Miji mikuu ya Kenya na Nigeria jana ilishuhudia maandamano ya kulaani ubaguzi wa rangi na mauaji ya George Floyd, raia wa Marekani mwenye asili ya Afrika aliyeuliwa kikatili na polisi mmoja mzungu katika mji wa Minneapolis, katika jimbo la Minnesota nchini Marekani wiki iliyopita.
Katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi waandamanaji walikusanyika nje ya ubalozi wa Marekani jijini hapo huku wakiwa wamebeba mabango yenye jumbe mbalimbali za kulaani jinai hiyo. Baadhi ya mabango hayo yalikuwa yameandikwa: Maisha ya weusi ni muhimu, komesha ubaguzi, na komesha mauaji kinyume cha sheria.
Sehemu ya barua ya waandamanaji hao waliyomuandikia Kyle McCarter, Balozi wa Marekani nchini Kenya imesema: George Floyd ameuawa na polisi aliyeshajiishwa na serikali unayoitumikia, alifanya hivyo akifahamu kuwa mfumo wa utawala utamkingia kifua."
Katika mji mkuu wa Nigeria, Abuja mambo hayakuwa tofauti. Waandamaji walikusanyika nje ya ubalozi wa Marekani wakiwa na ujumbe huo huo wa kutaka kuwajibishwa wahusika wa mauaji hayo na kufanyiwa marekebisho mfumo wa utawala na kijamii wa nchi hiyo ya kibeberu. Wananchi hao wa Nigeria wamefanya maandamano hayo hayo licha ya ubalozi huo wa US mjini Abuja kuzingirwa na maafisa usalama waliojizatiti kwa silaha.
Baada ya polisi mzungu kumuua kinyama George Floyd, Mmarekani mweusi raia wa Marekani raia wa nchi hiyo wamejawa na hasira na wamekuwa wakiminika barabarani kulaani jinai hiyo kwa zaidi ya wiki moja sasa.
Maandamano hayo ya kulaani ubaguzi wa rangi na ukatili wa polisi ya Marekani hivi sasa yameenea na kusambaa katika nchi mbalimbali duniani zikiwemo za Ulaya na Afrika.
Post a Comment