Mwenyekiti wa (CCM) Mabala Mlolwa akipiga ngoma ya Kabila la wasukuma(Waswezi) katika Uzinduzi wa Kampeni za Udiwani kata ya Malunga jana (Picha na Salvatorya Ntandu).
Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Shinyanga kimewaomba wananchi kuwa makini na baadhi ya wagombea wa vyama vya Upinzani wanaopita katika maeneo yao kuomba kura kwa kutumia lugha zenye kuwagawa sambamba na kubeza shughuli za maendeleo zilizotekelezwa na serikali ya awamu ya Tano chini ya Rais Dk John Pombe Magufuli.
Kauli hiyo imetolewa Jana na Mwenyekiti wa (CCM) mkoa wa Shinyanga Mabala Mlolwa wakati akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara wa uzinduzi wa kampeni za Udiwani wa kata ya Malunga katika Jimbo la Kahama Mjini,ambapo aliwataka wananchi kuwapuuza wagombea wasio kuwa na Ilani za uchaguzi wanaotumia majukwaa kubeza kazi zilizotekelezwa na Dk Magufuli.
Alisema kuwa wagombea wa vyama vya Upinzani wameshindwa kunadi sera na zilizopo katika Ilani zao za uchaguzi na badala yake wamekuwa wakilalamika majukwaani bila sababu za msingi kwa kusema kuwa kwa kipindi cha miaka mitano CCM hajafanya chochote kwa wananchi hoja ambayo ni dhaifu na haina ukweli wowote.
“Inawezekana Wapinzani wetu wanatumia miwani za mbao, hivi ni kweli Serikali ya Rais Dk Magufuli kwa kipindi cha miaka mitano hajafanya kitu chochote, hata Elimu bure hawaioni, ujenzi wa madaraja, Zahanati na vituo vya afya, barabara,umeme na Maji,”alisema Mabala.
Mabala aliwataka wananchi wa Jimbo hilo kuwapuuza kwa kutowasikiliza na badala yake wawachague wagombea wa CCM wakianza ngazi ya Udiwani wa Kata hiyo Joseph Mipawa, Mbunge Jumanne Kishimba na Rais, Dk John Pombe Magufuli ili waendelee kutekeleza kazi za maendeleo zilizoainishwa katika ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2010/25.
Kwa Upande wake Mgombea Ubunge wa Jimbo la Kahama Mjini Jumanne Kishimba (CCM) aliwataka wananchi kuendelea kukiamini chama hicho kwani katika Ilani ya iliyopita ya 2010/20 waliweza kutekeleza shughuli za maendelea kwa vitendo kama vile ujenzi wa hospitali ya Mji kahama,Kituo cha afya Nyasubi na Iyenze.
“Endapo mtanipa ridhaa ya kuongoza jimbo hili kwa kipindi cha miaka mitano ijayo nitahakikisha naisimamia serikali kwa kujenga miundombinu ya barabara na mitaro katika mitaa mbalimbali ya Kahama Mjini,na hivi karibuni Benki ya dunia inatarajia kujenga barabara zaidi ya kilomita 28 kwa kiwango cha lami katika jimbo letu,”alisema Kishimba.
Aliwaomba wananchi wa Jimbo hilo ifikapo Octoba 28 mwaka huu wakamchague Rai Magufuli,Wabunge na Madiwani wote wa (CCM) ili waweze kuendelea kuwaletea maendeleo wananchi kupitia miradi mbalimbali watakayoweza kuiimbua.
Post a Comment