Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Kassim akifurahi jambo wakati akisikiliza maelezo kutoka kwa Afisa Mkuu wa Wateja Wakubwa na Serikali wa Benki ya NMB – Alfred Shao (kulia), alipotembelea Banda la NMB kwenye maonyesho ya Saba Saba. Katikati ni Kaimu Afisa Mkuu wa Fedha wa NMB – Benedicto Baragomwa.
Maendeleo makubwa yaliyopatikana nchini katika kipindi cha kwanza cha uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano, yamechangiwa kwa namna mbalimbali na kwa kiasi kikubwa na mchango wa Benki ya NMB. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema hayo, alipotembelea banda la Benki ya NMB inayoshiriki Maonyesho ya 44 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF) yaliyoanza wiki iliyopita na yanaendelea hadi tarehe 13/07/2020. .
Hii ni pamoja na uzalendo wa viongozi wake chini ya Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo – Bi. Ruth Zaipuna, ambaye Waziri Mkuu alisema ni kati ya Wakurugenzi wanne Watanzania waliyoisaidia Serikali kuwahudumia vizuri na kuwaletea maendeleo Watanzania.
“NMB ni benki yetu…na Mkurugenzi wake ni mmoja wa Wakurugenzi sita walioichangia sana serikali ambapo wanne ni Watanzania…Kamwambieni Mkurugenzi wenu, nampongeza sana kwa kazi nzuri na kubwa anayoifanya, serikali inaitambua na kwakweli anafanya kazi nzuri sana,” Waziri Mkuu Majaliwa aliwaambia wafanyakazi wa benki waliokuwa kwenye banda la benki hiyo katika viwanja vya Saba Saba
Pongezi hizo alizitoa baada ya kumsikiliza Afisa Mkuu wa Wateja Wakubwa na Serikali wa NMB – Bw. Alfred Shao, katika hotuba yake fupi ya kumkaribisha kiongozi huyo na kumpa maelezo mafupi ya mchango wa benki hiyo katika ujenzi wa taifa na maendeleo ya nchi kwa ujumla.
Benki hiyo ni moja ya taasisi kubwa za fedha nchini ambayo tangu kubinafishwa kwake, imelihudumia taifa kikamilifu na kuchangia kwa kiasi kikubwa ukuaji wa uchumi wa nch. Maendeleo ya wananchi wa kawaida pamoja na sekta mbalimbali kama vile kilimo, kupitia huduma zake nyingi na zenye tija hasa zile za mikopo.
Kwa mujibu wa Bw. Shao, mambo yaliyofanywa na Benki ya NMB kupitia uwekezaji kwenye maeneo mengi ya kimaendeleo kwa miaka minne mpaka sasa hivi ni mengi, ikiwemo mikopo kwa sekta binafsi yenye thamani ya TZS 2 trilioni ambayo pia imesaidia kwa kiasi kikubwa kuchangia ujenzi wa uchumi wa viwanda. Benki hiyo ambayo kwa zaidi ya miaka kumi imekuwa kiongoza kwa kutengeneza faida kubwa, imetoa TZS 800 bilioni kusaidia kilimo na mnyororo wa thamani katika sekta hiyo.
Bw. Shao alisema mazao yaliyonufaika sana na mchango huo wa fedha kutoka NMB ni pamoja na pamba, mihogo, alizeti, kahawa na korosho.
“Benki ya NMB imeisaidia pia serikali kupitia kuchangia utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati. Zaidi ya TZS 1.2 trilioni imeishatolewa kusaidia miradi mikubwa ya serikali kama umeme, miradi ya maji, reli ya umeme almaarufu SGR,” kiongozi huyo mwandamizi alisema.
Waziri Mkuu Majaliwa pia alitoa pongezi maalumu kwa NMB kutokana na jinsi benki hiyo inavyopambana kuboresha maisha ya Watanzania hasa wale wa vipato vya chini wanaoishi vijijini. “Pia nawapongeza mlivyosaidia wananchi wa vijijini kufungua akaunti kupitia AMCOS,” alisema.
Post a Comment