Mchungaji wa huduma ya Jesus King of Kings Ministries, Alex King wa Maryland nchini Marekani akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) kuelezea hisia zake katika mkutano uliofanyika jijini Dar es Salaam.
…………………………………………………………………………………………………….
Na Mwandishi wetu
MCHUNGAJI wa Kitanzania anayehudumu Jesus king of kings ministries, Maryland Marekani, Alex King amesema Tanzania imepiga hatua kubwa katika kipindi kifupi, mafanikio ambayo yanatakiwa watanzania wote kujivunia.
Aidha amesema kwamba mwaka huu alirejea nyumbani kuja kuona sifa ambazo Rais John Magufuli amekuwa akipewa jinsi alivyoliendesha taifa katika kipindi cha miaka mitano, na kusema kiongozi huyo ni zawadi ya Mungu.
“Alisema Marekani ilichukua miaka 200 kutengeneza uchumi imara kwa kuwanyonya waafrika lakini Rais Magufuli kwa miaka mitano amefungua Tanzania na kuifanya kuwa moja ya taifa linalokua kasi kiuchumi na kiimani kwa Mungu.
“Nimefurahi ujenzi mkubwa unaoendelea hapa na kwamba makandarasi wote wanalipwa, hii ni neema Marekani ilijengwa na watumwa na sasa wanatafuta fidia” alisema King.
Alisema ameamua anaporejea Marekani kuwa balozi wa hiari wa kutangaza Tanzania ili kila mtu atambue nini kinafanyika katika taifa hili lililochaguliwa na Mungu.
“Hakuna watu wa kuisemea nchi yangu vizuri huko nje, nitaisemea” alisema King.
Mtanzania huyo mwenye asili ya Singida ambaye kwa sasa ana uraia wa Marekani kupitia mfumo wa Greencard, akizungumza na waandishi wa habari jana kabla ya kurejea nchini Maryland, alisema ujenzi wa miundombinu ya barabara na hospitali yameonesha ni kwa namna gani Tanzania inasonga mbele katika kuhakikisha kwamba wananchi wake wanaishi katika neema.
“Nimefika nyumbani Singida kuna hospitali kubwa ya rufaa pale, yaani sasa wananchi hawawezi kufa kwa kukosa huduma ya rufaa” alisema King.
Akizungumzia ugonjwa wa Covid-19 alisema kwamba Mungu ameisaidia Tanzania kukabiliana na mazingira ya ugonjwa huo kutokana na kiongozi wa nchi kuwa na imani kubwa na Mungu.
“unaweza kuona yote hayo yalianza kwa Rais Magufuli kuitisha maombi ya kufunga kwa siku 3 kwa watanzania wote. Haikuwa kwa waislamu na wakristo pekee aliwaagiza hata wapagani na kuagiza waite Mungu, na tunaona nini Mungu amekitenda” alisema King na kuongeza kuwa ni kama vile Nabii Elia alivyofanya nchini Israel.
Mtumishi huyo wa Mungu amesema kwamba Tanzania inalindwa na Mungu na katika yeye ametoa taifa lenye shuhuda nyingi na mafanikio makubwa katika elimu, afya na ustawi wa jamii.
“Nimefurahi sana na uwapo wa elimu bure manake hata watu maskini wanaweza kufika Chuo kikuu ambako pia wanakopeshwa kuendesha elimu hiyo. Nimefika nyumbani na kumkuta mpwa wangu akiwa anatunukiwa digrii yake ya kwanza. Aksante sana Magufuli kuwezesha hili'” alisema King
Pamoja na kuwataka watanzania waendele kutunza jamii yao kumuogopa Mungu aliwataka kuendelea kuchapakazi kwa bidiii kwa manufaa ya taifa na kuwasihi watanzania waliopo nje kurejesha mitaji nyumbani.
“Nimeona mambo yanayofanyika hapa nyumbani ni makubwa watanzania tuishio nje tupiganie nchi yetu turejeshe mitaji” alisema na kuongeza kwamba wakati umefika wa Rais John Magufuli kufikiria uraia pacha ili watanzania waliopo nje wawe na uhakika na uwekezaji nyumbani.
Post a Comment