Featured

    Featured Posts

OKASH: SITOLALA NITAZISAKA KURA ZA DK MAGUFULI POPOTE SOKONI, VIJIWE VYA KAHAWA, MAMA LISHE HADI VILABU VYA POMBE.

Mgombea Ubunge Viti Maalumu Mkoa wa Dodoma kupitia CCM,  Halima Okash akiomba kura kwa unyenyekevu  za wagombea wa CCM katika moja ya mikutano ya kampeni Jimbo la Mvumi, Dodoma.

Okash akioomba kura huku akiwa ameinama ikiwa ni ishara ya utii na unyenyekevu kwa wapiga kura.



 Halima Okash (aliyeshika kipaza sauti) akimwaga sera za CCM alipowaongoza wanawake kwenye vilabu vya pombe katika Kata ya Nhinhi, Jimbo la Mvumi, Dodoma kuwaombea kura wagombea wa CCM hivi karibuni.


Na Mwandishi Wetu

MGOMBEA Ubunge Viti Maalumu Mkoa wa Dodoma, Halima Okash amesema hatokata tamaa hadi ushindi mnono kwa CCM upatikane, aahidi  kuendelea  na utaratibu wake wa kuzisaka kura mahali popote kwenye masoko, vijiwe vya kahawa,  Mama Lishe, vilabu vya pombe hadi Saluni.

Okash, ambaye baadhi ya viongozi na wananchi wanamwita mwanamke jasiri na mpambanaji, tangu ameanza kampeni hadi sasa hajakata tamaa, amekuwa akihaha huku na kule kuzisaka kura za Mgombea Urais wa CCM, Dk. John Magufuli, wagombea Ubunge wa CCM na wagombea udiwani wa chama hicho.


"Hadi kieleweke mpaka ushindi upatikane, sitolala wala sitaona haya kumuendea mtu yeyote au kundi lolote la jamii hata mpinzani kumuomba kura kistaarabu ili Oktoba 28 mwaka huu wawapigie kura wagombea wa CCM chama chenye nia ya dhati ya kuwaletea maendeleo watanzania," alisema Okash kwa msisitizo.


Hivi karibuni baada ya kufanya kikao cha ndani na wanawake  katika Kata ya Nhinhi Jimbo la Mvumi, aliwaongoza akina mama kwenda kwenye vilabu vya pombe ambapo alimwaga sera za CCM na kuwaomba kura vijana kwa wazee  waliowakuta wakistarehe kwa pombe za kienyeji.

Okash anasema aliamua kuchukua uamuzi huo baada ya kuona asilimia kubwa ya wanaume hawahudhurii mikutano ya kampeni. 

Walipofika kwenye vilabu vya pombe ambapo asilimia kubwa wanywaji walikuwa wanaume vijana kwa wazee, Okash aliwasalimia kwa heshima za mila na desturi za kiafrika na kuanza kumuombea kura Dk. Magufuli, Mgombea Ubunge wa Jimbo la Mvumi, Livingstone Lusinde na Mgombea Udiwani wa kata hiyo, Msafiri Mdandalu.

Alitumia fursa hiyo kuinadi Ilani ya CCM ya Uchaguzi kwa kuelezea mambo mazuri yaliyomo humo kuhusu yatakayotekelezwa katika jimbo la Mvumi, Mkoa wa Dodoma na jinsi wazee watakavyosaidiwa, vijana kupata mikopo yenye riba nafuu ambapo pia wanawake na walemavu wataipata.

Akielezea kuhusu tukio hilo la kushtukiza, Mzee Mathayo Mazengo mmoja wa wanywaji, alisema kuwa kwanza walistuka kuona kundi la wanawake wakiwemo pia wake zao wakiwaendea eneo walililokuwa wakistarehe, lakini baada ya Okash kuwaelezea lengo lao na kuwaomba kura kistaraabu walifurahi na kukubaliana naye.

Mazengo anasema, huyo binti (Okash), ni jasiri na mpambanaji mzuri, tena ana lugha nzuri ya ushawishi kiasi kwamba hata asiyeipenda CCM ni rahisi kukubaliana naye.


Tukio lingine alilolifanya Okash ni pale alipoambatana na Katibu wa Umoja wa Wanawake (UWT) CCM Mkoa wa Dodoma, Sophia Kiwanga kwenda kuzisaka kura kwa Mama Lishe, Saluni za kike na kiume pamoja na vijiwe vya kahawa katika mitaa mbalimbali ya Jimbo la Chemba.

Pamoja na kumuombea kura Mgombea urais wa Tanzania kupitia CCM, Dk John Magufuli, na wagombea wengine wa chama hicho,  lakini vilevile waliunga mkono biashara zao kwa kununua vyakula na kunywa kahawa huku wakimwaga sera pamoja na kuelezea mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na mgombea huyo.

Okash na baadhi ya viongozi wa CCM walipita katika Kata mbalimbali za Chemba ikiwemo Kata ya Msaada, ambapo walikutana na watu wa kada tofauti, wakiwemo wazee, vijana, wanawake, Mama Lishe na wauza kahawa.

Wengi wa waliowatembelea na kuwaeleza mafanikio ya Serikali ya CCM inayoongozwa na Dk. Magufuli, walifurahi kuwaona viongozi hao na kufarijika kwa kuthaminiwa, hivyo kuahidi kumpigia kura Dk Magufuli, wabunge na madiwani wa CCM katika uchaguzi utakaofanyika Oktoba 28, mwaka huu.

"Kitendo hiki hiki cha kuzitembelea kada hizi hata sisi kimetupa faraja,ambapo licha ya sisi kuwaeleza mafanikio aliyoyafanya Dk. Magufuli, lakini hata wao pia walielezea na kutaja baadhi ya miradi mikubwa inayofanyika katika uongozi wake, ikiwemo; ujenzi wa barabara ya lami ya Dodoma-Manyara, kuunganishiwa umeme kwa gharama ya  27,000, ujenzi wa Reli ya kisasa ya Dar- Dodoma, ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato na kuhamishia makao makuu ya nchi Dodoma," alisema Okash.

Akiwa katika kikao cha ndani cha kampeni za CCM katika kata Bumbuta, Okash alipiga magoti kwa unyenyekevu na kuanza kumuombea kura Diwani wa Kata hiyo, Shamte Kapesa, kitendo kilichowashangaza baadhi ya wanawake  kuanza kutokwa na machozi ya furaha miongoni mwao akiwa mke wa mgombea huyo, Amina Sompa.

Alipoulizwa Amina kwamba kilichomliza ni nini? Alijibu kuwa imekuwa vigumu kuzuia machozi, kwani alikuwa haamini kama mumewe Kapesa ipo siku atakuja kupigiwa kampeni kwa unyenyekevu na mwanamke wasiye fahamiana naye hata siku moja, kama alivyofanya Okash na kwamba Mungu azidi kumpa uzima na baraka tele katika maisha yake.

Naye Mwahija Mohamed mmoja wa akina mama waliohudhuria kikao hicho alipoulizwa kuwa ni sababu ipi imewafanya wabubujikwe na machozi? Alijibu kuwa hawajawahi kuona mwanamke mwenye imani na uthubutu wa aina yake akipiga magoti kwa unyenyekevu kumuombea kura mwanaume ambaye siyo mumewe, lakini pia maneno aliyokuwa anayasema yaliwaingia moyoni.

Mwahija alisema, Okash ni mwanamke shupavu na atakuja kuwa mwanasiasa mzuri siku za usoni, anajua kupangilia maneno ya kampeni yenye ushawishi utakaowafanya wanaomsikiliza hata wakiwa wapinzani wabadilike na kuamua kuwapigia kura wagombea wa CCM.

Okash tayari amefanya mikutano ya kampeni ya ndani na hadhara kwa mafanikio na kuacha alama za ushindi kwa CCM katika Kata mbalimbali za majimbo ya Kondoa Vijijini, Kondoa Mjini, Chemba na Mvumi.







author

Author Name

Author Description!

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

www.CodeNirvana.in

Magazeti Ya Leo

Copyright © Magazeti ya Leo, Habari Leo Tanzania, Mwananchi, Michuzi, mwanaspoti, nipashe, Udaku | Designed By Code Nirvana