Baba wa Uzao akihubiria mamia ya waumini wakati wa Ibada iliyofanyika katika Kanisa Halisi la Mungu Baba, Tegeta jijini Dar es Salaam, leo. Picha nyingine zaidi ya 50 za ibada hiyo, Tafadhali >> BOFYA HAPA
CCM Blog, Tegeta.
Makanisa na Waumini wametakiwa kufanya jitihada za kuhakikisha hakuna matendo mabaya kama ujambazi na ukahaba kwa kuwa maovu hayo yakitendeka katika mitaa yao wao ndiyo wanaopaswa kulaumiwa badala ya kuwatupia lawama viongozi.
Hayo yamesemwa na Kiongozi wa Kanisa Halisi la Mungu Baba anayefahamika na Kanisa hilo kwa jina la Baba wa Uzao, wakati wa mahubiri yake aliyotoa kwa waumini wakati wa ibada ya leo Jumapili, iliyofanyika kwenye Kanisa hilo lilopo Tegeta jijini Dar es Salaam.
"Ili kuonyesha sura halisi ya Kanisa ni lazima kuwajibika katika kuhakikisha jamii inaishi katika maisha masafi, mjue kuwa yanapofanyika mambo maovu ya uzinzi, ukahaba, wizi au ujambazi na mengine kama hayo, katika eneo ambako Kanisa lipo na waumini wapo wakulaumiwa siyo watawala, siyo mwenyekiti wa serikali za mtaa, Diwani, siyo DC, Siyo Mkuu wa mkoa wala siyo Rais, ni ninyi Kanisa na ninyi wenyewe", alisema Baba wa Uzao akihubiri somo la 'Sura Halisi ya Kanisa.
"Makanisa yaliasisiwa katika Sura halisi ya Haki, Upendo na Uzalisaji, lakini walioleta kwetu wakageuza lengo, waleta utumwa na ukoloni, sasa kwa kuwa tumeiona haki, Upendo na Uzalishani hatuwezi kuendelea na ukoloni mamboleo, au ninyi mnasemaje, tuendelee na ukoloni mamboleo?" alisema Baba wa Uzao na kuwauliza waumini ambao walipaza sauti wakisema "Hapanaaa..."
Akizungumzia wanaotaka uongozi aliwashauri kuacha kwenda kwa waganga au kutumia rushwa badala yake waende kanisani na kuwahakikishia kuwa wakifuata njia hiyo ya haki watapata Ubunge au Udiwani watakaokuwa wanataka.
Baada ya ibada hiyo, maonyesho ya bidhaa mbalimbali zilizozalishwa au kutengenezwa na waumini wa Kanisa hilo yaliendelea kwa watu kuuza na wengine kununua bidhaa walizohitaji ambazo karibu zote zilionekana kuwa bora.
Maonyesho hayo ambayo yalianza rasmi Jumapili iliyopita, ni ya bidhaa ambazo waumini huzitengeneza kwa kuzingatia ubora katika viwango mbalimbali ikiwa ni kutokana na kuhimizwa na Kanisa hilo kufanya hivyo kwa maelekezo kwamba Ibada anayopendwa nayo Mungu Baba ni ya Uzalishaji na siyo ya kulialia makanisani na kusubiri miujiza.
Post a Comment