Featured

    Featured Posts

SHERIA NGUMU CHANZO CHA MIGOGORO NGORONGORO

 Kiongozi wa mila ya wafugaji wa Kimasai wa Bonde la Ngorongoro, Sembet Ngoidik akionesha ramani iliyoandaliwa na sehemu ya kahawia ndilo wanalotakiwa kubaki ambalo ni dogo kulingana na idadi ya vijiji vyao. 
Kiongozi wa mila ya Wafugaji wa Kimasai Medukenya Nepukol akisoma tamko la kumuomba rais afike eneo hilo kuwaokoa na Kero yao ya kuhamishwa kwa nguvu 
Kamishina wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA)  Dkt Freddy Manongi 

KUONGEZEKA kwa idadi ya watu, kupungua kwa maeneo ya malisho,  magonjwa yanayotoka kwa wanyama pori kwenda kwa binadamu na uwepo wa sheria ngumu katika eneo la Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA), ndiyo sababu ya kuwepo migogoro ya mara kwa mara.

Akizungumza katika mahojiano maalum na mwandishi wa habari hizi  ofisini kwake, Kamishina wa Uhifadhi wa NCAA Dkt Freddy Manongi, alisema kuwa migogoro inayojitokeza hivi karibuni baina ya wenyeji na mamlaka ya hifadhi inatokana na changamoto mbalimbali zilizojitokeza na ambazo tayari zimeanza kutafutiwa majawabu yake. 

"Sheria ya eneo hili la Ngorongoro ni kali na ni mbaya kuliko sheria yoyote ile duniani... Nilipokuja hapa nikaona sheria zinazotumika ni za kikoloni zinakandamiza maisha ya watu na maendeleo yap, " alisema Dkt Manongi. 

Alisema wamewasilisha maombi katika Tume ya Kurekebisha sheria ili angalau zibadilishe ziendane na mazingira halisi ya wananchi hasa katika suala la kilimo na ufugaji pamoja na mambo mengine.

"Sheria inazuia kulima humu katika eneo hili na wakati dunia nzima inategemea kilimo kwa ajili ya ustawi wa maendeleo ya jamii, humu ndani hata kujenga nyumba lazima upate kibali,"alisema na kuongeza,

"Sheria za hapa ni ant-human development tubadilishe sheria hizi tuwape unafuu wa maisha wananchi wanaoishi humu, hata kuchimba kisima unatakiwa upate kibali cha Kamishina".

Kamishina Dkt Manongi alisema anakubaliana na wananchi wanaoishi katika eneo hilo kwamba sheria ni ngumu na mbaya lakini hata hivyo tayari wameanza kutafuta maoni ya wananchi ili waweze kuzibadilisha ziendane na uhalisia wa sasa.

Hata hivyo, alisema pamoja na kuwepo na sheria ngumu, hivi sasa eneo hilo limekumbwa na migogoro baina ya wenyeji na mamlaka kutoka na mazingira yaliyopo sasa hayawezi kuendeleza uhifadhi kutokana na uwepo wa idadi kubwa ya watu, mifugo na kuongezeka kwa magugu katika malisho. 

Alisema mwaka 1959 idadi ya watu ilikuwa wastani wa watu 8,000 Lakini sasa watu wameongezeka hadi kufikia 93,000 mwaka 2017.

Alisema eneo la ardhi ya hifadhi lilikuwa hekta 8,992 lakini sasa lipo 8,100 kwa kipindi cha miaka 60 limepungua kutokana na kuongezeka kwa mifugo na idadi ya watu. 

"Humu katika hifadhi mwaka 1972 kulikuwa na Faru 5,000 
walikuwa kila sehemu lakini sasa waliopo hawazidi 100," alisema Dkt Manongi na kuongeza kwamba Faru sasa wapo eneo la Nyanda ya kaskazini ya hifadhi hiyo name Kreta kutokana na maeneo yao kuvamiwa na shughuli za kibinadamu. 

Kuhusu suala la malisho alisema mifugo na wanyama pori wamekuwa wakinyang'anyiana chakula kutokana na kuongezeka magugu katika maeneo ya malisho ambayo yameletwa kutokana na idadi kubwa ya mifugo hivyo kusababisha kuwepo na majani machache ya chakula. 

Dkt Manongi alisema mwaka 2018 Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt Hamisi Kigwangala ameunda Tume kufanya tathimini juu ya matumizi mseto ya ardhi katika eneo hilo baada ya malalamiko ya wenyeji kufanya marejeo ya namna bora ya kulihifadhi eneo hilo kutokana na changamoto zilizopo. 

"Mwaka huu Tume imemaliza kazi yake na ripoti imewasilishwa kwa Waziri,Kamati ya Bunge kabla ya kumfikishia Rais, " alisema. 

Mahojiano hayo yalifanyika baada ya Wazee wa Kimila wa eneo la Ngorongoro kumuomba Rais John Magufuli asikubali kupitisha mapendekezo hayo, wakidai kwamba tume hiyo iliyoundwa na Waziri haikushirikisha maoni ya wananchi. 

Kiongozi wa kimila wa kabila hilo Medukenya Nepukol alisema hata watu wachache waliojitokeza kutoa maoni walipuuzwa na hivyo taarifa itakayowasiloshwa kwa Rais haina maoni ya wananchi.

Hata hivyo, Dkt Manongi alikanusha kwa kusema kwamba maoni ya wananchi yamedhingatiwa na kutiliwa mkazo na tume hiyo.

"Hayo maoni ambayo walitaka yaingizwe kwenye Tume ni yepi mbona maoni yao yamo wametaka waruhusiwe kulima na kama wataondolewa walipwe fidia ni maoni yao na yamo katika ripoti hiyo, " alisema Dkt Manongi. 
author

Author Name

Author Description!

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

www.CodeNirvana.in

Magazeti Ya Leo

Copyright © Magazeti ya Leo, Habari Leo Tanzania, Mwananchi, Michuzi, mwanaspoti, nipashe, Udaku | Designed By Code Nirvana