Ikulu, Dodoma
Ikulu, Dodoma
Rais Dk. John Magufuli amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Singida Dk. Rehema Nchimbi na viongozi wa Wilaya ya Manyoni kutatua mara moja mgogoro wa ardhi wa eneo la Majengo lililopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni ambao umesababishwa na Idara ya Ardhi ya Halmashauri hiyo.
Rais Magufuli ametoa agizo hilo leo, aliposimama kuwasalimu wananchi wa Manyoni wakati akiwa safarini kutoka Tabora kwenda Dodoma ambapo baada ya kuwasalimu na kuwashukuru kwa kumpigia kura nyingi zilizomwezesha kuwa kwa kipindi cha pili, amesikiliza kero ya ardhi inayowakabili wananchi hao ambao wamelalamikia kitendo cha Idara ya Ardhi kuchukua maeneo yao bila kuwalipa fidia na wengine kuamriwa kuondoka katika eneo hilo baada ya kupewa nyaraka za kupatiwa radhi (Offer) hali iliyozua mgogoro kati ya wamiliki wa asili wa eneo hilo na Idara ya Ardhi.
Rais Magufuli ameagiza wananchi wenye Offer waruhusiwe kuendeleza maeneo waliyopatiwa, na wamiliki wa asili wa eneo hilo kulipwa fidia kwa mujibu wa sheria na kuagiza eneo lililokuwa mali ya Mama mmoja aitwaye Elizabeth Msalali (90) ambalo lilichukuliwa na Afisa Ardhi mmoja aitwaye Msafiri na kisha kupangishwa kwa kampuni ya simu za mkononi ambayo imeweka mnara wa mawasiliano, lirejeshwe mara moja kwa Mama huyo ambaye ndiye ataingia mkataba wa upangaji na kampuni hiyo.
Rais Magufuli ameeleza kutofurahishwa na uelewa mdogo wa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya hiyo Mhe. Jumanne Mlagaza kuhusu masuala mbalimbali ya halmashauri ikiwemo masuala ya kibajeti, miradi na kero za wananchi, na amewataka Madiwani kote nchini kuwa makini na kufuatilia kwa ukaribu masuala yahusuyo halmashauri zao badala ya kuwaachia watendaji wafanye wanavyotaka.
Aidha, Rais Magufuli amewasalimu wananchi wa Bahi Mkoani Dodoma ambapo pamoja na kuwasihi kulima mashamba ya mazao mbalimbali hasa ya chakula ametoa changamoto kwa viongozi wa Wilaya hiyo kuvuna maji ya mvua na kisha kuyasambaza kwa wananchi ili kukabiliana na kero kubwa ya uhaba wa maji unayowakabili.
Post a Comment