Featured

    Featured Posts

34 WAKAMATWA KWA KUTOTUMIA MASHINE ZA EFDS

 


 Kaimu meneja wa mamlaka ya mapato(TRA)wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma Lewis Charles akitoa taarifa ya hali ya ukusanyaji mapato kwa kipindi cha miezi sita kuanzia mwezi Julai hadi Desemba 2020 katika kikao cha  kamati ya ushauri ya wilaya hiyo kilichofanyika jana katika ukumbi wa kanisa katoriki jimbo la Mbinga ambapo mamlaka hiyo ilifanikiwa kukusanya zaidi ya bilioni 2 kati ya lengo la kukusanya bilioni 1.9.

*************************************************

Na Muhidin Amri,
Mbinga

MAMLAKA ya mapato(TRA)wilaya ya Mbinga  mkoani Ruvuma, imefanikiwa kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 2,108,203,163.70 sawa na asilimia 117 kati ya lengo la kukusanya shilingi bilioni  1,798,607,033.71 katika kipindi cha miezi sita kutoka mwezi Julai hadi Desemba 2020.

Hayo yamesemwa na Kaimu Meneja wa Mamlaka hiyo wilayani humo Lewis Charles, wakati akitoa taarifa ya ukusanyaji wa mapato katika kipindi cha nusu Mwaka wa fedha 2020/2021 katika kikao cha kamati ya ushauri ya wilaya ya Mbinga(DCC)kilichofanyika katika Ukumbi wa kanisa Katoriki Jimbo la Mbinga.

Aidha alisema, katika mwaka wa fedha 2020/2021 Tra wilaya ya Mbinga imepewa lengo la kukusanya shilingi bilioni 3.604 na malengo hayo yatafikiwa iwapo wananchi,wafanya biashara na wadau wengine watatoa ushirikiano kwa mamlaka hiyo.

Kwa mujibu wa Lewis, katika kipindi hicho  Tra imewakamata watu 34 wakiwemo wafanyabiashara,wanunuzi wa bidhaa  na watoa huduma mbalimbali  kwa kosa la kutozingatia matumizi sahihi ya mashine za Kielektroniki(Efds) ambao  wametozwa shilingi milioni 58,500,000 kama adhabu, kati ya hizo  shilingi milioni 22,580,000 zimelipwa na milioni 35,920,000  zinategemewa kulipwa.

Alisema, mamlaka ya mapato inaendelea kuwakumbusha wafanya biashara na wananchi wote kwa jumla  kuwa msingi wa makadirio ya kodi kwa haki ni utunzaji sahihi wa kumbukumbu na ni wajibu na  kila mwenye sifa kulipa kodi stahiki za serikali.

Lewis ameonya kuwa, mfanyabiashara yeyote atakayebainika kutotumia vyema mashine za kielektroniki  katika biashara yake au kukaidi kutimiza wajibu huo wa kisheria atakuwa ametenda kosa na atachukuliwa hatua kali za kisheria.

Alisema, mfanyabiashara atakayekamatwa kwa kosa la  kutotumia mashine za Efds adhabu yake ni faini  kuanzia milioni 3 na isiyozidi milioni 4.5  au kifungo cha miaka mitatu jela au vyote kwa pamoja kwa mujibu wa sheria za usimamizi wa kodi ya mwaka 2015.

Pia, amewataka wanunuzi wote wa bidhaa mbalimbali kuhakikisha wanadai risiti pindi wafanyapo manunuzi  kwani ni haki ya msingi na kisheria kwa kila mnunuzi, na kutofanya hivyo ni kosa linaloweza kupelekea kupata adhabu kali ikiwemo kutozwa faini kati ya shilingi 30,000 hadi  milioni 1.5.

Alisema, Tra inategemea sana ushirikiano kutoka kwa wadau wote  katika suala zima la kukusanya mapato ya Serikali na kusisitiza,ni wajibu wa kila mwananchi kuonyesha uzalendo kwa kulipa kodi ili kuisaidia Serikali kutoa huduma bora na haraka zaidi.

Lewis amesisitiza kuwa,  ni haki na lazima kwa mwananchi kudai risiti sahihi kila anunuapo bidhaa au huduma pamoja na kutoa taarifa ya upotevu wa mapato ili kuiwezesha mamlaka hiyo kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi katika kuwahudumia Watanzania.

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Mbinga Kosmas Nshenye aliwataka wafanyabiashara na watoa huduma mbalimbali katika wilaya hiyo kuhakikisha wanalipa kodi stahiki za serikali  kwani suala la kodi ni lazima na kutoa ushirikiano kwa mamlaka ya mapato.

Alisema, nchi zote zilizoendelea zimepiga hatua ya kiuchumi kutokana na mwamko mkubwa wa watu wake kulipa kodi na kuwaagiza watendaji wa mamlaka hiyo kuhakikisha wanafanya kazi usiku na mchana ili kufikiwa malengo waliyopewa na Serikali ya kukusanya zaidi ya shilingi bilioni 3 katika mwaka wa fedha 2020/2021.

author

Author Name

Author Description!

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

www.CodeNirvana.in

Magazeti Ya Leo

Copyright © Magazeti ya Leo, Habari Leo Tanzania, Mwananchi, Michuzi, mwanaspoti, nipashe, Udaku | Designed By Code Nirvana