Featured

    Featured Posts

MBUNGE JANETTH MAHAWANGA AMUOMBA MKUU WA MKOA WA DAR KUVISAIDIA VIKUNDI VYA VYA UJASIRIAMALI VYA KINAMAMA KUPATA USAJILI

Mwenyekiti wa chama cha Women of Hope Alive (WHA), kinachojiahughulisha na masuala ya ujasiriamali ikiwa ni pamoja na kutoa mafunzo ya Uchumi na Ujasiriamali kwa vikundi vya kinamama, Mbunge wa Viti Maalum kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Janeth Mahawanga (katikati) akizungumza wakati wa Kongamano la Wanawake wajasiriamali la Wanawake na Vikoba, lilofanyika katika Ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam, jana.

Na Bashir Nkoromo, CCM Blog

Mwenyekiti wa chama cha Women of Hope Alive (WHA), kinachojiahughulisha na masuala ya ujasiriamali ikiwa ni pamoja na kutoa mafunzo ya Uchumi na Ujasiriamali kwa vikundi vya kinamama, Mbunge wa Viti Maalum kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Janeth Mahawanga, amemuomba Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Abubakar Kunenge kusaidia Wanawake kupata usajili wa vikundi vyao kwa kuwa wengi bado hawajui pa kuanzia ili kusajili vikundi hivyo kutokana na baadhi ya watendaji wa Manispaa kuwapiga kalenda kila wakienda kuomba usajili huo, huku wakipewa taarifa zisizo rasmi katika mitandao ya kijamii.


"Maana wakienda Manispaa wanaambiwa bado na wakati huo huo wanakuwa wanapata taarifa zisizo rasmi kupitia mitandaoni, sasa imefikia wengine wamevunjika moyo na wamevunja vikundi kutokana na majibu ya watendaji wa Manispaa na kwa uwoga kutokana na kupata taarifa ambazo si rasmi kuhusu usajili wanazozipata mitandaoni", amesema Janeth ambaye pia ni Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Kata ya Makongo jijini Dar es Salaam.


Janeth alitoa ombi hilo, katika Kongamano wa Vikundi vya Ujasiriamali vya Wanawake la Wanawake na Vikoba, kutoka dar es Salaam, Morogoro na Pwani, lililofanyika jana katika Ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam, Mgeni rasmi akiwa Mkuu wa Wilaya ya Temeke Godwin Gondwe kwa niaba ya Mkuu huyo wa mkoa wa Dar es Salaam.


Amesema kutokana na kukosa usajili vikundi hivyo vimeshindwa kukopesheka benki na vile vilivyosajiliwa vimekuwa vikifanya Ujasiriamali mdogo kwa kuwa havina sifa za kukopesheka kwani bado havina biashara ambayo ndio ingesimama kama dhamana ya mikopo yao na kwamba vile vyenye usajili navyo vimekuwa vikitamani kufanya ujasiariamali mkubwa lakini inashindikana kwa kuwa havina mitaji ya kutosha. 


"Vikundi vingi vimekuwa vikinufaika na mikopo ya Manispaa ambayo hutoka kwenye Kata kupitia Ofisi za Bibi Maendeleo wa Kata ambayo huanza na kiasi cha Sh. 300,000/=  na kikundi kinapomaliza kurejesha huongezwa hadi kinafikia Sh. 1,500,000/=, kwa hiyo unapozungumzia Wanawake kuingia kwenye uwekezaji mkubwa wa kilimo, viwanda vidogo na kufanya ujasiriamali mkubwa ambao pia utatoa ajira baina ya watu unajikuta  unahitaji mikopo mikubwa kidogo", alisema  Janeth..


Akizungumzia hatua ambazo WHA imekwishafanya kukabiliana na changamoto hizo, Janeth alisema aliwatoa hofu Wanawake na kuwaomba wasivunje vikundi vyao vya vikoba na vya ujasiriamali na kuwataka wapuuze taarifa za kwenye mitandao ya kijamii kisha akafanikiwa kumwalika Afisa kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ambaye alizungumza na wanawake kuhusu sheria mpya za vikundi na kuwatoa hofu iliyokuwa imetanda kwao na kwenye jamii kwa jumla. 


Janeth alisema, baadaye alimwalika Mwalimu wa vikundi na masuala ya usajili Evans Chipindi ambaye aliwasaidia Wanawake kupata picha halisi kuwa Serikali haina nia mbaya na usajili bali kwa faida yao ni kuondokana na ile tabia ya kudhulumiwa pesa zao na wajanja ambao wanachukulia mwanya wa kutokuwa na usajili na kutofahamu vema sheria zinazowalinda.


Alisema, kufuatia kongamano la Mwanamke na Uwekezaji lililofanyika mwaka jana Wanawake wengi walihamasika na kuingia kwenye ujasiriamali ndani ya vikundi na kuacha na dhana ya kufanya ujasiriamali wa mmoja mmoja na matokeo yanekuwa chanya sana, na kwamba  ndiyo sababu Kongamano kama holo la mwaka huu  mwitikio umekuwa mkubwa sana kiasi kwamba zaidi ya wanawake 900 wameweza kushiriki kongamano hilo na kuufanya ukumbi wa Diamond Jubilee lilokofanyika ukafurika. 


"Kongamano hili la Mwanamke na Uwekezaji ni 'platform' ya kuwakutanisha Wanawake na wadau wa maendeleo yao katika nyanja zote kwani WHA inawakutanisha na Taasisi za kifedha ambazo zina bidhaa maalum kwa ajili ya wanawake wajasiriamali, wataalam wa masuala ya fursa na uwekezaji, wataalam wa masuala ya kisaikolojia, wanasheria waonatambua na kutoa misaada ya haki za wanawake, vikundi vilivyofanikiwa ili kubadilishana uzoefu na vikundi vichanga kwani kuna changamoto nyingi sana kwenye vikundi vya Wanawake ili visimame hivyo hakuna sababu ya kuwaacha wengine wapitie changamoto hizo kama kuna waliopitia na wakafanikiwa ni vizuri kuwaeleza nini cha kufanya na nini cha kuepuka", Alisema Janeth.


Janeth pia amesema kufuatia hotuba ya  Rais Dk. John Magufuli aliyoitoa wakati akihutubia Bunge la 12, akisisitza kuwa pamoja na kutoa mikopo Serikali itaendelea kutekeleza program mbalimbali za kukuza ujuzi na maarifa ikiwemo maarifa ya ujasiriamali ili kiwapa ujuzi na uzoefu wananchi utakaowawezesha kujiajiri au kuajirika ndani na nje ya nchi, hivyo WHA katika kumuunga mkono Rais ili masuala hayo ya Wanawake wafanikiwe ni lazima kuwakutanisha pamoja ili kuwapa elimu, kuwakutanisha na wadau wa maendeleo na kuwatia moyo kuwa yote yanawezekana kinachotakiwa ni utayari wao kwani tayari serikali mipango mizuri juu yao.


Akizungumza na niaba ya Mkuu wa mkoa wa Dares Salaam, Mkuu wa Wilaya ya Temeke Godwin Gondwe alisema Mkuu huyo wa mkoa anawapongeza WHA walioandaa kongamano hilo, akisema wamefanya jambo la muhimu sana kwa kuwa licha ya kulifanya kwa ajili ya manufaa yao lakini pia wameisaidia Serikali kwa kuwa ndiyo aliyopaswa kulifanya kujumu hilo.


Aliwataka wanawake kuongeza bidii katika kujitafutia vipato kwa njia hiyo ya Ujasiriamali huku akizitaka taasisi zinazohusika na masuala ya kisheria kama Umoja wa Wanasheria wanawake Tanzania (TAWLA) kuwa mstari wa mbele katika kujitolea kuwapatia elimu ya mambo ya kisheria katika masuala ya fedha na biashara.


Gondwe alisema, Mkuu huyo wa mkoa ameahidi kuwapa ushirikianao WHA ili kuhakikisha changamoto alizozisema Mbunge mahawanga anazifanyia kazi ili kuwezesha sekta ya Ujasiriamali hasa kwa vikundi vya Wanawake inapata mafanikio yanayotarajiwa.


author

Author Name

Author Description!

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

www.CodeNirvana.in

Magazeti Ya Leo

Copyright © Magazeti ya Leo, Habari Leo Tanzania, Mwananchi, Michuzi, mwanaspoti, nipashe, Udaku | Designed By Code Nirvana