UONGOZI ni kuonyesha njia, tena bila woga. Hicho kimedhihirika Tanzania, na dunia nzima sasa wanakiri kwamba Rais John Magufuli ni kiongozi mahiri na kwa hakika wapo wanaoitamani na kuionea wivu Tanzania kwa kuwa na kiongozi wa aina hii.
Ni rahisi sana Watanzania kuona namna taifa lilivyovuka janga la korona kama suala la kawaida tu, lakini kwa hakika siyo kawaida. Uthubutu alioonyesha Rais John Magufuli katika kuvusha Tanzania kwenye janga hili hatari ni aina ya uongozi wenye neema zote za Mwenyezi Mungu.
Ukitazama jinsi mataifa mengine wanavyoshughulikia ugonjwa huo na ambavyo wananchi wao walivyoteseka na hata kufilisika kutokana na misimamo ya serikali zao kuhusu korona, utaelewa ni kwanini Rais Magufuli ni wa kipekee.
Wapo watanzania wengi, pengine hata wewe msomaji wa makala haya, mwanzoni ulikuwa na wasiwasi juu ya masimamo wa serikali ya Rais Magufuli kuhusu Korona. Ushawishi wa nje ulifikia kiasi cha kutuchota akili hata sisi wenyewe kama watanzania kuamini kwamba rais wetu anakosea namna ya kushughulika na Korona.
Lakini kama ilivyo kanuni ya maisha, njia ya muongo huwa ni fupi na tena Mungu hamfichi mnafiki. Hatimaye ukweli umedhihirika, maisha ya watanzania yanaendelea kama kawaida, bila kufungiwa, na dunia imebaki inaumbuka.
Sasa hivi huwezi kusikia tena kwenye vyombo vya habari vya kimataifa wanazungumzia kuhusu Korona katika nchi yetu ya Tanzania. Mwanzoni kila mtu wakiwemo watanzania wenzetu mitandaoni kulijaa dhihaka dhidi ya taifa letu na serikali yake, kisa tunamtegemea Mungu badala ya wanasayansi, tena tunajielekeza kwenye tiba za kujifukiza zisizoidhinishwa na wanasayansi.
Mungu wetu amesimama na taifa letu, amesimama na Rais Magufuli, Tanzania imekombolewa kwa jina la Mwenyezi Mungu, hekima ya ulimwengu na ya kidunia imeshindwa, hekima ya Kimungu imeiokoa Tanzania.
Kupita katika shinikizo hilo kubwa haikuwa kazi rahisi kwa kiongozi wa nchi, kwamba kila siku dunia ilikuwa inaimba wimbo mmoja na kiitikio kile kile, bila kujali mazigira ya nchi husika, kwa kuwa wakubwa walitaka dunia yote iwe sare sare na iimbe wimbo wenye korasi moja, ilitarajiwa kuwa kitikio hicho kitakuwa na mvumo wa pekee hasa kwa nchi za dunia ya tatu.
Dunia ilibaki inashangaa, pale nchi moja kutoka Pwani ya Afrika Mashariki, ilipoanza kusikika sauti ya wimbo tofauti na dunia nzima. Mwanzoni dunia ilidhani wanasikia vibaya, kwamba huenda mawimbi na upepo wa Bahari ya Hindi, unafanya sauti isisikike vizuri, lakini imani yao ilikuwa kwamba wote tunaimba wimbo ule ule.
Kadiri muda ulivyosonga mbele ilizidi kudhihirika kuwa kumbe Tanzania chini ya jemedari wake, Rais magufuli ilikuwa inaimba wimbo tofauti, kwa taharuki dunia ikajidai kutuhurumia, eti tunapotea, wataalamu na mawakala wao wakaanza propaganda za kututisha tunapotea.
Wakaenda mbali kiasi cha kutabiri tutaanza kushushudia maiti zinaokotwa barabarani, kutoka na ‘ukaidi’ wetu wa kuitikia wimbo wa ukombozi unaoimbwa na dunia.
Tulipoendelea kudumu katika wimbo wetu wa kumtumainia Mwenyezi Mungu na tiba asili zinazotokana na matunda aliyoyaumba na kuyaweka bustanini Edeni, wakaanza uzushi kwamba hospitali zetu zimelemewa na wagonjwa, baadhi ya wenzetu wakaanza kuamini kinachosemwa kutoka London na Washington, kuwa Hospitali ya Amana imezidiwa wagonjwa, yaani hata anayeishi Ilala, pembeni tu ya Amana aliamini yaliyotoka huko wakati haoni dalili zozote zisizo za kawaida hapo jirani yake.
Hatimaye ukweli umedhihirika, wimbo wa dunia umezimwa hawauimbwi tena, wanasimama kusikiliza kwa mbali wimbo pekee uliobaki wa ushujaa wa Tanzania na Mungu wake, waliokuwa mstari wa mbele kuhanikiza utabiri wa balaa litalotukuta sasa wako kimya.
Twitter za mabalozi wa nchi za magharibi haziandiki tena, wanaona haya, wameumbuka, ramli chonganishi walizokuwa wakipiga kuhusu hatma ya Tanzania na korona sasa zimewarudi, Tanzania inasonga mbele.
Nyuma ya yote haya yupo Rais John Magufuli, haikuwa kazi rahisi kusimama imara dhidi ya wakubwa wa dunia, waliokuwa wanatutisha kwa kila namna, ujasiri na ushujaa wake leo umeipa Tanzania heshima kubwa duniani.
Baada ya kuonyesha ushujaa wa kiuongozi namna hiyo, kwa hakika hatuwezi kujitendea haki sisi wenyewe na Tanzania yetu kama hatutamchangua kwa kura nyingi Rais Magufuli ikifika Oktoba 28, 2020.
Nasema hivi kutokana na hali halisi, umeshajiuliza hivi kingetokea nini kama tungekuwa na mtu mwingine kama kiongozi wa nchi. Kama chama kikuu cha upinzani walikosa hata ujasiri wa kuendelea na vikao vya bunge, wangepata wapi ujasiri wa kuwaruhusu wafanyabiashara wa Kariakoo waendelee na shughuli zao? Hilo lingefanyika leo Tanzania ingekuwa wapi?
Hebu fikiria maisha yangekuwaje, nchi ingekuwa kwenye lockdown (imefungiwa) shule zingekuwa zimefungwa na wanafunzi wangelazimika kurudia madarasa mwakani, jiji la Dar es Salaam na miji mingine ingekuwa imefungwa, hakuna mawasiliano kati ya mji na mji, maduka na huduma zote zimefungwa, hakuna mmachinga au kibarua kwa miezi sita tangu machi mpaka sasa, tungekuwa wageni wa nani?
Watu wasiuchukulie poa uamuzi wa Rais Magufuli kusimama imara na kupigana na kila aina ya shinikizo la kumtaka afuate mkumbo wa dunia inavyotaka bila kujali mazingira yetu yakoje. Hii ni ishara ya uwezo mkubwa wa uongozi, msimamo usioyumba na mtetezi wa kweli wa wananchi wake wanyonge.
Heshima peke yake tunayoweza kumpa Rais Magufuli ni kumchagua kwa kura nyingi ili apate ushindi wa kishindo katika Uchaguzi Mkuu Oktoba 28, ameonyesha kwa vitendo dhahiri shhiri kwamba anastahili kura zetu zote, kwa jinsi anavyotutetea Watanzania wanyonge. Hana wa kuinganisha naye, anastahili miaka mingine mitano kwa heshima kubwa.
*Magufuli Mitano Tena*
Post a Comment