Philipe Nyusi
Rais wa Msumbiji Felipe Jacinto Nyusi anatarajiwa kuanza leo ziara ya kikazi ya siku mbili hapa nchini Tanzania na atapokewa na Mwenyeji wake, Rais Dk. John Magufuli, katika Uwanja was Ndege wa Chato mkoani Geita.
Taarifa iliyotolewa na Idara ya Habari (Maelezo), imesema, ziara hiyo ilipangwa kufanyika mwaka jana lakini haikufanyika kwa sababu mbalibali ikiwemo Uchaguzi Mkuu mwaka wa 2020.
Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhandisi Robert Gabriel amesema Rais Nyusi atawasili saa 4 asubuhi, na kuwataka wananchi kujitokeza kwa wingi katika Uwanja wa Ndege kwa ajili ya kumpokea
Kwa mujibu was taarifa, ziara hii itahusu masuala ya Mahusiano ya Kidiplomasia, Kisiasa na Kiuchumi, kama ambavyo yaliasisiwa na viongozi waanzilishi wa nchi za Tanzania na Msumbiji, Mwalimu Julius Nyerere na Samora Machel chini ya TANU na baadaye CCM na Frelimo cha Msumbiji iliyopta Uhuru wake mwaka 1975.
Viongozi wote walioongoza nchi hizi mbili katika vipindi tofauti wameendelea kuhamasisha uhusiano huu wa undugu wa damu, ndio maana hata wakati wa mazishi ya Rais wa Awamu ya Tatu, Hayati Benjamin William Mkapa, Balozi wa Msumbiji hapa Tanzania aliwasilisha salamu maalum kutoka kwa Rais Nyusi.
Mahusiano haya ya kindugu na kidiplomasia yameendelea kuimarika na uchumi umeendelea kuimarika kutoka na biashara inayofanyika katika nchi hizi.
Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mauzo ya bidhaa za nje kati ya nchi hizi mbili yaliongezeka kutoka shilingi bilioni 76.4 mwaka 2018 na hadi kufikia shilingi bilioni 93.5 mwaka 2019.
Kampuni kubwa za Kitanzania zilizowekeza Msumbiji ni pamoja na Bakhresa, Magodoro Dodoma na kampuni za usafirishaji wa abiria na mizigo.
Post a Comment