Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Mwanaidi Ali Khamis (Mb), akiweka jiwe la Msingi la ujenzi wa miundombinu ya Chuo Cha Mipango ya Maendeleo Vijijini Kituo cha Mafunzo cha Kanda ya Ziwa – Mwanza, kilichopo katika Kijiji cha Kitumba Wilayani Magu, Mkoani Mwanza, kulia ni Mkuu wa Chuo cha Mipango, Prof. Hozen Mayaya.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Mwanaidi Ali Khamis (Mb) (kulia), akisikiliza maelezo ya Bw. Joshua Mirumbe, kutoka Wilayani Bunda Mkoani Mara ambaye ni miongoni mwa wanufaika wa mradi wa ufugaji ng’ombe unaosimamiwa na Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini, wakati wa maonesho ya miradi hiyo kabla ya kuweka jiwe la Msingi la ujenzi wa miundombinu ya Kituo cha Mafunzo cha Chuo hicho Kanda ya Ziwa, kilichopo katika Kijiji cha Kitumba Wilayani Magu, Mwanza.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Mwanaidi Ali Khamis (Mb) (katikati) na Mkuu wa Wilaya ya Magu, Bw. Salumu Kali, wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya viongozi wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini (IRDP) baada ya hafla ya uwekaji jiwe la Msingi la ujenzi wa miundombinu ya Chuo Kituo cha Mafunzo cha Kanda ya Ziwa Mwanza.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Mwanaidi Ali Khamis (Mb) (kulia), akitoa maelekezo kwa wanufaika wa miradi mbalimbali inayosimamiwa na Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini (IRDP) kuhakikisha wanatumia miradi hiyo kujikwamua kiuchumi na kukuza pato la taifa, wakati wa maonesho ya miradi Wilayani Magu, Mkoani Mwanza. Kushoto ni Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo hicho, Prof. Martha Qorro.
Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini (IRDP), Prof. Martha Qorro, akimshukuru Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Mwanaidi Ali Khamis (Mb) (hayupo pichani) kwa kuweka jiwe la Msingi la miundombinu ya Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini (IRDP) Kituo Cha Mafunzo Kanda ya Ziwa – Mwanza kilichopo katika Kijiji cha Kitumba Wilayani Magu, Mkoani Mwanza.
Muonekano wa jengo la Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini (IRDP) Kituo Cha Mafunzo Kanda ya Ziwa kilichopo katika Kijiji cha Kitumba Wilayani Magu, Mkoani Mwanza ambalo ujenzi wake umefikia asilimia 80.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Mwanaidi Ali Khamis (Mb) (kulia) akisikiliza maelezo ya Bw. Hamadi Nyumanda, kuhusu virutubisho vya mifugo vikiwemo vinavyosaidia ng’ombe kuongeza maziwa, wakati wa maonesho ya miradi mbalimbali inayofadhiliwa na Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini (IRDP) Kituo Cha Mafunzo Kanda ya Ziwa – Mwanza.
(Picha na Farida Ramadhani, WFM, Mwanza)
********************************************
Na Farida Ramadhani na Peter Haule, Mwanza
NAIBU Waziri wa Fedha na Mipango Mheshimiwa Mwanaidi Ali Khamis, amevishauri vyuo vya elimu ya juu nchini kuhakikisha vinasimamia malezi na maadili ya wanafunzi wao kutokana na wengi wao kujiunga na masomo wakiwa na umri mdogo.
Mheshimiwa Mwanaidi ametoa rai hiyo wakati wa hafla ya kuweka jiwe la msingi la miundombinu ya Chuo Cha Mipango ya Maendeleo Vijijini Kituo cha Mafunzo Kanda ya Ziwa – Mwanza kinachojengwa katika kijiji cha Kitumba wilayani Magu mkoani Mwanza kwa gharama ya zaidi ya shilingi bilioni 2.
Alisema hatua ya Serikali ya kuondoa ada na michango katika elimu ya msingi na sekondari, idadi ya wanafunzi wanaojiunga na masomo ya elimu ya juu imeongezeka baadhi yao wakiwa na umri mdogo huku kukiwa na changamoto ya maendeleo ya kiteknolojia (utandawazi), yanayoathiri tabia na mienendo yao.
Aidha, Mhe. Mwanaidi amekitaka Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini, kuhakikisha kuwa kinafanya tafiti mbalimbali zitakazoibua suluhisho na changamoto zinazokwaza maendeleo ya wananchi hususani wa vijijini na kuziandika tafiti hizo kwa lugha rahisi ya Kiswahili ili tafiti hizo ziweze kuwanufaisha wananchi na kuchangia kujikwamua kiuchumi.
Vilevile amekishauri Chuo hicho kuboresha mitaala itakayovutia wanafunzi wengi zaidi wakiwemo wanaotoka nje ya nchi zikiwemo nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki na Nchi za maendeleo Kusini mwa Jangwa la Sahara (SADC) pamoja na kuanzisha vituo vya umahili ili kuwapa vijana ujuzi utakaosaidia wajiajiri na kujipatia kipato.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi la Chuo Cha Mipango ya Maendeleo Vijijini Profesa Martha Qorro, alisema kuwa ushauri uliotolewa na Mheshimiwa Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mheshimiwa Mwanaidi Ali Khamis utafanyiwa kazi na chuo hicho wakianza na maadili na malezi ya vijana.
Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini Profesa Hozen Mayaya, akitoa taarifa ya ujenzi wa Kituo hicho cha Mafunzo Kanda ya Ziwa -Mwanza, alisema ujenzi wa miundombinu umefikia asilimia 80 ukihusisha kumbi za mihadhara na madarasa.
“Mradi huu unahusisha ujenzi wa majengo mawili ya taaluma kila moja likiwa na ukumbi mmoja wa mihadhara wenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 440 kila mmoja na darasa moja lenye uwezo wa kuchukua wanafuzi 180 pamoja na ofisi 6 zenye uwezo wa kuchukua wafanyakazi 12.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Magu Bw. Salumu Kali, aliishukuru Wizara ya Fedha na Mipango na uongozi wa Chuo cha Mipango kwa kujenga miundombinu ya chuo katika Wilaya yake hatua itakayochochea maendeleo ya wilaya hiyo.
Alisema kuwa wananchi wa Kijiji cha Kitumba, wilayani Magu, walikipatia Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini ezari 20 bure kwa kutambua umuhimu na mchango wa elimu katika taifa na katika wilaya yao yenye idadi kubwa ya wanafunzi wanaohitimu elimu ya msingi na Sekondari wanaohitaji kujiendeleza kielimu.
Pamoja na pongezi hizo alimwomba Mheshimiwa Mwanaidi Ali Khamis kufikisha ombi lake kwa uongozi wa Wizara ya Fedha na Mipango ili wapatiwe zaidi ya shilingi milioni 750 walizoomba kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa ofisi ya Halmashauri ya Wialaya ya Magu.
Post a Comment