Na Scolastica Msewa, Rufiji
Rais wa Dk. John Magufuli ameamua kumsamehe Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Rufiji Brighton Eliud Kilimba aliyetoa taarifa za uongo kuwa gari la Kituo cha Afya Ikwiriri haliwezi kutembea wakati Rais akizungumza na wananchi alipopita Ikwiriri Rufiji mkoani Pwani.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Kamanda wa mkoa wa kipolisi Rufiji Kamishina Msaidizi Mwandamizi wa Jeshi la Polisi Onesmo Lyanga amesema Uchunguzi ulifanyika kwa gari lenye namba za usajili STL 940 aina ya T/land Cruiser la Kituo cha Afya Ikwiriri na kugundulika kwamba linao uwezo wa kutembea na sio kama taarifa aliyotoa Kaimu Mkurugenzi.
Amesema “Tulimkamata tarehe 01.08.2020 kwa kosa la kutoa taarifa ya uongo na taratibu za kumfikisha mahakamani kwa kosa hilo zilikuwa zinakamilishwa, leo amepata bahati ya mtende mhe Rais ameamua kumsamehe na kwa sasa yuko huru”.
Amefafanua kuwa “mnamo tarehe 30/07/2020 majira ya tisa, eneo la Stendi ya Ikwiriri Wilaya ni Rufiji Mheshimiwa Rais wakati akiwasalimia wananchi wa Ikwiriri akitokea Mkoani Mtwara kwenye mazishi ya Hayati Benjamin William Mkapa, Rais Mstaafu wa awamu ya tatu, alipokea kero mbali mbali kutoka kwa wananchi moja wapo ikiwemo ubovu wa gari za kubebea wagonjwa katika wilaya ya Rufiji”.
Aidha Kamanda wa Polisi mkoa wa Kipolisi Rufiji anatoa wito kwa viongozi waliopewa dhamana mbali mbali za kuwahudumia wananchi wawewanatoa taarifa mbele ya viongozi wao wakiwa wamejiridhisha ukweli wa taarifa hizo kwani zinaweza kuwafanya kuingia matatani na mara nyingine wananchi kukosa imani na serikali yao.
Hata hivyo Lyanga amewataadharisha wananchi wa Rufuji kutotoa taarifa ambazo hazina ukweli kwani ni kosa kisheria
Post a Comment