Mgombea Ubunge wa Viti Maalumu wa Mkoa huo kupitia CCM, Halima Okash wakati wa kampeni za kuwanadi Mgombea Urais wa CCM, Dk. Magufuli, Mgombea Ubunge Jimbo la Mvumi, Livingstone Lusinde (Kibajaji) na Mgombea Udiwani wa Kata ya Manga.
Akina mama wakimsikiliza Okash akimwaga sera nzuri za CCM katika Kata ya Manga, Mvumi. |
Na Mwandishi Wetu, Mvumi.
WANAWAKE wa Mkoa wa Dodoma wameombwa kumpatia kura nyingi za kutosha Mtoto wa mwanamke mwenzao, Mgombea Urais wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli kwa heshima alioupa mkoa huo kuwa Jiji na makao makuu ya Nchi.
Ombi hilo limetolewa na Mgombea Ubunge wa Viti Maalumu wa Mkoa huo kupitia CCM, Halima Okash wakati wa kampeni za kuwanadi Mgombea Urais wa CCM, Dk. Magufuli, Mgombea Ubunge Jimbo la Mvumi, Livingstone Lusinde (Kibajaji) na Mgombea Udiwani wa Kata ya Manga.
"Mtoto wa mwanamke mwenzetu Dk. Magufuli ametufanyia mambo makubwa sisi wana Dodoma, kwa kuipa heshima Dodoma kuwa Jiji, makao makuu ya nchi ambao ndiyo Reception ya Nchi, kwa kumpigia kura nyingi za ushindi," alisema Okash katika kampeni hizo.
"Jamani Mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni, huo ndiyo ukweli kwa miaka mitano DK Magufuli amefanya makubwa kwa mkoa wetu wa Dodoma na nchi yetu kwa ujumla, hivyo anastahili kupewa kura hizo,"alisema Okash huku akipigiwa makofi ishara ya kwamba wanakubaliana naye.
Okash, alitaja baadhi ya mambo makubwa yaliyofanywa na yanayoendelea kutekelezwa Dodoma chini ya Uongozi wa Dk. Magufuli kuwa ni; Ujenzi wa barabara za kisasa ikiwemo ya Pete (Ring Road) ya njia nne itakayozunguka jiji la Dodoma.
Pia, ujenzi wa Reli ya Kisasa ya SGR, Hospitali za kisasa ikiwemo ya Benjamin Mkapa, Soko la kisasa la Ndugai, Stendi ya kisasa ya mabasi na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato unaoanza kujengwa hivi karibuni. Pia ameahidi kujenga uwanja mkubwa wa kisasa wa michezo.
Pia aliwasihi wasisahau kumpa kura nyingi mtoto wao anayegombea Jimbo hilo la Mvumi, Lusinde maarufu kama Kibajaji, Mbunge mpigania haki za wananchi, mmoja wa wabunge wazalendo, wachapakazi na machachari katika kutetea maslahi ya wananchi bungeni.
"Mtoto wenu Kibajaji ni mmoja kati ya wabunge wazalendo na machachari mno bungeni, hivyo msiipoteze hiyo dhahabu mpeni kura nyingi aendelee kuwaongoza kwa mustakabali wa maendeleo ya Mvumi na Kata ya Manda kwa ujumla," alisema Okash huku akishangiliwa na wanawake walioshiriki kampeni hizo katika Kata ya Manda.
Akiwa katika Kikao cha ndani cha Kata ya Ilangali, Mvumi, Okash akiwaombea kura wagombea wa ngazi ya urais na ubunge na udiwani, aliwasihi akina mama kutotishika wala kutotoa shahada zao kwa kuwapigia wapinzani, bali wahakikishe katika Uchaguzi Mkuu Oktoba 28, kura zote wanampigia Dk. Magufuli, Lusinde na Mgombea Udiwani wa Kata hiyo, Wandiyamba.
Post a Comment