Mwenyekiti wa madereva na wamiliki wa Bajaji na bodaboda Manispaa ya Singida Ahmed Juma akitoa ufafanuzi wa tamko la kulaani vijana wanaotaka kufanya vurugu.
Dereva wa Bodaboda Manispaa ya Singida Ramadhani Zuberi akitoka ufafanuzi kwa waandishi ambao hawapo pichani kupinga na kulaani maandamano ya vijana ambao wanataka kutumika kuvuruga amani
Sehemu ya madereva wa bodaboda Manispaa ya Singida
John Mapepele na Rose Nyangasa, Singida
Wamiliki na Madereva wote wa Bajaji Mkoa wa Singida wametoa tamko rasmi la kulaani baadhi ya vijana ambao wameanza kutumiwa na baadhi ya vyama vya upinzani kuandamana kupinga matokeo ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 28, Mwaka huu.
Akitoa tamko kwa niaba ya wanachama 2000 wa Mkoa wa Singida kwenye Kituo cha Bajaji Soko Kuu la Mjini Singida, Mwenyekiti wa Madereva na Wamiliki wa Bajaji na Boda boda Manispaa ya Singida, Ahmed Juma amesema umoja wao umepinga njama zinazofanywa na baadhi ya vyama ya kuwatumia madereva hao na kusisitiza kuwa njama hizo hazitafanikiwa katika Mkoa wa Singida .
“Tumejipanga kukabiliana na uhuni wowote ambao umepangwa kufanywa kwenye kipindi hiki na baadhi ya wahuni wachache wasioitakia mema nchi yetu, tunaomba vyombo vya ulinzi visimamie hili kikamilifu na sisi tupo nyuma yao” aliongeza Juma
Amesema kinachotaka kufanyika sasa baada ya uchaguzi kukamilika na matokeo kutangazwa kwa kufuata taratibu zote za uchaguzi na Mamlaka halali ni vurugu na uvunjifu wa amani jambo ambalo amesema halikubaliki badala yake amewasihi wananchi wafanye kazi ili kuiletea nchi yetu maendeleo zaidi katika awamu ya sasa.
Amemwomba Rais, John Pombe Joseph Magufuli kuendelea kuiletea maendeleo Tanzania ili itoke kwenye Uchumi wa Kati hadi Uchumi wa juu kabisa na hatimaye kuboresha maisha ya watanzania wote.
Mwenyekiti wa Madereva wa Boda boda wa eneo la Soko Kuu Mjini Singida, Kulwa Moshi ameonya madereva wa Bodaboda ambao kwa namna moja au nyingine watatumika katika kuvunja Sheria za nchi kwa kupanga njama za kufanya maandamano yasiyo ya amani.
Moshi ameongeza kuwa wananchi wameamua kuwachagua viongozi wanao wapenda hivyo hakuna sababu ya watu kuandaa njama za kupinga matokeo ya uchaguzi.
Naye Ramadhani Zuberi, Dereva wa Bajaji kwenye Kituo Kikuu cha Mabasi ya Mkoa wa Singida amepongeza Serikali kwa kufanikisha Uchaguzi Mkuu wa Mwaka huu kwa uwazi ambao umeweza kufuata taratibu zote na kutoa matokoa kwa wakati
Kwa mujibu wa Tume ya Uchaguzi Nchini (NEC), Rais mteule wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa John Pombe Joseph Magufuli anatarajiwa kuapishwa Novemba 5 Mwaka huu kwenye uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma.
Post a Comment