Nana Addo Dankwa Akufo-Addo ameeleza juu ya kushtushwa na kusikitishwa kwake na mauaji ya Floyd na kueleza bayana kuwa, watu weusi kote duniani wameghadhabishwa na kusikitishwa na mauaji hayo ya kikatili dhidi ya mtu mweusi ambaye hakuwa na silaha yoyote.
Amesema taifa la Ghana limesimama na Wamarekani wenye asili ya Afrika katika kipindi hiki kigumu cha simanzi. Rais wa Ghana amebainisha kuwa: Si sawa katika karne hii ya 21, Marekani, kitovu cha demokrasia, inaendelea kukabiliana na tatizo la ubaguzi wa rangi unaofanyika kwa mpangilio maalumu.
Rais Nana Akufo-Addo wa Ghana ameongeza kuwa, mauaji hayo ya kutisha ya Mmarekani mweusi yanabeba taswira ya hali halisi ya kila siku inayoumiza, na kumbukumbu yenye sura ya kutisha.
Mei 25, afisa mmoja mzungu wa jeshi la polisi la Marekani alimuua kikatili George Floyd, Mmarekani mmoja mwenye asili ya Afrika katika mji wa Minneapolis, ukatili ambao umezusha wimbi kubwa la maandamano na machafuko katika kona zote za Marekani, na hivi sasa maandamano hayo yameenea katika nchi mbalimbali duniani.
Post a Comment