Na Mwandshi Wetu, DAR ES SALAAM
VIGOGO Yanga SC wametokea nyuma na kushinda 3-2 dhidi ya Ndanda SC katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, Uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam.
VIGOGO Yanga SC wametokea nyuma na kushinda 3-2 dhidi ya Ndanda SC katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, Uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam.
Ushindi huo unairejesha Yanga SC nafasi ya pili, ikifikisha pointi 60 katika mchezo wa 32, sasa inazidiwa pointi 18 na mabingwa watetezi, SImba SC ambao wana mechi moja mkononi.
Katika mchezo wa leo uliochezeshwa na refa Raphael Ikambi wa Morogoro aliyesaidiwa na Sunday Komba wa Kilimanjaro na Credo Mbuya wa Mbeya, Yanga walikuwa wa kwanza kupata bao kupitia kwa kiungo wake, Deus David Kaseke dakika ya tano tu akimalizia pasi ya mshambuliaji Ditram Adrian Nchimbi.
Lakini Ndanda SC wakatoka nyuma kwa mabao mawili ya Abdul Hamisi dakika ya 10 na 15 mara zote akimalizia kazi nzuri ya mchezaji mwenzake Omary Mponda na kuongoza kwa 2-1.
Mchezaji wa zamani wa Mbeya City, Deus Kaseke akaisawazishia Yanga dakika ya 45 akimalizia kazi nzuri ya beki wa kulia, Juma Abdul Mnyamani.
Mkongwe Mrisho Khalfan Ngassa akatokea benchi kipindi cha pili na kuifungia Yanga SC bao la ushindi dakika ya 72 akimalizia kazi nzuri ya Juma Abdul.
Mechi nyingine za Ligi Kuu leo, Bao la dakika ya 90 na ushei la Gershon Kabeja likainusuru Biashara United kulala nyumbani mbele ya Azam FC iliyotangulia kwa bao la Frank Domayo dakika ya 48 timu hizo zikitoka sare ya 1-1 Uwanja wa Karume, Musoma mkoani Mara.
Nayo Kagera Sugar ikalazimishwa sare ya 1-1 na KMC ya Kinondoni, Dar es Salaam, wageni wakitangulia kwa bao la Abdul Hassan dakika ya 22, kabla ya Yussuph Mhilu kuwasawazishia wenyeji dakika ya 40 Uwanja wa Kaitaba, Bukoba.
Ruvu Shooting nayo ikatoa sare ya 1-1 na Namungo FC Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani - Abeid Athuman akiwatanguliza wageni dakika ya 16, kabla ya William Patrick kuwasawazishia wenyeji dakika ya 30.
Na Uwanja wa Mwadui Complex, wilayani Kishapu mkoani Shinyanga, bao pekee la Wallace Kiango dakika ya 56 likaipa Mwadui FC ushindi wa 1-0 dhidi ya Mtibwa Sugar, wakati Uwanja wa Nyamagana Jijini Mwanza, bao pekee la Martine Kiggi dakika ya 47 likawapa wenyeji, Alliance FC ushindi wa 1-0 dhidi ya Coastal Union.
Uwanja wa Sokoine Jijini Mbeya, mabao ya Peter Mapunda dakika ya 37 na Patson Shigala dakika ya 90 na ushei yakaipa Mbeya City ushindi wa 2-0 dhidi ya JKT Tanzania.
Singida United wakachapwa 3-2 na Lipuli FC Uwanja wa Liti mkoani Singida, mabao ya wageni yakifungwa na Daruwesh Saliboko dakika ya 32 kwa penalti na 33 na Joseph Ntamack dakika ya 57, huku ya wenyeji yakifungwa na Stephen Sey dakika ya 35 na 41.
Kikosi cha Yanga SC leo kilikuwa; Farouk Shikhalo, Juma Abdul, Adeyoum Ahmed, Said Juma ‘Makapu’, Kelvin Yondan, Feisal Salum, Haruna Niyonzima/ Patrick Sibomana dk78, Raphael Daudi/ Abdulaziz Makame dk46, David Molinga/ Tariq seif dk78, Ditram Nchimbi/Mrisho Ngassa dk64 na Deus Kaseke.
Ndanda SC; Ally Mustapha ‘Barthez’, Swalehe Abdallah, Hemed Khoja, Abdulrazak Mohamed, Paul Maona, Danald Taro, Abdul Hamisi/ Kassim Mdoe dk70, Vitalis Mayanga, Omar Mponda/Athumani Chubi dk85, Omary Ramadhani/Omary Hamisi dk80 na Kiggi Makassy.
Post a Comment