Trump alisema kupitia Twitter kuwa alizungumza binafsi katika nyakati tofauti na rais wa Lebanon Michel Aoun na rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, ambae pia atajiunga na mazungumzo hayo ya simu. Alisema amemwambia Aoun kuwa ndege kubwa tatu za Marekani zimo njiani kwenda Lebanon kupeleka madawa, chakula, maji na madaktari.
USA I Donald Trump (picture-alliance/dpa/newscom/UPI/K. Dietsch)
Rais Donald Trump wa Marekani
Trump na Macron walizungumza kwa simu na walieleza masikitiko yao makubwa kutokana na upotevu wa maisha na uharibifu mjini Beirut, msemaji wa Ikulu ya Marekani Judd Deere alisema katika taarifa.
Rais wa Lebanon hata hivyo amekataa uchunguzi wa kimataifa kuhusiana na maafa ya mripuko mjini Beirut, akisema kombora ama uzembe unaweza kuwa chanzo cha mripuko huo wakati waokoaji wanatafuta bila kuchoka watu walionusurika.
Tabaka la viongozi lililojichimbia katika utawala wa nchi hiyo limekuwa lengo la mashambulizi kwa mara nyingine tena tangu mripuko huo kutokea siku ya Jumanne, ambao umewauwa kiasi watu 154 na kuharibu sehemu kubwa ya mji huo mkuu.
Ufichuaji kwamba shehena kubwa ya kemikali hatari ya aminia nitrate ilikuwa kwa miaka kadhaa katika bohari katikati ya mji mkuu Beirut umekuwa ni ushahidi wa kushitua kwa wengi wa watu wa Lebanon kuhusiana na kuoza kwa kitovu cha mfumo wao wa kisiasa.
Wakati huo huo waraka mpya uliopatikana unaeleza kuwa kwa karibu mara 10 katika miaka sita iliyopita maafisa kutoka idara ya forodha ya Lebanon, jeshi, idara ya usalama na mahakama walieleza wasi wasi wao kuwa shehena hiyo kubwa ya kemikali zinazoweza kuripuka zimewekwa bila kuzingatia usalama katika bandari katikati ya Beirut.
Post a Comment