Madiwani katika mji mkuu wa Ujerumani , Berlin wamepiga kura ya kuondoa jina la barabara moja linalompatia heshima gavana mmoja wa nyakati za ukoloni katika eneo la Afrika mashariki aliyeshutumiwa kwa kuagiza mauaji na kuweka jina la mmoja wa wanaharakati wa kupigania uhuru nchini Tanzania.
Barabara ya Wissmannstraße, iliopatiwa jina la Hermann von Wissmann, sasa itaitwa Lucy-Lameck-Straße.
Alikuwa waziri wa kwanza mwanamke nchini Tanzania pamoja na kuwa miongoni mwa viongozi maarufu katika vuguvugu lililopigania uhuru wa taifa hilo.
Lameck alikuwa naibu waziri wa maendeleo ya kijamii na Afya na alifanya kazi kuimarisha nafasi ya mwanamke.
Von Wissman alikuwa gavana wa taifa la Ujerumani Afrika mashariki ambayo kwasasa ndio mataifa ya Tanzania , Burundi na Rwanda katika mwisho wa karne ya 19 na anadaiwa kuwa chanzo cha mauaji ya wakaazi wengi limetangaza gazeti la Ujerumani, Der Tagesspiegel .
Kundi la Berlin Postkolonial, mojawapo ya kundi lililohusika na mabadiliko liliunga mkono hatua ya serikali hiyo ya mtaa.
Katika taarifa lilisema kwamba kampeni hiyo ilizuia kuheshimiwa kwa ''Von Wissmann na mahala pake kuchukuliwa na mwanamke Mtanzania ambaye alipinga ukoloni na ubaguzi wa rangi''.
"Wissmann alikuwa mbaguzi na muhalifu wa kivita . Lucy Lameck anawakilisha mchango ulioshushwa thamani wa wanawake wa Tanzania waliopigania uhuru wa taifa hilo'', alinukuliwa akisema mwanaharakati wa Tanzania Mnyaka Sururu Mboro.
Je Lucy Lameck ni nani?
Alizaliwa mnamo 1934 Moshi mjini iliyokuwa wakati ule sehemu ya Tanganyika ya Kiingereza.
Alizaliwa katika familia ya wakulima, akajifunza kazi ya uuguzi kabla ya kuingia katika shughuli za siasa.
Baada ya mafunzo ya kazi ya muuguzi mnamo 1950, hakutaka kushiriki katika mfumo wa matibabu wa kikoloni wa Uingereza, na kwa hiyo alianza kufanya kazi ya karani.
Lucy Lameck alikuwa mwanasiasa wa Kitanzania, na mwanamke Mtanzania wa kwanza kuwahi kushika wadhifa wa uwaziri kwenye serikali ya kitaifa.
Alisoma baadaye kwenye Chuo cha Ruskin, huko Oxford, Uingereza.
Mwaka 1960 aliingia mara ya kwanza katika Bunge la Tanganyika kabla ya kuchaguliwa katika Bunge la Kitaifa la Tanzania mnamo 1965.
Anakumbukwa kama kielelezo cha kuigwa, akiwa amefanya kazi katika maisha yake yote kuboresha hali ya wanawake nchini Tanzania.
Post a Comment