WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli imetoa zaidi ya sh. bilioni 25 mkoani Songwe ili kugharamia miradi ya maji na afya ukiwemo na ujenzi wa hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Tunduma.
Ameyasema hayo leo (Jumatatu, Julai 06, 2020) wakati akizungumza na wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kata ya Mpemba, wilaya ya Momba mkoani Songwe akiwa katika ziara yake ya kikazi. Kabla ya kuzungumza na wananchi, Waziri Mkuu alikagua ujenzi wa hospitali hiyo.
Waziri Mkuu amesema ujenzi wa hospitali hiyo inayojengwa kwa awamu tatu utaimarisha upatikanaji wa huduma za afya katika mji wa Tunduma na akawasihi wananchi wa mkoa wa Songwe waendelee kuiunga mkono Serikali hii ambayo imedhamiria kuwaletea maendeleo.
“Nawasihi Watanzania muendelee kuiunga mkono Serikali yenu. Nawasihi Watanzania muendelee kumuunga mkono Rais wetu, Dkt. John Pombe Magufuli pamoja na kuliombea Taifa hili na viongozi wake. Serikali yenu inaendelea kufanya kazi nyingi kwa ajili ya maendeleo yenu.”
Waziri Mkuu amesema awali, Serikali ilitoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa hospitali hiyo lakini baadhi ya watendaji walitaka fedha hizo zitumike kwa ajili ya ujenzi wa jengo la utawala huku wakitaka wananchi waendelee kukosa huduma bora za afya, ambapo Serikali haikukubaliana nao na kuagiza ijengwe hospitali.
Naye, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Tunduma, Regina Bieda amesema ujenzi wa hospitali hiyo ya wilaya ulianza baada ya agizo la Waziri Mkuu alilolitoa Julai 21, 2017 alipofanya ziara katika halmashauri hiyo.
Amesema kukamilika kwa hospitali hiyo kutaboresha utoaji wa huduma za afya katika halmashauri hiyo ambayo ambayo ina wakazi zaidi ya 170,000 ambapo pamoja na idadi hiyo kubwa ya watu haikuwa na hospitali yenye hadhi ya wilaya, hivyo huduma za afya zinatolewa na Kituo cha Afya cha Tunduma.
Kwa upande wake, David Silinde ambaye alikuwa mbunge wa jimbo la Momba, amesema wananchi hawana budi kuiunga mkono Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. Magufuli kwa sababu imefanya kazi kubwa za kuboresha maendeleo nchini.
Mbali na kutoa wito huo kwa wananchi, pia Silinde, aliwaongoza wananchi kumuombea Rais Dkt. Magufuli ili Mwenyezi Mungu azidi kumbariki pamoja na viongozi wengine waweze kuwatumikia Watanzania. “Chini ya uongozi wa Rais Dkt. Magufuli, Tanzania itafika mbali zaidi kimaendeleo,” alisema.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
Post a Comment