Na Bashir Nkoromo, Kinondoni
Mwenyekiti wa Taifa wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Heri James amesema wapinzania wanatumia 'akili ndogo' kujaribu kujenga hoja kwamba Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupitia kwa Mwenyekiti wake Rais Dk. John Magufuli kinakosea kuleta maendeleo nchini kwa kuwekeza nguvu katika ujenzi wa maendeleo ya vitu badala ya kuanza na maendeleo ya watu.
Amesema, mbali na kudhihirisha kwamba kwa kusema hivyo wapinzania hawana hoja ya kupiku sera za CCM, lakini pia kulingana na imani za kidini wanakiuka hekma ya Mwenyezi Mungu, ambayo inafundisha kwamba inatakiwa binadamu kuwekewa miundombinu ya vitu ambavyo vinamwezesha kuishi na kupata maendeleo.
James alisema hayo jana katika hotuba yake wakati akizindua Kampeni za CCM za Ubunge Jimbo la Kinondoni katika mkutano uliohudhuriwa na maelfu kwa maelfu ya wananchi katika Viwanja vya Biafra Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.
"Askofu Gwajima yupo hapa, ni shahidi, hata katika vitabu vya Mungu imeandikwa ya kwamba Mungu kabla ya kumuumba Binadamu kwenye Uumbaji wake alianza na Mbingu na ardhi kisha akaweka na viumbe mbalimbali ikiwemo mimea, ndiyo akamuumba binadamu. Sasa hawa wapinzani hawajui hekma ya hili, kwamba Mungu alifanya hivyo ili atakapomuumba binadamu vitu alivyotanguliza kuumba ndivyo vimuwezeshe huyo binadamu kuishi na kupata maendeleo", alisema na kuongeza.
"Rais Dk. Magufuli alivyoweka jitihada katika ujenzi wa vitu kama barabara, ununuzi wa ndege, ujenzi wa hospitali, vituo vya afya na zahanati na Reli ya kisasa, lengo kuu ni kutaka vitu hivi viwe ndiyo vichocheo vya kuleta maendeleo kwa wananchi, kwa hiyo wapinzania wanapobeza hatua hizi wanakuwa ni watu wa kushangaza sana"
Akizungumzia wapinzania kulalamikia juu ya baadhi ya wagombea wa vyama vyao kuenguliwa kwenye kinyang'anyiro cha uchaguzi kutokana na kushindwa kujibu pingamizi dhidi ya makosa katika fomu zao za kuomba ridhaa ya kugombea, James alisema hilo halikutokana na maelekezo ya CCM bali ni kwa mujibu wa sheria.
Alisema, hakuenguliwa hata mgombea mmoja wa CCM kwa sababu ya siri moja amabayo aliitaja kuwa ni kutokana na CCM kuwa Chama kikubwa chenye uzoefu na weledi wa miaka mingi katika masuala ya uchaguzi, hivyo wagombea wake kwanza walifundwa njia zote anazopaswa kuzingatia mgombea na pia wagombea walisimamiwa na fomu zao kuhakikiwa na wataalam wa CCM wa masuala ya uchaguzi kabla ya kupeleka fomu zao Tume ya Taifa ya Uchaguzi.
"Sasa hawa wapinzania, unakuta mtu anaomba udiwani hana wa kumsimamia, anajaza fomu yake akiwa nyumbani yeye na mkewe asubuhi anaipeleka Tume ya Uchaguzi, bila kuhakikiwa na mtaalamu yeyote, sasa unatarajia kweli fomu hizi zitakuwa na maelezo sahihi au zitakosa kuwa na makosa?" alisema na kuhoji.
Akimuombea kuraTariba baada ya kuomba za Mgombea Urais kwa tiketi ya CCM Rais Dk. John Magufuli, James alisema wana Kinondoni wamepata mtu sahihi, kwa kuwa siyo Mgeni katika Uongozi kwa kuwa amewahi kuongoza katika maeneo mbalimbali ikiwemo Udiwani wa Hananasif na pia ni mwanamichezo kindakindaki kwa kuwa hakuna anayeweza kuzungumzia maendeleo ya michezo nchini ikiwemo soka akimtaje Tarimba.
Mkutano huo, ambao ulishajihishwa na wasanii mbalimbali akiwemo Harmonize, ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Daniel Chongolo na Mgombea Ubunge jimbo la Kawe Askofu Dk. Josephat Gwajima ambaye uzinduzi wa kampeni zake unafanyika leo katika Viwanja vya Bunju B, Dar es Salaam.
Post a Comment