Featured

    Featured Posts

MAJALIWA: SH. MILIONI 700 KUJENGA SHULE YA SEKONDARI YA WASICHANA RUANGWA

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na viongozi wakati alipowasili katika kijiji cha Chikwale wilayani Ruangwa kuzungumza na wananchi, Juni 22, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Ruangwa, Lindi
WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema Serikali imedhamiria kuboresha elimu kwa watoto wa kike nchini kote ikiwemo wilaya ya Ruangwa ambayo imepewa sh. milioni 700 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa shule maalumu ya sekondari ya wasichana.

Amesema Serikali inataka mtoto wa kike asome kuanzia darasa la awali hadi elimu ya juu na kwamba ujenzi wa shule za wasichana utasaidia katika kuwaondolea vikwazo watoto wa kike ambavyo vinasababisha washindwe kufikia malengo yao kielimu.

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumatatu, Juni 22, 2020) wakati akizungumza kwa nyakati tofauti na wananchi katika vijiji vya Chikwale, Nangurugai, Machang’anja, Narungombe na Liuguru wilayani Ruangwa akiwa katika ziara ya kikazi.

“Serikali imejipanga vizuri katika sekta ya elimu, wazazi mnatakiwa muhakikishe watoto wote wa kike na wa kiume wanakwenda shule. Na kuhusu elimu kwa mtoto wa kike tumeboresha na sheria kali imetungwa kwa watakaokatisha masomo yao.”

Waziri Mkuu ameongeza kuwa mbali na ujenzi wa shule hiyo maalum ya sekondari ya wasichana ambayo itajengwa Ruangwa mjini, pia Shule ya Sekondari ya Liuguru inatarajiwa kujengewa mabweni na kubadilishwa kuwa ya wasichana. 

“Tayari Serikali imetoa sh. milioni 180 kwa ajili ya ujenzi wa mabweni na bwalo katika Shule ya Sekondari ya Liuguru ambayo tunataka iwe ya watoto wa kike ili wasome kwa utulivu bila kuguswaguswa na waweze kutimiza ndoto zao. Hivyo watoto wa kike wilayani Ruangwa watasoma kwa uhakika bila ya kuwa na mashaka..”

Kuhusu watoto wa kiume waliokuwa wanasoma shule ya Sekondari ya Liuguru, Waziri Mkuu amesema watakwenda kusoma katika shule ya Sekondari ya Narungombe ambayo nayo itakuwa ya bweni kwa watoto wa kike na wa kiume na tayari Serikali imetoa sh. milioni 80 kwa ajili ya ujenzi wa bweni.

Kadhalika, Waziri Mkuu amezungumzia kuhusu wananchi wanaotaka kwenda kufanya shughuli za maendeleo hususani ya kilimo katika vijiji vilivyoko kwenye wilaya nyingine, kwamba hawazuiliwi lakini wanatakiwa wafuate taratibu zilizopo.

Waziri Mkuu ameyasema hayo baada ya wananchi wa kijiji cha Chikwale ambacho kinapakana na wilaya ya Liwale na Kilwa kwa kutengenishwa na mto Mbwenkuru kuwa wakienda kulima ng’ambo ya mto huo wanazuiwa na baadhi yao wanapigwa.

Akizungumzia kuhusu kuporomoka kwa bei ya ufuta, Waziri Mkuu amesema inatokana na bei ya soko la Dunia na kwamba hali hiyo itakoma kwa kujenga viwanda vya kuchakata mazao hayo nchini, amewataka wakulima wawe watulivu wakati Serikali ikilifanyia kazi suala hilo.

Amesema moja ya msisitizo wa Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli ni kuboresha sekta ya kilimo ili iweze kujitosheleza kwa chakula. “Suala la bei ya mazao linapangwa na wanunuzi Serikali inasimamia tu.” 

Pia, Waziri Mkuu ameendelea kuwashukuru wananchi wa wilaya hiyo kwa umoja na mshikamano mkubwa waliompatia katika kipindi chote cha miaka mitano na amewasisitiza waendelee na ushirikiano huo kwa ajili ya maendeleo ya wilaya yao na Taifa kwa ujumla.
author

Author Name

Author Description!

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

www.CodeNirvana.in

Magazeti Ya Leo

Copyright © Magazeti ya Leo, Habari Leo Tanzania, Mwananchi, Michuzi, mwanaspoti, nipashe, Udaku | Designed By Code Nirvana