Kaburi la umati la watu waliouawa na kundi la kigaidi la Daesh limegunduliwa katika mkoa wa Nineveh huko kaskazini mwa Iraq.
Kaburi hilo limegunduliwa katika kijiji cha Hamidat katika eneo la Badush magharibi mwa Mosul na lina mabaki ya maiti za raia mia sita waliouawa na kuzikwa kwa umati na kundi la kigaidi la Daesh.
Uchunguzi uliofanywa na shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch umeonyesha kuwa, watu wasiopungua 1500 waliokuwa wanashikiliwa katika jela la Mosul walihamishiwa katika kijiji cha Hamidat na 600 miongoni mwao waliuawa na Daesh na kuzikwa katika kaburi hilo la umati.
Novemba mwaka 2018 Umoja wa Mataifa ulitangaza kuwa kundi la kigaidi la Daesh lilitengeneza zaidi ya makaburi 200 ya umati katika maeneo mbalimbali liliyoyavamia ya Iraq katika kipindi cha baina ya mwaka 2014 na 2017.
Mwaka 2014 kundi hilo la kigaidi lilivamia na kuteka baadhi ya maeneo ya kaskazini na magharibi mwa Iraq likisaidiwa kijeshi na kifedha na Saudi Arabia, Marekani na washirika wao na kufanya uhalifu na jinai za kutisha. Wakati huo Iraq iliiomba msaada Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa ajili ya kupambana na genge hilo.
Novemba 17 mwaka 2017 jeshi la Iraq likisaidiwa na washauri wa kijeshi wa Iran lilifanikiwa kukomboa ngome ya mwisho ya kundi la kigaidi la Daesh katika mji wa Rawa na kulifurusha rasmi kundi hilo.
Post a Comment