Aliyekuwa mtumishi wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) Abdulhakim Kabuga amehukumiwa kwenda jela miaka mitatu au kulipa faini ya sh. 500,000, baada ya kupatikana na hatia ya kupokea hongo ya sh.30,000 ili amsaidie mtoa taarifa kupata Kitambulisho cha Taifa haraka.
Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoani Dodoma Sostenes Kibwengo, amesema Kabuga alifikishwa mahakamani na TAKUKURU kwa kosa la kupokea hongo ya sh. 30,000 ili amsaidie mtoa taarifa kupata kitambulisho cha Taifa haraka.
Aidha Mahakama ya Wilaya ya Kondoa imemuhukumu Mtendaji wa Kata ya Thawi Hashim Ally Mohamed kulipa faini ya sh. 300,000 au kifungo cha miaka miwili baada ya kuridhishwa na ushahidi kwamba alishawishi rushwa ya sh. 175,000 na kupokea Sh. 80,000 ili asimchukulie hatua mzazi ambaye hakumpeleka binti yake sekondari baada ya kufaulu.
Katika hatua nyingine Kibwengo amesema, TAKUKURU imeokoa sh. 45.760 milioni alizolipwa Mkandarasi wa Kmpuni ya Leostart Engineering ya jijini Dar es Salaam alizolipwa mkandarasi kinyume na utaratibu wa utekelezaji wa mradi wa maji wa kijiji cha Mlongila wilayani Chemba fedha hizo ni sehemu tu ya fedha alizolipwa mkandarasi huyo.
“Mtakumbuka siku za nyuma tuliwahi kuwataarifu kuhusu ufuatiliaji wetu wa mradi huo na ukaguzi maalum uliofanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ulionyesha kuwa Mkandarasi wa mradi huo wenye thamani ya shilingi milioni 579.323 ulioanza mwaka 2013 na kukamilika mwaka 2014 alilipwa fedha zaidi ya kazi zilizofanyika na hivyo kutakiwa kuzirejesha.” amesema Kibwengo.
Post a Comment