WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameiagiza Wizara ya Kilimo ikiimarishe kituo cha utafiti wa zao la michikichi cha Kihinga kilichopo mkoani Kigoma kwa kukitengea bajeti kwa ajili ya ujenzi wa majengo ya kudumu pamoja na baabara ili kuboresha shughuli za utafiti zinazofanywa kituoni hapo.
Ameitaka wizara hiyo ihakikishe suala la utoaji wa elimu kwa wakulima kuhusu zao la michikichi linaimarishwa na kupewa kipaumbele, pia iendelee kushirikiana na wadau wa sekta binafsi katika kuhakikisha utafiti wa mbegu unaofanywa una tija.
Waziri Mkuu ametoa maagizo hayo leo (Jumamosi, Desemba 19, 2020) wakati akizungumza na wadau wa zao la michikichi katika ukumbi wa NSSF, Kigoma. Ametumia fursa hiyo kuwasisitiza watumishi wa umma kuwekeza katika zao hilo ili kujiongezea kipato.
“Wizara ya Kilimo hakikisheni mnatumia vyombo vya habari zikiwemo redio za kijamii kwa ajili ya kutoa elimu ya umuhimu wa zao la michikichi. Pia tumieni magari maalumu kwa ajili ya kutolea elimu kwa umma kuhusu zao la michikichi na faida zake.”
Waziri Mkuu amesema hadi sasa mbegu zilizozalishwa tangu kuanza kwa zoezi hilo ni 4,205,335 ambazo zinatosha kupanda eneo la ekari 84,106.7 ambapo kati yake asilimia 71 imechangiwa na Wizara ya Kilimo kupitia TARI na asilimia 29 ni mchango wa sekta binafsi (FELISA & Ndugu Development Foundation (NDF) na Yangumacho Group).
Amesema mpaka sasa mbegu 2,184,111 zimeshasambazwa na TARI kwa ajili ya kuziotesha ili miche bora iweze kusambazwa kwa wakulima na kati ya mbegu zinazooteshwa tayari miche 1,370,318 imeshaota na kupandwa kwenye viriba vidogo na vikubwa ikiwa ni hatua ya kuzifikisha kwa wakulima.
Waziri Mkuu amesema idadi hiyo ya miche inatosha kupandwa kwenye eneo la ekari 27,406.36 na kwamba shughuli ya ukuzaji wa miche kwenye viriba inaendelea. “Mpaka sasa, ekari 270 zimekwishapandwa ambapo katika Gereza Kwitanga ekari 50, Gereza Ilagala ekari 80 na JKT Bulombora ekari 140.”
Kadhalika, Waziri Mkuu amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Thobias Andengenye kwa kushirikiana na wakuu wa wilaya wahakikishe zao hilo linaendelea kulimwa na wawe na kanzidata itakayowasaidia kujua idadi ya wakulima ili kurahisisha zoezi la ufuatiliaji.
Pia, Waziri Mkuu amewahamasisha wananchi waweke utaratibu wa kuwazoesha watoto wao kulima zao hilo, ambapo amesema iwapo wazazi watawaandalia watoto wao mashamba ya zao hilo yatawawezesha kuweza kupata fedha za kulipia gharama za masomo katika siku za usoni.
Mahitaji ya mafuta nchini kwa sasa ni zaidi ya tani 570,000 huku uzalishaji ukikadiriwa kuwa tani 210,000 tu. Hivyo, kiasi cha tani 360,000 huagizwa kutoka nje ya nchi na kugharimu kiasi cha shilingi bilioni 443 kila mwaka.Tuna ardhi nzuri, wakulima wenye nia na hali ya hewa nzuri na uongozi wenye dhamira.
Serikali imeona hakuna sababu ya kupoteza fedha hizo badala ya kuzibakisha ndani tumeona tuokoe fesdha hizo kwa kuwekeza kwenye kilimo cha michikichi, hatua hiyo pia itawezesha wakulima kuongeza uzalishaji na hivyo kujiongezea kipato kwani watapata soko la mafuta hayo hapa hapa nchini.
Baada ya kikao hicho Waziri Mkuu ameshiriki zoezi la kugawa miche kwa wawakilishi wa vyama ushirika kwa msingi( AMCOS) na kupanda miche katika shamba la mkulima Onyango katika kata ya Mahembe
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Andengenye amesema mkoa umeanza jitihada za kutafuta afisa atakayekuwa na dhamana ya kusimamia zao hilo tu ikiwa ni pamoja na kuwa na kanzi data itakayomuwezesha kujua idadi ya wakulima za zao hilo.
Amesema watahakikisha katika taasisi zote za Serikali zikiwemo shule na vyuo watoto wanafundishwa kuhusu kilimo cha zao hilo kuanzia hatua za awali za uandaaji wa mashamba hadi uvunaji ili wawe na uelewa mzuri na hatimaye waje kuwa wakulima wazuri wa zao hilo.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
Post a Comment