Featured

    Featured Posts

NAPE: UCHAGUZI MKUU MWAKA HUU TUMPE TENA RAIS MAGUFULI ILI AMALIZIE MAMBO, AWASHUKURU WANA MTAMA NA KUAHIDI KUCHUKUA FOMU TAREHE 14, MWEZI HUU

Nape Nnauye
Mtama, Lindi
Mbunge wa Jimbo la Mtama mkoani Lindi kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Nape Nnauye amesema atawania tena nafasi ya kuwa Mbunge wa jimbo hilo akiahidi kuwa  Julai 14, 2020  atakwenda kuchukua fomu ya kuomba ridhaa ya Chama (CCM) na ana imani kuwa atateuliwa, hivyo wananchi  wamuunge mkono.

Nape amesema hayo leo Julai 3, 2020 wakati  akizungumza na wananchi katika jimbo hilo la Mtama kuwashukuru kwa kuwa pamoja kwa kipindi cha miaka mitano wakifanya kazi kwa pamoja hataua ambayo alisema imeleta mafanikio katika jimbo hilo.

Katika Mkutano huo Nape ametumia nafasi hiyo kuelezea maendeleo ambayo yamefanyika katika jimbo la Mtama chini ya uongozi mahiri wa Mwenyekiti wa CCM, Rais Dk. Magufuli akitolea mfano wa barabara ya lami kutoka Mtwara hadi Masasi.

"Barabara kutoka Mtwara mpaka Masasi imepatikana kwa sababu Rais alibana matumizi, pia amerudisha heshima ya utumishi  na ndio maana mpaka leo unawasikia watumishi wanalalama vyuma vimekaza, unajua maana yake nini hakuna semina, hakuna posho za hovyo hovyo.

Na sisi tunajua maendeleo yoyote yana maumivu yake, unataka uvune vizuri amka asubuhi nenda kalime, utaumia kwa muda lakini utakapopeleka magunia 100 gulioni unaanza kula maisha, sasa kuna watu wanataka wasiumie lakini wale maisha haiwezekani, dunia haiko hivyo", alisema Nape na kuongeza;

"Ndio maana wana Mtama nawahakikishieni tutampa tena Rais Magufuli miaka mitano amalizie kazi ya kunyoosha mambo, akishakamilisha tutakwenda na ndio utaratibu wa nchi yetu, alianza Mwalimu Nyerere akanyooshanyoosha, akaja Mzee ruksa (Mzee Ali Hassani Mwinyi) akalegeza kidogo, akaja Mkapa (Rais Mstaafu Benjamin Mkapa) ukapa ukasambaa kila mahali akakaza kidogo, akaja Jakaya Kikwete akalegeza , amekuja Mzee wetu wa Hapa Kazi Tu amekaza kidogo, baada ya hapo atakuja mwingine sijui Nape, atalegeza kidogo, mambo yatakwenda mbele.

Mimi naamini mmenielewa, nisema sana naomba mnisamehe lakini nilidhani niguse mambo Mtama yetu sasa hivi njema hebu haya mavyama tuwekeni pembeni, hakuna hata chama kimoja kimezaliwa hapa tusigombane kwa sababu ya vyama, Mtama inapendeza tukikaa wenyewe, tufurahi tuijenge Mtama yetu,".

"Nimekuja kuwashukuru kwa kuishi nanyi kwa kipindi cha miaka mitano na nimekuja kuwaambieni Julai 14, 2020 naenda kuchukua fomu kwenye Chama (CCM), ndani ya Chama changu sina mashaka nitashinda lakini baada ya kuteuliwa na chama changu naomba mniunge mkono tena  tukamilishe kazi tuliyoianza.

Tumlee mtoto wetu anaitwa Halmashauri, tukamilishe umeme kule kulikobaki, tupeleke huduma za afya kule ambako hazijafika, tuioboreshe Mtama yetu, mimi na nyie tukifanya kazi pamoja inawezekana, amueni kwa pamoja, tusonge mbele kwa pamoja." Nape alihitimisha hotuba yake.
author

Author Name

Author Description!

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

www.CodeNirvana.in

Magazeti Ya Leo

Copyright © Magazeti ya Leo, Habari Leo Tanzania, Mwananchi, Michuzi, mwanaspoti, nipashe, Udaku | Designed By Code Nirvana