Featured

    Featured Posts

KUAGA DUNIA RAMADHAN ABDALLAH; NEMBO YA JIHADI YA PALESTINA

Palestina haina upungufu wa shakhsia wabunifu, wema, waasisi na wanajihadi katika historia ya nchi hiyo. Mmoja wa shakhsia hao ni Dakta Ramadhan Abdallah Shalah ambaye amekuwa na nafasi muhimu katika mapambano dhidi ya utawala ghasibu wa Israel unaoikalia kwa mabavu Quds Tukufu.
Dakta Ramadhan Abdallah ni mmoja wa wasomi, wanasiasa na wanajihadi wa Palestina ambaye alianza kuiongoza Harakati ya Jihadul Islami mwaka 1995 mara tu baada ya kuuawa kigaidi Fat'hi Shaqaqi na utawala katili wa Israel na kuhudumu katika nafasi hiyo hadi mwaka 2018, yaani baada ya miaka 23 ya uongozi wa harakati hiyo.
Harakati ya Jihadul Islami ilikamilika na kuimarika zaidi katika kipindi cha uongozi wa Ramadhani Abdallah. Alikuwa aikisisitiza sana mapambano ya silaha dhidi ya utawala ghasibu wa Israel na kupinga kila aina ya mapatano na utawala huo. Ni kwa msingi huo ndipo harakati hiyo ya Kiislamu ikasusia kushiriki katika uchaguzi wa bunge la Palestina wa miaka ya 1996 na 2006 ili kuthibitisha kwamba si tu kuwa ulikuwa ukipinga mapatano na utawala wa Kizayui bali na hata waungaji mkono wa mapatano hayo.
Ramadhan Abdallah alipokutana na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu
Hata kama Ramadhan Abdala hakufanikiwa kupata daraja ya kuuawa shahidi, lakini alikabiliwa na majaribio mengi ya mauaji ya kigaidi kutoka kwa utawala huo unaokalia kwa mabavu Quds Tukufu pamoja na serikali ya utawala wa Marekani. Muda mfupi baada ya kuarifishwa kuwa Katibu Mkuu wa Harakati ya Jihadul Islami, serikali ya Marekani tarehe 27 Novemba 1995  ililiweka jina la Ramadhan Abdallah Shalah katika orodha yake nyeusi na kumukumu katika mahakama ya Florida kwa tuhuma 53 zikiwemo za kushiriki katika vitendo vya ugaidi, shughuli za kuhatarisha maslahi ya Israel, kuongoza makundi ya jihadi ya Palestina na shughuli za uasi pamoja na utegaji mabomu.
Mwaka 1998 pia serikali ya Marekani ilitangaza kutenga zawadi ya dola milioni 5 kwa ajili ya kukamatwa kwake jambo lililompelekea kujulikana kama 'mtu wa dola milioni tano.' Alikuwa akifuatiliwa sana na makachero wa FPI kutokana na nafasi yake muhimu katika kuunga mkono malengo matukufu ya Palestina na mapambano yake dhidi ya utawala haramu wa Israel. Hatua hiyo ya kigadi ya serikali ya Marekani dhidi ya Dakta Ramadhan Abdallah, Katibu Mkuu wa zamani wa Harakati ya Jihadul Islami, kabla ya jambo lolote lile ilithibitisha wazi kuwa alikuwa na nafasi muhimu katika kuimarisha shughuli za harakati hiyo na mapambano ya Wapalestina dhidi ya maghasibu wa Israel.
Ziyad al-Nakhala, katibu Mkuu wa Harakati ya Jihadul Islami
Nukta nyingine ni kuwa Dakta Ramadhan Abdallah hakuwa shakhsia wa kisiasa aliyefungamana tu na Harakati ya Jihadul Islami bali alikuwa shakhsia wa taifa zima la Palestina na hata aliyekuwa na umashuhuri mkubwa katika uwanja wa mapambano ya Kiislamu nje ya mipaka ya Palestina. Kufuatia kifo chake si harakati za Palestina za Jihadul Islami na HAMAS pekee ndizo zilisikitishwa na kifo chake bali hata chama cha Fat'h, Mahmoud Abbas, Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina na viongozi wa chama cha Hizbullah cha Lebanon pia wametuma salamu zao za rambirambi wakielezea kusikitishwa kwao na kumpoteza shakhsia huyo muhimu wa kitaifa wa Palestina. Harakati ya HAMAS imetoa taarifa ikisema kuwa taifa la Palestina limempoteza shakhsia mkubwa wa Kipalestina katika uwanja wa mapambano na Jihadi na kwamba alikuwa nembo ya subira, ukakamavu, Jihadi na juhudi za kufanikisha suala la Palestina. Naye kwa upande wake, Mahmoud Abbas, Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina ametoa taarifa akisema kuwa kifo cha Ramadhan Abdallah ni kupoteza nguzo madhubuti ya kitaifa.
Bila shaka kifo cha Dakta Ramadhan Abdallah ni tukio chungu na la majonzi kwa taifa zima la Palestina. Pamoja na hayo hakuna shaka yoyote kwamba njia ya shakhsia huyo shupavu na mkubwa wa Palestina itaendelezwa kwa nguvu zote na shakhsia wengine wakubwa wa taifa hilo, akiwemo, Ziyad al-Nakhala, Katibu Mkuu mpya wa Jihadul Islami.
author

Author Name

Author Description!

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

www.CodeNirvana.in

Magazeti Ya Leo

Copyright © Magazeti ya Leo, Habari Leo Tanzania, Mwananchi, Michuzi, mwanaspoti, nipashe, Udaku | Designed By Code Nirvana