CCM Blog, Dar es Salaam
Subhash Patel ambaye alikuwa mfanyabiashara maafuru hapa nchini aliyefariki jana, anatarajiwa kuzikwa kesho, siku ya Alhamisi, Desemba 17, 2020 kwenye Makaburi ya Wahindu yaliyoko Kijitonyama, Dar es Salaam, wanafamilia wamesema.
Tofauti na taarifa za awali kwamba Bilionea Patel alikuwa amefika katika Hospitali ya Agakhan jijini Dar es Salaam, wanafamilia wamesema alifia nyumbani kwake, Kisutu jijini Dar es Salaam ambako alikuwa akiendelea na matibabu.
Mfanyabiashara huyo maarufu nchini alikuwa Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni za Motisun Group, zinazozalisha Bidhaa za plastiki, saruji, mabati, nondo, nyaya za umeme, vinywaji baridi ikiwemo aina ya Sayona, rangi na pia alimiliki hoteli za White Sands, Sea Cliff na Pearlsun Hotel & Resorts.
Subhash ambaye kifo chake kimeonyesha kustusha watu mbalimbali akiwemo Waziri Mkuu Majaliwa Kassim Majaliwa, alikuwa pia Mwenyekiti wa Shirikisho la Wenye Viwanda Nchini (CTI) na Mjumbe wa Bodi ya Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF).
“Hayati Shubash, ana mchango wake kwenye sekta ya viwanda, alikuwa rafiki wa wote, mcheshi, ametoa msaada kwa maskini na matajiri na hakuwa mbaguzi,” amesema Waziri Mkuu Majaliwa Kassim Majaliwa katika Salam hizo za Rambirambi.
“Ninatoa pole kwa wanafamilia, ndugu na wote walioguswa na msiba huu. Taifa limempoteza mmoja wa wazalendo wake. Mwenyezi Mungu aiweke roho yake mahali pema peponi, Amina.” alisema Waziri Mkuu Majaliwa Kassim Majaliwa katika salam za rambirambi alizotoa jana.
Post a Comment