Dodoma, Tanzania
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 11 Juni, 2020 amezindua majengo ya Ofisi za Makao Makuu ya Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa barabara za Mji wa Serikali Makao Makuu Dodoma na kukabidhi pikipiki 448 za Maafisa Tarafa hapa nchini.
Sherehe za uzinduzi wa jengo la TARURA, uwekaji jiwe la msingi la ujenzi wa kilometa 51.2 za barabara za lami katika Mji wa Serikali Mtumba Jijini Dodoma na kukabidhi pikipiki 448 za Maafisa Tarafa, zimefanyika katika Mji wa Serikali Mtumba na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Mawaziri, Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu, viongozi Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na usalama, viongozi wa Dini na viongozi wa Mkoa wa Dodoma wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa huo Dkt. Binilith Mahenge.
Jengo la Makao Makuu ya TARURA ambalo ni la ghorofa 2, mita za mraba 1,961, ofisi 34 na ukumbi wa mikutano, limejengwa kwa gharama ya shilingi Bilioni 1 na Milioni 969 kwa kutumia utaratibu wa ‘Force Account’ ambao umesaidia kuokoa fedha nyingi, badala ya utaratibu wa kutumia mkandarasi ambao ungegharimu zaidi ya shilingi Bilioni 7.
Ujenzi wa barabara za lami ngumu ya Mji wa Serikali zenye urefu wa kilometa 51.2 ambao umeanza tarehe 01 Februari, 2020, unatarajiwa kukamilika tarehe 31 Julai, 2021 kwa gharama ya shilingi Bilioni 89.232 ambapo kilometa 11.2 zitakuwa na njia 4 na kilometa 28.8 zitakuwa na njia mbili.
Pikipiki 448 zilizonunuliwa kwa ajili ya Maafisa Tarafa zimegharimu shilingi Bilioni 1 na kununuliwa kwake kutafanya Maafisa Tarafa wote hapa nchini kuwa na pikipiki kwa ajili ya kuwahudumia wananchi.
Akizungumza katika sherehe hizo, Mhe. Rais Magufuli ameipongeza TARURA kwa kujenga ofisi ya makao yake makuu kwa kutumia kiasi kidogo cha fedha na kwa kuanza ujenzi wa barabara za Mji wa Serikali, na pia amezipongeza wizara, idara na taasisi zingine za Serikali zilizojenga ofisi zake katika Mji wa Serikali. Ameelezea kuridhishwa kwake na maendeleo makubwa ya Mji wa Serikali na Jiji zima la Dodoma.
Hata hivyo ameitaka TARURA kutojenga ofisi zake Wilayani na Mikoani, badala yake watumie majengo ya Serikali yaliyopo, na ameitaka Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kuhakikisha jengo lake la Makao Makuu linalojengwa Dodoma linakamilika ndani ya mwaka huu, badala ya kutumia majengo yasiyo yake.
Mhe. Rais Magufuli amesema licha ya kwamba wapo ambao hawakuamini kuwa Serikali inaweza kuhamia Dodoma, jambo hilo limewezekana ambapo watumishi wa umma 13,361 wamehamia Dodoma, viongozi wakuu wote wakiwemo Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Mawaziri na viongozi Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama wamehamia Dodoma. Amelipongeza Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kupitisha sheria ambayo imetambua rasmi kuwa Dodoma ndio Makao Makuu ya nchi.
Amebainisha kuwa sambamba na mafanikio hayo, Serikali inachukua hatua madhubuti za kuimarisha huduma za kijamii katika Jiji la Dodoma ikiwemo kujenga hospitali, kujenga kilometa 110 za barabara ya mzunguko, kujenga uwanja wa ndege wa kimataifa wa Msalato, soko, kituo cha mabasi na kuimarisha barabara za ndani ya Jiji.
Mhe. Rais Magufuli amelishukuru Shirika la Fedha Duniani (IMF) kwa kutoa msamaha wa Dola za Marekani Milioni 14 (sawa na shilingi Bilioni 31.934) kwa Tanzania kwa ajili ya kukabiliana na athari za ugonjwa wa Corona.
Kuhusu pikipiki za Maafisa Tarafa, Mhe. Rais Magufuli amewataka Maafisa Tarafa hao kuzitunza na ameonya kuwa atayeiharibu kutokana na matumizi mabaya atalipa.
Mhe. Rais Magufuli amezindua jengo la Makao Makuu ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Jijini Dodoma. Jengo hili lenye ghorofa tatu limejengwa kwa gharama ya shilingi Bilioni 2.656 kwa utaratibu wa ‘Force Account’ na ujenzi wake ulioanza Februari 2019 umekamilika Machi 2020.
Mhe. Rais Magufuli amelipongeza jeshi hilo kwa kukamilisha ujenzi wa jengo lake la Makao Makuu na katika sherehe za uzinduzi huo ametangaza kumsamehe aliyekuwa Kamishna Jenerali wa Zimamoto na Uokoaji Thobias Andengenye aliyeondolewa katika nafasi hiyo pamoja na Makamishna wengine 4 kufuatia kuhusika kwao katika andiko la kutaka kukopa fedha nyingi kinyume cha utaratibu.
Hata hivyo amesema Kamishna Andengenye ambaye ndiye chimbuko la kujengwa kwa jengo hilo, hatorudi katika nafasi ya Kamishna Jenerali wa Zimamoto na Uokoaji na badala yake atampangia majukumu mengine.
Mhe. Rais Magufuli amezitaka halmashauri zote za Majiji, Manispaa, Miji na Wilaya hapa nchini kuhakikisha mipango miji yake inazingatia uwepo wa miundombinu ya zimamoto na uokoaji ili kuliwezesha jeshi hili kufikia maeneo yote yanayokubwa na ajali za moto na kutekeleza majukumu yake.
Amekubali ombi la Kamishna Jenerali wa Zimamoto na Uokoaji Meja Jenerali John Masunga aliyeomba fedha za kujengea nyumba za Maafisa na Askari, ambapo ameahidi kutoa shilingi Bilioni 5 katika kipindi cha wiki 1 ili ujenzi wa nyumba 80 Jijini Dodoma uanze mara moja.
Mhe. Rais Magufuli amewashukuru Watanzania wote kwa kuitikia vizuri maelekezo yake tangu ugonjwa wa Corona ulipoingia hapa nchini na ameagiza kitengo cha tiba cha Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kiimarishwe kwa kuongezewa bajeti ili kiongeze uwezo wa kuzitambua na kuziidhinisha dawa za asilia ambazo zitathibitika kuwa zinatibu maradhi.
Katika shughuli alizofanya leo, Mhe. Rais Magufuli amewaongoza wananchi kusimama kwa dakika moja kwa ajili ya kumkumbuka Rais wa Burundi Mhe. Pierre Nkurunziza aliyefariki dunia tarehe 06 Juni, 2020 na watu 8 waliofariki dunia leo huko Mwanza baada ya basi dogo la abiria walilokuwa wakisafiria kugongwa na lori.
Post a Comment