Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli anasikitika kutangaza kifo cha Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Balozi Dkt. Augustine Philip Mahiga (Mbunge) kilichotokea leo alfajiri tarehe 01 Mei, 2020 Jijini Dodoma.
Mhe. Balozi Mahiga ameugua ghafla akiwa nyumbani kwake Jijini Dodoma na amefikishwa hospitali akiwa tayari ameshafariki dunia.
Mhe. Rais Magufuli ametoa salamu za pole kwa familia ya Marehemu, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Yustino Ndugai, Wabunge, Wafanyakazi wa Wizara ya Katiba na Sheria na wananchi wa Mkoa wa Iringa kwa kuondokewa na mpendwa wao, na amesema anaungana nao katika kipindi hiki kigumu cha majonzi.
Mhe. Rais Magufuli amemuelezea Marehemu Balozi Mahiga kuwa alikuwa mchapakazi, mwadilifu, mzalendo na Mwanadiplomasia mahiri aliyeiwakilisha na kuipigania Tanzania katika njanya za Kimataifa kwa miaka mingi.
“Pamoja na umri wake mkubwa na uzoefu wa kushika madaraka katika nyadhifa mbalimbali za Kitaifa na Kimataifa, Marehemu Balozi Mahiga alikuwa mnyenyekevu na mtiifu kwa kila jukumu nililomtuma” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Amemuombea kwa Mwenyezi Mungu aipumzishe roho yake mahali pema peponi, Amina.
Post a Comment