Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga, Kilimanjaro, Zefrin Lubuva akizungumza na watumishi wa Halmashauri na Wandishi wa habari wakati akipokea mashine za kisasa za kunawia kutoka kwa Taasisi ya Dk Msuya.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Dk. Msuya na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha UDOM, Dk Ombeni Msuya akizungumza wakati wa kukabidhi mashine za kisasa za kunawia kwa ajili ya kujikinga na Corona wilayani Mwanga leo.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mwanga, Zefrin Lubuva akinawa kwa kutumia mashine za kisasa zilizotolewa wilayani hapo na Taasisi ya Dk. Msuya
Mkurugenzi wa Taasisi ya Dk Msuya, Dk Ombeni Msuya akiwaonesha watumishi wa Halmashauri ya Mwanga namna ya kutumia mashine za kisasa za kunawia ambazo Taasisi yake imezitoa kwa ajili ya kujikinga na Corona.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga, Kilimanjaro, Zefrin Lubuva (wa pili kulia) akiwa katika picha ya pamoja na Mkurugenzi wa Taasisi ya Dk Msuya pamoja na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya baada ya kukabidhiwa mashine hizo leo.
Charles James, Michuzi TV
KATIKA kuiunga mkono serikali kwenye mapambano ya kujikinga na maambukizi ya ugonjwa wa Corona, Taasisi ya Dk Msuya imekabidhi mashine 10 za kunawia kwa Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga, Kilimanjaro.
Mashine hizo zenye thamani ya Sh Milioni 2.5 zimekabidhiwa kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga, Zefrin Lubuva kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya hiyo, Thomas Mwang'onda.
Akizungumza baada ya kukabidhiwa mashine hizo, Lubuva ameishukuru taasisi hiyo ya Dk Msuya kwa msaada huo ambao anaamini utakua na manufaa makubwa katika kujikinga na ugonjwa huo hatari kwa sasa ulimwenguni.
Amesema wao kama Halmashauri tayari walishachukua hatua ya kutoa elimu kwa wananchi ya kujikinga na maambukizi kwa kuwahamasisha kunawa mikono kwa sabuni na maji yanayotiririka au kutumia vitakasa mikono lakini pia kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima.
" Tunafahamu Rais wetu amekua na nia nzuri ya kuwalinda wananchi wake hivyo kama Halmashauri tumetoa elimu ya kujikinga kwa wananchi wetu na kusisitiza haswa suala la matumizi ya uvaaji barakoa na kunawa mikono," Amesema Lubuva.
Ameiomba taasisi ya Dk Msuya kuendelea kushirikiana na Halmashauri ya Mwanga bila kuchoka katika kuwahudumia wananchi wetu katika sekta mbalimbali.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Taasisi ya Dk Msuya ambaye pia ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Dk Ombeni Msuya amesema kila mtanzania ana wajibu wa kuiunga mkono serikali katika mapambano haya bila kujali Itikadi zake alizonazo.
Amesema Rais Dk John Magufuli ameendelea kuwaruhusu watanzania kuendelea kufanya shughuli zao za kiuchumi, kijamii na kiimani hivyo akaona kama kijana wa kitanzania ana wajibu wa kumuunga mkono Rais kwa kutoa mchango wake katika mapambano hayo.
" Ni wajibu wetu sote kuungana katika kipindi hiki cha Corona. Hivyo nimeona nitoe michango hii ya mashine hizi ambazo zitasaidia kujikinga na maambukizi kwani ni za kisasa ambapo mtu anaweza kunawa bila kushika koki ya bomba au sabuni kwa kutumia mashine tu.
Ni matumaini yangu kwamba mashine hizi zitatumika katika maeneo ya muingiliano wa watu kama Stendi na Sokoni lakini tofauti na mashine hizi tayari tulishatoa kwenye Zahanati na Taasisi za Dini kwa maana ya Makanisa na Misikiti kwenye Wilaya yetu," Amesema Dk Msuya.
Pia amemshukuru Rais Magufuli kwa kuendelea kuruhusu shughuli za Ibada na kusisitiza watanzania kuendelea kumuomba Mwenyezi Mungu ili atuepushe na ugonjwa huu.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Wilaya, Dk Abdul Mussa amesema vifaa hivyo hivyo vitakua ni mchango mkubwa kwao katika kupambana na Corona huku akiwaomba wadau wengine kujitokeza katika kutoa mchango wa vifaa vingine vya kujikinga na ugonjwa huo.
Taasisi ya Dk Msuya imekua ikiiunga mkono serikali katika sekta mbalimbali hasa kwenye elimu ambapo inahudumia vijana kutoka maeneo tofauti nchini.
Post a Comment