Na Bashir Nkoromo, Ubungo
Kamati za Afya za Kituo cha Afya cha Sinza na Zahanati ya Malamba Mawili katika Manispaa ya Ubungo jijini Dar es Salaam, zimetakiwa kuhamasisha wananchi katika makundi mbalimbali ya kijamii kujiunga na huduma ya Bima ya Afya ikiwa ni sehemu ya kutimiza wajibu wao.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo Beatrice Dominic wakati akizindua Kamati hizo, katika hafla iliyofanyika jana katika Ukumbi wa Lapaz, katika Manispaa hiyo, na kuongeza kuwa pamoja na kuhamasisha wananchi kujiunga na Bima ya Afya, pia Kamati hizo zinatakiwa zihakikishe zinashirikisha wadau wa maendeleo katika kuboresha afya ya jamii.
Aliwafunda wajumbe wa Kamati hizo kwamba kazi zao siyo kwenda katika ofisi au Kituo cha Afya au zahanati na kuanza kukagua mapato na matumizi au shughuli zingine bali ni kuhakikisha wanasimamia na kuchambua kwa makini taarifa watakazokuwa wakipatiwa na watendaji kuhusu huduma za afya na kisha kuelekeza au kutoa ushauri pale panapostahili.
Mkurugenzi huyo amewataka pia wajumbe wa kamati hizo kuhamasisha wananchi wenye Bima za Afya kwenda kupata huduma za afya katika Kituo cha Afya cha Sinza na Zahanati ya Malamba Mawili kwa sababu hivi sasa Serikali imeziboresha na zinatoa huduma nzuri.
Alisema, pamoja na wananchi kwenda katika Kituo na zahanati hiyo kupata huduma bora, lakini pia kwa wale wenye bima za afya watakuwa gharama za matibabu yao zitakazokatwa kwenye bima zao za afya zitarejea katika Manispaa ya Ubungo na hivyo kurudi kuwanufaisha wananchi hao baadaye.
"Sasa jambo hili ni muhimu niwafafanulie, mtakapokwenda kupata matibabu katika Hospitali za binafsi gharama za bima zenu mtakazokatwa zitaenda kwa watu binafsi hivyo hazitawasaidia tena, lakini mkienda kutibiwa katia Kituo na Zahanati za serikali gharama zitarudi serikalini na kuwanufaisha tena", alisema Mkurugenzi huyo.
Akizungumzia Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wagunge na Madiwani uliopangwa kufanyika siku ya Jumatano, Oktoba 28, mwaka huu, Mkurugenzi huyo aliwataka wananchi wa Ubungo kuhakikisha kila mmoja anajitokeza siku hiyo na kupiga kura kumchagua kiongozi ambaye atalijenga Taifa.
Mabaraza hayo kwa kawaida hufunguliwa na Diwani, lakini Mkurugenzi huyo amelazimika kufungua kwa kuwa kipindi hiki ndiyo unafanyika mchakato wa kupatikana madiwani wapya katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika siku hiyo ya Jumatano, Oktoba 28, mwaka huu.
MATUKIO MBALIMBALI KATIKA PICHA HAYA HAPA👇👇
Post a Comment