Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba Kabudi, akiwaonyesha dawa ambayo Madagascar imetoa msaada kwa Tanzania, alipozungumza na Waandishi wa habari Jijini Dae es Salaam, leo.
Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, imesema dawa ambayo nchi ya Madagascar imeitoa kama msaada wa Serikali ya Tanzania ni kwa ajili ya utafiti kwanza.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba Kabudi, leo jijini Dar es Salaam kwamba dawa hiyo inayojulikana kitaalamu kama "COVIDORGANICS" ni kwa ajili ya utafiti na siyo kwa ajili ya matumizi ya binadamu.
"Dawa hii tuliyokuja nayo jana kutoka Madagascar mara baada ya utafiti kukamilika na kupata ushauri wa kitaalamu kutoka kwa wataalamu wetu wa afya itatumika kukinga wananchi ambao hawajaathirika na kutibu wale walioathirika," Prof. Kabudi
"Huu mzigo (dawa) ni kwa ajili ya kufanyiwa utafiti, na kazi kubwa tunayoianza leo ni na wataalamu wetu wa afya ni kufanya utafiti," Amesema Prof. Kabudi.
Prof. Kabudi ameongeza kuwa dawa hiyo siyo kwa ajili ya kugawa kwa wananchi, bali ni kwa ajili ya utafiti na mara baada ya utafiti kukamilika wataalamu wa afya watatoa maelekezo ya jinsi ya utumiaji wa dawa hiyo.
Aidha, dawa hiyo imegawanyika katika makundi mawili ambapo kundi la kwanza la dawa ni kwa ajili ya kujikinga na maambukizi ya COVID 19 kwa wale ambao hawajaambukizwa ugonjwa wa Corona. Kundi la pili ni kwa ajili ya matibabu kwa wananchi ambao tayari wameathirika na COVID 19.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa serikali Prof. Abel Makubi amesema kuwa mara baada ya kupokea dawa hiyo kazi ya kwanza ya ni kuanza utafiti ambao utaonesha kama dawa hiyo ni salama na haina madara kwa wananchi na pili utafiti wa kuangalia ubora wa kutibu au kupunguza makali ya COVID 19.
"Mara baada ya utafiti wa dawa hii kukamilika itatumika katika makundi matatu ambayo kundi la kwanza ni wagonjwa kutumia dawa ya kawaida, kundi la pili watapata dawa ya kawaida na hii iliyotoka Madagascar na kundi la tatu wagonjwa watatumia dawa ya kawaida na ile inayozalishwa na Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (Nimr)," Amesema Prof. Makubi.
Prof. Makubi pamoja na mambo mengine ametoa wito kwa watanzania kuchukua tahadhari katika kujikinga na ugonjwa wa COVID 19 na wasibweteke na lolote.
Nae Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (Nimr) Prof. Yunus Mgaya amesema kuwa Nimr imejipanga kushirikiana na taasisi nyingine za Serikali hasa Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali katika kuhakikisha inafanya utafiti wa kina juu ya matumizi ya dawa hiyo.
"Nimr inafanya tafiti mbalimbali za kupambana na ugonjwa huu wa COVID 19 na itaendelea kufanya tafiti hizo ili kuwasaidia watanzania," amesema Prof. Mgaya.
Kwa upande wake Mkemia Mkuu wa Serikali, Dkt. Fidelice Mafumiko amesema kuwa Ofisi ya Mkemia Mkuu inalo jukumu lakuchunguza dawa au sumu zozote kwenye sampuli, kukadiria kwa usahihi kiasi cha dawa, umetaboli au sumu.
Dk. Mafumiko ameongeza kuwa, kupitia utafiti wa dawa hiyo, ofissi yake kwa kushirikiana na wataalamu wa afya watatafsiri matokeo ya uchunguzi katika dawa hiyo kutoa maelekezo sahihi juu ya matumizi yake kwa mwananchi.
Mkutano huu ulihudhuriwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb), Mganga Mkuu wa serikali Prof. Abel Makubi, Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (Nimr) Prof. Yunus Mgaya, Mkemia Mkuu wa Serikali, Dkt. Fidelice Mafumiko pamoja na Mkuu wa Kitengo cha Tiba za Asili Dk. Paul Mkama.
Post a Comment