya Afrika jambo ambalo limekuwa likitia huzuni kila siku ndani ya nchi hiyo. Katika malalamiko makubwa kufuatia kuuawa mikononi mwa polisi mzungu, Mmarekani mmoja mweusi asiye na silaha katika mji wa Minneapolis, jimbo la Minnesota, mtu mwengine mweusi ameuawa pia kwa kupigwa risasi. Afisa mmoja wa ngazi ya juu wa polisi wa mji wa Minneapolis ameelezea vurugu zilizojiri kati ya waandamanaji na polisi usiku wa Jumatano iliyopita ambapo sambamba na kuonyesha kukatishwa tamaa alisema kuwa, usiku huo ulitofautiana na usiku wa kabla yake. Kufuatia vurugu hizo, Jacob Frey, meya wa mji wa Minneapolis amewataka wakazi wa mji huo kutoruhusu mauaji ya George Floyd, Mmarekani mweusi aliyeuawa na polisi, kusababisha mauaji zaidi. Maandamano hayo yaliyosababisha umwagaji damu ni radiamali ya msururu wa ukandamizaji, dhulma, na zaidi ya yote, ukatili usio na ukomo wala mpaka wa polisi wa Marekani dhidi ya Wamarekani weusi. Jinai mpya ya polisi wa nchi hiyo dhidi ya Wamarekani weusi imewaitia wasi wasi na hofu kubwa Wamarekani na pia watu wa nje ya mipaka ya nchi hiyo.
Namna George Floyd alivyouawa kinyama na polisi katili mzungu
Hii ni baada ya polisi mmoja siku ya Jumatatu kumuua kwa namna ya kutisha George Floyd, rais mweusi mwenye umri wa miaka 46 katika mji wa Minneapolis, jimbo la Minnesota. Inaelezwa kuwa Jumatatu jioni Floyd alikumbwa na ukatili wa polisi mzungu ambapo akiwa amefungwa mikono alilazwa chini kifudifudi. Polisi wanadai kwamba Floyd alikuwa na matatizo ya kiafya na kwamba alifariki dunia baada ya kufikishwa hospitali. Hii ni katika hali ambayo video zilizosambazwa mitandaoni za watu walioshuhudia ukatili huo zinamuonyesha raia huyo akiwa amekandamizwa ardhini kwa namna ya kutisha na goti la kushoto la polisi kwenye shingo lake huku akipiga kelele za kuomba msaada akisema: "Siwezi kupumua." Hata Jacob Frey, meya wa mji wa Minneapolis amelitaja tukio hilo kuwa kashfa kubwa kwa kusema: "Kuwa mtu mweusi nchini Marekani hakupasi kuwa sababu ya kutolewa hukumu ya kifo. Nimeona kwa dakika tano afisa mweupe akiwa amebana shingo la mtu mmoja mweusi kwa goti lake." Nalo gazeti la Washington Post limeitaja taarifa ya polisi kuhusiana na tukio hilo kwamba eti 'ni kifo cha mtu aliyekuwa na matatizo ya kiafya akijaribu kukabiliana na polisi' kuwa ni ya kuchekesha. Naye Nancy Pelosi, Spika wa Bunge la Wawakishi la Marekani amezungumzia ukatili wa hivi karibuni wa polisi dhidi ya raia wa nchi hiyo mwenye asili ya Afrika kwa kusema: "Hili ni janga. Hii ni jinai. Ninaisikitikia sana familia yake na pia wakazi wa huko." Itakumbukwa kuwa miaka sita iliyopita, Mmarekani mwingine mweusi kwa jina la  Eric Garner alipoteza maisha mikononi mwa polisi mjini New York kwa njia hiyo hiyo ya kukosa pumzi na kubanwa kifua huku akipiga kelele kwa kusema: "siwezi kupumua." Aidha miaka kadhaa iliyopita, Michael Brown, Walter Scott, Tamir Rice na Wamarekani wengi weusi pia walipoteza maisha kutokana na vitendo vya ukatili wa polisi wa Marekani.
Eric Garner, Mmarekani mwingine mweusi aliyeuawa na polisi miaka sita iliyopita kwa kubinywa na kukosa pumzi
Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limeandika ujumbe kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter kwamba: "Mtu yeyote hapasi kuamka akiwa na fikra hii kwamba je, leo ni siku ambayo afisa wa polisi atamaliza maisha yake au la? Ama kwa kweli watu wa rangi,  hususan weusi nchini Marekani wanaishi na ukweli huu mchungu. Kitendo cha hivi karibuni cha polisi wa Minneapolis kimewatia hofu kubwa raia weusi wa nchi hiyo ambao kufikia sasa wamepoteza vitu vingi." Ushahidi unaonyesha kwamba ukatili na unyama wa polisi wa Marekani dhidi ya wanawake na wanaume weusi umeongezeka sana katika maeneo mengi ya Marekani.
Unyama huo unaenda sambamba na kuenea kwa virusi vya Corona. Kwa upande mmoja ni kwamba jamii ya watu weusi nchini Marekani imeathirika pakubwa na virusi vya Corona sambamba na kushuhudia vifo vingi, na kwa upande mwingine jamii hiyo inakabiliwa pia na ukandamizaji na ukatili wa polisi ya nchi hiyo. Suala la kuuawa kiholela na polisi Wamarekani weusi huibua ghasia nchini humo ambapo kufuatia jinai hizo watu wengi humiminika mabarabarani na na kushiriki katika machafuko ambayo hupelekea watu wengine kupoteza maisha kutokana na ukandamizaji mwingine wa polisi. Licha ya kujiri maandamano na ghasia hizo, lakini si serikali kuu wala Kongresi zimechukua hatua yoyote ya maana kwa ajili ya kuzuia kukaririwa ukatili huo wa polisi dhidi ya watu weusi kama ambavyo hata chunguzi nyingi kuhusiana na jinai hizo huwa zinaishia katika kuwatoa hatiani washukiwa na wahusika wakuu. Kwa hakika kitendo hicho kinawavunja moyo Wamarekani weusi na kuwafanya kuunda harakati za malalamiko na maandamano zaidi.
author

Author Name

Author Description!

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

www.CodeNirvana.in

Magazeti Ya Leo

Copyright © Magazeti ya Leo, Habari Leo Tanzania, Mwananchi, Michuzi, mwanaspoti, nipashe, Udaku | Designed By Code Nirvana