Nuru Mwasampeta na Steve Nyamiti,WM
Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo azitaka Benki zilizopo nchini kushirikiana na Wizara ya Madini katika kuwawezesha kimitaji wachimbaji wadogo na wafanyabiashara wa madini ili kuwawezesha kuwekeza katika shughuli zao.
Naibu Waziri Nyongo aliyasema hayo tarehe 6 Agosti, 2020 wakati akifungua mafunzo yaliyoandaliwa hususani kwa ajili ya wafanyakazi wa benki ya CRDB yaliyofanyika katika hoteli na NAShera jijini Dodoma.
Alisema mafunzo hayo yatawasaidia wataalamu hao wa benki kuwa na uelewa wa namna shughuli za uchimbaji na biashara ya madini kwa ujumla zinavyoendeshwa.
“Biashara ya Madini ni kama biashara nyingine hivyo msisite kutoa mikopo kwa wachimbaji wadogo pindi wanapohitaji kwa ajili ya kuwekeza katika uchimbaji na biashara ya madini”. Nyongo alikazia.
Akizungumzia dhumuni la kutoa mafunzo hayo kwa taasisi za benki nchini, ambapo awali mafunzo kama hayo yalitolewa kwa watumishi wa benki ya NMB, Nyongo alisema hatua hiyo ni utekelezaji wa sera ya Madini ya Mwaka 2009 inayoitaka Serikali kuwasaidia wachimbaji wadogo wa Madini katika kutatua changamoto za mitaji zinazowakabili na kuwafanya wawekeze kwa tija.
Wizara ikishirikiana na Tume ya Madini imeona njia bora ya kuwawezesha wachimbaji hao ni kuwaunganisha na taasisi muhimu za fedha ili kutoa elimu muhimu kwa taasisi hizo zitakazowasaidia wakati wa kuhakiki taarifa za wachimbaji na wafanyabiashara wa madini pindi watakapowasilisha taarifa zao benki kwa ajili ya kuomba mikopo.
Akizungumzia matarajio ya wizara mara baada ya elimu kutolewa, Nyongo alisema benki zilizopo nchini kuwawezesha kwa kuwapa mikopo na elimu ya biashara wachimbaji wa Madini hasa wachimbaji wadogo.
Vilevile Waziri Nyongo amesema, mafunzo hayo yataendelea kutolewa kwa taasisi nyingine za fedha nchini ili kuwezesha taasisi hizo kujifungamanisha kwenye uchumi wa Madini ambayo ni sekta inayoongoza kwa ukuaji nchini.
Akihitimisha hotuba yake ya ufunguzi, Nyongo alisisitiza kuwa elimu ya biashara ya madini itaendelea kutolewa kwa wataalamu wa benki nchini ili kuwajengea uwezo wakopeshaji kutambua fursa zilizopo kwenye sekta ya madini na kuwataka kuajiri wataalamu wenye uelewa na masuala ya madini watakaoweza kuchambua michanganuo ya mikopo ya uchimbaji wa madini vile inavyostahili.
Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Profesa Shukrani Manya alisema, sekta ya madini ni sekta muhimu katika uchumi wa nchi ambayo inahitaji mitaji mikubwa katika uwekezaji wake hivyo ni muhimu kwa watoa huduma za mikopo kuwa na uelewa wa sheria na kanuni za madini.
“Sekta ya madini ni biashara kama biashara nyingine inahitaji mitaji mikubwa hivyo ninyi watu wa benki inabidi mjue vizuri suala la leseni za madini, uhai wa leseni hizo na sheria na kanuni zinazoongoza sekta hii muhimu”.
Pamoja na hayo, Prof. Manya alisema mafunzo hayo yataondoa kusitasita kutoa mikopo kwa wachimbaji wa madini mara baada ya wataalamu wa mikopo kuwa na uelewa mpana kuhusu mnyororo wa madini unaohusu wachimbaji, wauzaji, vifaa vya uchimbaji na uchakataji wa madini na watoa huduma wengine katika sekta hiyo.
Kwa upande wake, Meneja wa Dawati maalum kwa wateja wakubwa kutoka benki ya CRDB, Frederick Mwamyalla amekirii kuwa semina hiyo imekuwa na manufaa makubwa kwao na kuwawezesha kuona fursa zilizopo kwenye sekta ya madini zitakazowasaidia kuongeza mchango wao katika kusukuma mbele ukuaji wa sekta ya madini ili iweze kuchangia vilivyo katika miradi ya maendeleo.
Alisema ni muhimu kwao kama taasisi ya kifedha kuongeza nguvu na kuboresha huduma zao ili kuhakikisha mchango wa benki hiyo unaongezeka kwa kuwawezesha wachimbaji wadogo na hivyo kuinua vipato vyao pamoja na kuongeza mchango wa sekta kwenye pato la taifa.
Post a Comment