Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Abel Makubi
Na Englibert Kayombo WAMJW, Dodoma
Serikali imesema imeweka mkakati wa kusogeza karibu huduma za tiba asili kwa jamii ambazo sasa dawa hizo asilia zinawekewa mikakati ya kupatikana hadi kwenye vituo vya kutolea huduma za afya pamoja na maduka ya kuuza dawa za binadamu.
Hayo yamesewa na Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Abel Makubi mara baada ya kufanya kikao na wazalishaji wa dawa hizo asilia nchini ambao dawa zao zimethibitishwa Usalama na Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali pamoja na Msajili wa Tiba Asili nchini na kukidhi vigezo vya kutumika kwa binadamu.
“Sisi watendaji tumeona ni muhimu kukutana ili tuweze kuweka mikakati ya kuhakikisha hizi dawa asili zinawafikia wananchini kwa urahisi zaidi”amesema Prof. Makubi.
Amesema kuwa tunasumbuliwa na magonjwa ya kuambukiza na yasiyo ya kuambukiza hivyo ni lazima tutumie silaha (dawa asilia na za kisasa) zote ambazo ni salama zinaweza kusaidia wananchi kwa afya.
“Kuna hizi dawa asili zenye usalama, ambazo zimekuwa zikitumika kutibu magonjwa ya kuambukiza na yasiyoambikiza hivyo ni lazima tuzisogeze karibu kwa wananchi kupitia mawakala, maduka ya madawa ya binadamu nata hospitalini kwa usalama ziweze kuwafikia wananchi” ameeleza Prof. Makubi.
Aidha Prof. Makubi amewataka wasomi na wataalam wa afya kwa ujumla kubadili mtazamo wao juu ya tiba asili kwa kuwa zimekuwa na mchango mkubwa wa kutibu magonjwa mbalimbali ya binadamu na kuwaasa wataalam kutokuwa kikwazo kwa wananchi kutumia tiba asili.
“Kama dawa sisi tumeshaihakiki na tukaikubali kwamba hii dawa ni salama, basi pasiwepo na kinyongo au ugumu wowote wa sisi watumishi wa afya kuruhusu mwananchi kutibiwa kwa dawa hiyo ”Amesisitiza Prof. Makubi.
Katika hatua nyingine Prof. Makubi hakusita kuwaasa wananchi kuendelea kuchukua tahadhari zote za kinga za magonjwa magonjwa yote ikiwemo kufanya mazoezi, kubadili mtindo wa maisha na kula chakula bora. Wananchi siyo lazima wasubiri matamko ya Serikali katika kujikinga na magonjwa; njia nyingi za kujikinga na magonjwa zimeshatolewa na wanazijua; kwa hiyo ni suala la wao kujenga mazoea ya kujikinga kila siku ya Mungu.
Prof Makubi alielezea pia umuhimu wa kufanya tafiti zaidi katika tiba asilia ili ziweze kuhakikia kwa miongozo ya nchi na kimataifa na baadae kuweza hata kuhudumia wananchi wa nchi za jirani. Aidha alisisitiza kuwa Wagunduzi watalindwa na Serikali na kuhakikisha umiliki wa ugunduzi wa dawa hizo haupotei wakati na baada ya utafiti.
Naye Dkt. Paul Mhame, Mkurugenzi Msaidizi Tiba Asili kutoka Wizara ya Afya amesema kuwa Serikali kupitia Taasisi zake imeweza kuchambua na kuidhinisha dawa za kunywa aina 5 na dawa aina 4 za mafuta tete kwa ajili ya kujifukiza ambazo zimekidhidi vigezo kuweza kutumika kwa binadamu. Amezitaja dawa hizo za kunywa kuwa ni NIMRICAF, COVIDOL, BINGWA, PLANET ++ pamoja na COVOTANZA huku zile za mafuta tete zikiwa ni BUPIJI pamoja na UZIMA.
“Aidha Serikali inaendelea kufanya kazi kwa karibu na wazalishaji wengine ambao wakikidhi vigezo dawa zao zitaongezwa kwenye orodha hii” Amesema Dkt. Mhame na kuwasisitiza wananchi kujitokeza kwenda kununua dawa hizo kwa ajili ya kujikinga na magonjwa ambukizi na yasiyoambukiza.
Akizungumuza kwa niaba ya wazalishaji wa dawa asili Bw. George Buchafwe ambaye ametengeneza dawa ya kujifukiza kwa mafuta tete ya Bupiji ameishukuru Serikali kwa kuona mchango wao na kuwa sehemu ya kuchangia na kuboresha afya za wananchi.
“Tunaishukuru Serikali kwa kutambua kuwawapo watafiti ambao wanaweza wakaisaidia jamii yetu na ikawezakutoka katika hatua kwenda hatua nyingine kwa kutumia tiba zetu za asili” Amesema Bw. Buchafwe.
Amesema kuwa wao wazalishaji wa dawa za asili wapo tayari kushirikiana na Serikali kuzalisha bidhaa bora ye usalama kwa afya ya binadamu.
Kwa upande wake Dr Otieno kutoka Taasisi ya Tiba Asilia Muhimbili amesisitiza umuhimu wa wananchi kuacha kuchanganya dawa zaidi ya moja kwa wakati mmoja wakati wa kutumia. Amesema ni vema pia wananchi wafuate maelekezo sahihi ya matumizi ya hizi dawa na kuzingatia usalama wake.
Post a Comment