Kampuni ya Huduma za Meli Nchini (MSCL) imetangaza rasmi kurejea kwa safari za meli ndani ya ziwa Victoria kutoka Mwanza kwenda mkoani Kagera na Kutoka Mwanza kuelekea visiwa vya Ukerewe baada ya kukamilika kwa ukarabati wa meli zinazohusika na safari hizo.
Akizungumuzia kurejea kwa safari hizo juzi jijini Mwanza, Afisa Mtendaji Mkuu wa MSCL Eric Hamis alisema meli zilizokuwa zinafanyiwa ukarabati ni Mv Victoria ambayo sasa itafahamika kama New Victoria Hapa kazi tu na Mv Butiama ambayo sasa itafahamika kama New Butiama hapa kazi tu zitaanza rasmi safari zake agosti 16 mwaka huu.
Eric alisema kuanza kwa safari hizo ni baada ya kukamilika kwa ukarabati wa meli ulioigharimu serikali jumla ya Sh. Bilioni 28 kwa meli zote mbili, kufanyiwa majaribio ya safari za kawaida na mizigo pamoja na kupatiwa cheti cha ubora kinachoruhusu utoaji huduma kilichotolewa na Wakala wa Huduma za Meli Nchini (TASAC).
Eric alisema meli ya New Victoria Hapa kazi tu itafanya safari zake kutoka Mwanza hadi Bukoba mkoani Kagera kupitia Kemondo kila siku ya jumapili, jumanne na alhamis saa tatu na nusu usiku ambapo gharama za usafiri kwa abiria zitakuwa ni sh. 16,000/= kwa daraja la uchumi, 30,000/= kwa daraja la biashara na 45, 000/= kwa daraja la kwanza.
Alisema kuhusu meli ya New Butiama Hapa Kazi tu itakuwa inaanzia safari zake Nansio Ukerewe kuja Mwanza kila siku saa mbili na nusu asubuhi na kurejea Ukerewe kutoka Mwanza saa tisa na nusu jioni ambapo itakuwa na madaraja mawili ya abiria ambao watalipia sh.8000/= kwa daraja la uchumi lenye uwezo wa kubeba abiria 180 na sh.10,000/= kwa abiria wa daraja la kwanza lenye nafasi za abiria 20.
Eric alieleza meli ya New Victoria Hapa Kazi tu itakuwa na uwezo wa kubeba abiria 1200 na Tani 200 za mizigo ambapo gharama ya tani moja ya mizigo itaghramu kiasi cha sh. 27,000/= tu ili kutoa fursa kwa wakulima na wafanyabiashara wa mazao kusafirisha mizigo yao pasipo changamoto yeyote.
Kaimu Meneja Masoko na Biashara wa MSCL, Philemon Bagambilana alisema wameweka upatikanaji wa tiketi kwa njia ya mtandao kwa kuingia wovuti ya www.mscl.co.tz inayomupa abiria fursa ya kuchagua safari, daraja, idadi ya abiria wanaosafiri, sehemu ya kulipia na atapewa control namba na ataruhusiwa kuchapisha tiketi yake na pia wanapokea maoni ya wateja kupitia namba +255 739 606 600.
Mkuu wa Bodi ya Utalii Kanda ya Ziwa, Gloria Munhambo alisema kurejea kwa safari za meli ziwa victiria kutachagiza kukua kwa utalii kwa mikoa ya kanda ya ziwa hasa Kagera, Mwanza na Visiwa vya Ukerewe kwani kwa nyakati tofauti wamekuwa wakipokea taarifa kutoka kwa watalii wakiulizia kuhusu usafiri wa majini ambao umekuwa kivutio kikubwa kwao.
Post a Comment