Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la SPRF nchini, Dk Suleiman Muttani akizungumza kwenye kikao hicho.
Baadhi ya wajumbe wakifuatilia mada mbalimbali zilizokuwa zikiwasilishwa.
Afisa Maendeleo Wilaya ya Ikungi Haika Massawe akizungumza.
Dk Philipo Kitundu (kulia) akiwa na Afisa Maendeleo Wilaya ya Ikungi Haika Massawe kwenye kikao hicho.
Kikao kikiendelea.
Afisa Elimu Wilaya ya Ikungi, Ngwano J. Ngwano akizungumza.
Mtendaji wa Kata ya Dung’unyi , Yahaya Njiku akizungumza.
Mtendaji wa Kijiji cha Siuyu, Rebeca Ngubita akizungumza kwenye kikao hicho.
.
Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Ikungi, SSP Fortunatus Biyacca akizungumza katika kikao hicho. |
Na Godwin Myovela, Singida
JIOKOE NA UMASKINI yaani Stars of Poverty Rescue Foundation (SPRF) ni Shirika lisilo la kiserikali ambalo siku hadi siku limekuwa likiakisi kwa vitendo malengo ya kuanzishwa kwake, ikiwemo utetezi wa haki na usawa wa kijinsia kwa wanawake, watoto na makundi mengine athirika.
Tangu kusajiliwa kwake takribani miaka sita iliyopita, SPRF imekuwa na kasi ya aina yake kwenye nyanja ya uwajibikaji, sanjari na ‘ari’ ya kujitoa na kuijali jamii, hususani kwenye maeneo ya kupunguza umaskini wa kipato na kutoa huduma za afya.
Shughuli nyingine za kikatiba zinazofanywa na shirika hilo ni pamoja na kujenga uwezo wa shirika endelevu na wadau wanaolizunguka ili kujiletea maendeleo.
Mkurugenzi Mtendaji wa SPRF nchini, Dkt Suleiman Muttani anasema kwa sasa shabaha iliyopo ni kuhakikisha wanaendeleza kasi ya kutekeleza mradi wa AWARE, baada ya kukamilika kwa kikao cha kimkakati cha kurasimisha mradi huo kwa mwaka 2020, kilichofanyika hivi karibuni.
“Kikao hicho tayari kimekwisha-fanyika na kilihusisha viongozi wa Wilaya ya Ikungi mkoani hapa, pamoja na watekelezaji wote wa sera na sheria, na kikubwa tuligusia masuala yaliyojitokeza wakati wa utekelezaji wa mradi kwa mwaka 2019, na tuliweka malengo na mwelekeo wa pamoja wa utekelezaji wake kwa mwaka 2020,” anasema Dkt Muttani.
Mkurugenzi huyo anasema kwa kipindi kirefu sasa, takribani miaka 4, SPRF chini ya ufadhili wa Foundation for Civil Society (FCS) imekuwa ikitekeleza mradi wa AWARE ndani ya Wilaya ya Ikungi unaofanya utetezi wa haki za wanawake na mtoto wa kike dhidi ya athari zitokanazo na mila na desturi zilizopitwa na wakati.
Muttani ambaye pia ni Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Wanawake nchini, anafafanua kwamba nguvu kubwa ya shirika hilo kwa sasa imeelekezwa zaidi kwenye Kata 2 za Siuyu na Dung’unyi kutokana na maeneo hayo kukithiri kwa matukio ya ukeketaji, mimba na ndoa katika umri mdogo, sanjari na ukatili dhidi ya wanawake na watoto na hasa mtoto wa kike.
Aidha, mara kadhaa aliishukuru serikali, FCS na wadau wengine kwa namna wanavyojali na kutambua juhudi mbalimbali zinazofanywa na SPRF katika mapambano ya kupinga na kufichua vitendo vya matukio ya ukatili wa kijinsia ndani ya jamii.
“Nakutaarifu Mkuu wangu wa Wilaya kuwa shirika letu limepata ruzuku ya milioni 30 kuendelea na utekelezaji wa mradi wa ‘AWARE’ kwenye Kata za Siuyu na Dung’unyi kutoka ‘the Foundation for Civil Society 2020,” anaeleza Muttani.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Edward Mpogolo, kupitia hotuba yake iliyowasilishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya hiyo Justice Kijazi, wakati wa kikao cha kurasimisha mradi wa AWARE kwa mwaka 2020, alisema anashukuru na kuupongeza uongozi wa SPRF nchini kwa kutekeleza mradi huo kwa ufanisi mkubwa.
“Mradi huu upo hapa Ikungi kwa miaka minne sasa…na sote tunashuhudia jinsi mradi huu unavyoendelea kuleta matokeo chanya katika vita dhidi ukeketaji, mimba na ndoa za utotoni kwa vijana wetu walio katika umri mdogo, “ anasema Mpogolo.
Anasema mradi huo ulipiga hodi Ikungi mwaka 2017 na umeendelea kutekelezwa kwa mafanikio makubwa hadi kufikia Februari 2020. Na katika kipindi chote hicho walengwa wapatao 303, 944 walifikiwa.
Miongoni mwa idadi hiyo, walengwa wa moja kwa moja walikuwa 7932 huku wale wasio wa moja kwa moja idadi yao ikiwa ni 296,012.
“Kwa taarifa zilizopo walengwa wa moja kwa moja walifikiwa na SPRF wenyewe, na wale wasio wa moja kwa moja wakifikiwa na vikundi vya Sauti ya Mwanamke, Sauti ya Wanafunzi na Kamati za Ulinzi wa Mwanamke na Mtoto za vijiji (MTAKUWWA) chini ya uratibu wa SPRF,” anasema Mpogolo.
Mkuu huyo wa wilaya anasema njia zilizotumika kusambaza elimu na kuhamasisha ni pamoja na redio, magazeti, vipeperushi, majarida na mitandao ya kijamii.
Mpogolo Anaeleza kufurahishwa kwake na ushiriki wa Kamati za MTAKUWWA ngazi ya vijiji, Sauti za Wanawake za vijiji na zile za Wanafunzi hasa kutoka shule za Sekondari za Siuyu na Munkinya, Mungaa, Dadu, Puma na Miandi wakati wa utekelezaji wa mradi huo.
Anasema vikundi hivyo vimekuwa chachu ya mabadiliko kwenye jamii zao, vikijikita katika kuhamasisha na kueneza elimu dhidi ya ukatili wa kijinsia, ikiwa pamoja na kutembelea wenzao, kucheza ngoma zenye ujumbe na maudhui maalum, maigizo, mashairi, ngonjera na kufanya malumbano ya hoja.
“Kwenye eneo hili kauli yao ilikuwa ni ‘Simama Sema kwa Sauti Usikike:’ Ukimkata Hatulii,” anasema Mpogolo kupitia hotuba yake iliyosomwa na Mkurugenzi wa Ikungi, Kijazi.
Anatoa wito kwa jamii na wadau kuendelea kushikamana na kushiriki kikamilifu katika kukabiliana na ukatili wa kijinsia katika sura zote…
“Hapa SPRF wametukumbusha wajibu wetu, na wametupa kazi ya kufanya, basi; na tuifanye kazi hii, na tuwe sote, tushirikiane nao katika kuwabaini na kuwaibua wote wanaofanya vitendo vya ukatili wa kijinsia kwenye maeneo yetu…lakini bila kusahau kuwasaidia wahanga wa ukatili ili wapate haki stahiki,” anasema Mpogolo kwa kumalizia.
Post a Comment