Katika ibada ya Jumapili iliyopita, Kanisa Halisi la Mungu Baba, lilitumia ibada hiyo kufanya maonyesho makubwa ya bidhaa na huduma mbalimbali. ibada hiyo kwa mujibu wa Kanisa hilo inaitwa 'Mauzo ya Uzalishaji'. mtiririko w ibada hiyo iliyoongozwa na Kiongozi wa Kanisa hilo Baba wa Uzao, ni ifuatayo;
KWA NINI IBADA NI UZALISHAJI?
UFUNGUO:
Katika Mathayo 21:13 Yesu aliwaambia watu aliowakuta wanafanyia biashara hekalumi kwamba; “Nyumba yangu itakuwa Nyumba ya Sala, lakini nyie mumeifanya kuwa pango la wezi na wanyang’anyi…” Mstari uliotangulia wa 12 unasema kuwa; “Yesu akaingia Hekaluni akazipindua meza za wabadili fedha, na viti vyao waliokuwa wakiuza njiwa”.
Yesu alikuwa ana maanisha kitu gani hasa? Yeye alikuwa ana maana ya Moyo ambao ni Chanzo cha Uzalishaji kutobeba dhambi, uasi, uovu na mawazo mabaya. Hivyo, hakumaanisha kukataa Uzalishaji kama huu ambao tunao mezani leo hii. Fahamu kuwa Nyumba ya Ibada ni Moyo, kwa kuwa wakati ule wa Yesu ilikuwa bado ni kipindi cha Kao la Nafsi haikuwa rahisi kupindua Meza zile alizozikuta hekaluni.
Kilichokuwa kimemuudhi Yesu ni kumkataa kwa sababu ya mizimu na waganga waliokuwa wamejaa ndani ya mioyo yao badala yake wakaweka vitu tofauti na yeye. Wote waliokuwa pale Hekaluni, kwa sababu ya Kao la Nafsi Majira ile ya Yesu, hakuna hata mmoja aliyekuwa na chumba cha MUNGU BABA ndani ya Moyo wake. Wote walikuwa wamemkataa.
MUNGU BABA ameweza kupindua Meza ili akae Yeye kwa kuwa ni Moyo, yaani Uzalishaji wa Mazuri tu. Hivyo, wale wanaohoji kuwa Uzalishaji Kanisani ni kutotenda alichosema Yesu katika Mistari niliyonukuu hapo juu ni kutoelewa tofauti ya Majira ya Mwana na ile ya MUNGU BABA anayetawala sasa.
Majira ya Yesu ilikuwa ni Kao la Nafsi, ikiwa na maana ya enzi ya dhambi uasi na uovu wakati majira ya MUNGU BABA ni Kao la Moyo, ikiwa na maana ya enzi ya Uzalishaji wa vitu vizuri peke yake, kama inavyoonekana kwenye ibada ya leo.
Tulipoanza Ibada ni Uzalishaji, baadhi walichukia kwa kuwa walitaka tuendelee na Ibada ya kulia na kuomboleza badala ya Uzalishaji. Hawakujua kuwa Kusudi la MUNGU BABA, ambaye ndiye Chanzo Halisi ni Uzalishaji; ikiwa na maana kuwa ukitaka kumpa Ibada MUNGU BABA, anayostahili ni kwenye Uzalishaji, siyo kilio na maombolezo. Wengi tunajenga Nyumba za Ibada (kwa maana ya Makanisa na Misikiti) kwenye vituo vya kazi bila kujua kuwa zile Kazi za halali tunazofanya ndiyo Ibada hasa anayoitaka MUNGU BABA. Hapa Kanisani tunatakiwa tuje kumshukuru tu MUNGU BABA kwa yale aliyotuwezesha kuyafanya Kazini, tukiwa na vitu vile tulivyozalisha mkononi. Vilio na maombolezo kwenye Ibada, vilianza baada ya uovu kuzidi juu ya Nchi, MUNGU BABA akawa mbali na watu; sasa ni kuzalisha vitu vizuri na kumshukuru MUNGU BABA huku tukimwimbia kwa makuu aliyotutendea kazini.
Katika Mwanzo 1:28 kitu cha kwanza alichoambiwa Adamu akiwa bado kwenye Kitanga cha Mkono wa MUNGU BABA (Isaya 49:16) ni: kuzalisha; kuongezeka; kutiisha; na kutawala vyote alivyoumba MUNGU BABA. Baada ya MUNGU BABA kumfinyanga Adamu na kuanza kuonekana juu ya Nchi (Mwanzo 2:7), MUNGU BABA alimkabidhi Uzalishaji katika Bustani ya Edeni (Mwanzo 2:15).
Kwa mantiki hiyo, Ibada ambayo MUNGU BABA alikuwa anaitaka kutoka kwa Adamu ni Uzalishaji, siyo kulia na kuomboleza kwa sababu ya shida. Hata hivyo Adamu alifukuzwa kabla ya kutoa Ibada hiyo ya Uzalishaji kwa MUNGU BABA. Ibada ya Uzalishaji ambayo Adamu alitakiwa ampe MUNGU BABA, alimwachia nyoka katika Bustani ya Edeni kwamujibu wa Mwanzo 3:1-6. Hadi sasa hivi ambao walikuwa wanatoa Ibada ya Uzalishaji kwa miungu (ambayo ndiyo ibada anayoitaka MUNGU BABA) ni uzao wa nyoka, maana walioachiwa na Kanisa katika Bustani ya Edeni.
Hali hiyo ya kufukuzwa kwa Atendaye kwa Haki katika Bustani ya Edeni, ilianzia kule juu kwenye Bustani ya kwanza ya Adeni (Ezekieli 28:13-15). Kerubi alipewa na MUNGU BABA Bustani iliyokuwa imejaa madini na vito vya thamani, na vyombo vya kila aina kwa ajili ya muziki. Alitakiwa ampe MUNGU BABA Ibada ya kuzalisha Madini na Muziki mtamu. Kabla hajaanza kuzalisa Madini na Muziki mzuri; nyoka na wenzake walimdanganya kerubi akafukuzwa, akiwa najisi na kitu kisichofaa. Nyoka na uzao wake wakabaki na ile Bustani ya Adeni na vyombo vyote vya muziki. Ndiyo maana aliyefuata, yaani Adamu, akapatwa na hali ile ile iliyotokea kwenye Bustani ya kwanza juu Mlimani kwa Kerubi.
Katika Kitabu cha Mwanzo ambao walijitahidi kuendeleza Ibada ya Uzalishaji ni Nuhu (wakati wa kujenga Safina) pamoja na Ibrahimu, Isaka na Yakobo ambao walikuwa ni matajiri wa mifugo, fedha na dhahabu (Mwanzo 13:2). Yusufu pia katika Mwanzo 47:14, tunasoma kuwa alitoa Ibada kwa MUNGU BABA kupitia Uzalishaji wa kukusanya nafaka katika Taifa la Misri.
Hali ilibadilika baada ya Kitabu cha Mwanzo kuisha, Kanisa lilipoenda utumwani. Kama unavyofahamu mtumwa hawezi kuzalisha kwa ajili yake, bali hufanya kazi kwa ajili ya bwana wake! Utumwa ndiyo iliyokuwa hali ya Kanisa katika vizazi vyote vilivyopita. Utumwa wa Kanisa kule Misri, ulianzia kwa Watoto wa Ibrahimu wakiwa bado hawajazaliwa (Mwanzo 15:8-15). Walipozaliwa walijikuta wako Misri tayari. Baada ya kutoka katika utumwa Misri walirudi utumwani tena Babeli (Daniel 9:2).
Walipotoka katika utumwa wa Babeli wakajikuta wako kwenye utumwa wa kutoisikia Sauti ya MUNGU BABA kwa miaka 400 (Malaki 4:4-6).
Walipotoka kwenye utumwa huo wa kutoisikia Sauti ya MUNGU BABA, wakaingia kwenye utumwa wa kumkataa Mwokozi wao (Yohana 9:28-29). Wakiwa bado wako katika utumwa huo wa kumkataa Masihi, wakajikuta wako kwenye utumwa wakuibiwa Majira ya MUNGU BABA kupitia Papa Gregory Mwaka 1582! Utumwa huu wa kuishi kwa kutumia Majira ya dunia na ulimwengu (badala ya Majiara ya MUNGU BABA), ulikuwa mbaya zaidi maana hata sasa unaendelea na ndio unaosababisha watendao kwa haki wasielewe kuwa Ibada ni Uzalishaji.
Hata baada ya Kanisa kutoka kwenye utumwa kupitia Sauti Mpya iliyosikika Kigoma Tanzania (2019), utumwa wa fikra bado haujaisha kabisa. Hadi sasa Kanisa lilikuwa bado linadhani Ibada ni kumletea shida MUNGU BABA, kumbe Ibada ambayo MUNGU BABA anataka ni Uzalishaji. Haina maana MUNGU BABA hajali matatizo tuliyonayo, maana Yeye ndiye Mponyaji wa Namba Moja, ila anataka Ibada Halisi ilioibiwa na dunia na ulimwengu irejee mahali pake (Yohana 4:23).
HITIMISHO
Jamii leo ielewe kuwa Ibada ambayo MUNGU BABA anapendezwa nayo ni Uzalishaji siyo kilio na maombolezo. Tuache ile fikra kuwa Kanisani ni mahali pa wenye shida na matatizo na kusubiri muujiza. Huo ni utumwa ambao tuliingizwa na nyoka ambaye ndiye alibaki na Bustani zote.
Ili tusimtoe huyo nyoka katika Bustani alizoteka, alituletea Ibada feki ya kulia na kuomboleza, Uzalishaji tukamwachia yeye na uzao wake. Baada ya MUNGU BABA kuja juu ya nchi kupitia Tanzania, sasa amerejesha ile Ibada aliyokuwa anaitaka ya Uzalishaji. Tuanze sasa: kuzalisha; kutangaza; na kuuza bila ukomo. Hiyo ndiyo Bustani Mpya aliyokuja nayo MUNGU BABA kwetu.Tuipokee kwa upendo maana naye MUNGU BABA ametupatia hiyo Bustani kwa upendo pia.
Post a Comment