Charles James, Michuzi TV
KATIBU MKUU Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk Hassan Abbas amekijia juu chombo cha habari cha NTV kwa kutoa taarifa alizoziita za uzushi kuhusiana na maendeleo ya ugonjwa wa Corona nchini.
Kupitia akaunti yao ya Twitter NTV waliweka taarifa inayosema idadi ya watu wanaokufa kwa ugonjwa wa Corona jijini Dar es Salaam kwa siku ni 50 jambo ambalo Dk Abbas amelikanusha akisema ni uongo.
" Watu 50 wanakufa kwa siku jijini Dar es Salaam kwa maambukizi ya Corona, Kiongozi Mkuu wa Upinzani Tanzania siku ya Jumatano aliishutuma serikali kwa kuficha taarifa sahihi za ugonjwa huo na kushindwa kuchukua tahadhari ya kudhibiti maambukizi," Hii ndio taarifa iliyowekwa na NTV kwenye mtandao wao wa Twitter.
Sasa baada ya taarifa hiyo kusambaa, Dk Abbas ameishutumu NTV kwa kuripoti taarifa hiyo ambayo siyo sahihi huku akiwakumbusha kufuata misingi ya taaluma ya habari.
" Huu ni Uandishi au Uhandisi wa habari? Inasikitisha kuona jinsi NTV Kenya inavyokua wakala wa uongo na uzushi. Nawakumbusha wazandiki hawa kuenzi misingi ya taaluma badala ya umaamuma," Imesomeka hivyo taarifa ya Dk Abbas aliyoiandika kwenye ukurasa wake wa Twitter.
Ikumbukwe jukumu la kutoa taarifa ya maendeleo ya ugonjwa wa Corona inatolewa na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa au Rais Dk John Magufuli.
Post a Comment